Hamas yapuuza madai kwamba inazuia makubaliano ya amani
16 Januari 2025Afisa wa ngazi za juu wa Hamas Izzat al-Rishq amesema kundi hilo liko tayari kabisa kuyatekeleza makubaliano hayo pamoja na maafisa wengine wawili wa tawi la kisiasa la Hamas, baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kulilaumu kundi hilo kufanya hujuma katika dakika za mwishomwisho za kupatikana kwa makubaliano hayo. Sami Abu Zuhri, ameyapuuzilia mbali na kuliambia shirika la habari la AFP kwamba, madai hayo hayana msingi wowote.
Ni kutokana na hali hiyo, Netanyahu akasema mapema leo kwamba, Baraza la Mawaziri halitayaidhinisha makubaliano hayo hadi pale kundi hilo litakapokuwa tayari kuheshimu kila kipengele kwenye makubaliano hayo. Kulingana na ofisi ya Netanyahu, Baraza hilo halitakutana hadi pale wapatanishi watakapoiarifu Israel kwamba Hamas wamekubaliana na vipengele vyote. Lakini kwa upande mwingine, bado kuna mvutano baina ya vyama vinavyounda serikali ya Israel kuhusiana na hatua hiyo.
Mateka wawili wanaozuiwa kwa muda mrefu kuachiliwa kwanza
Huku hayo yakiendelea, vyombo vya habari vya Israel vimeripoti mchana wa leo kwamba mateka wawili wanaotarajiwa kuachiliwa katika awamu ya kwanza ya makubaliano hayo, walikuwa wakizuiliwa katika Ukanda wa Gaza kwa muda mrefu. Kulingana na ripoti, raia mmoja wa Israel ambaye ana asili ya kiarabu, ambaye pia ana tatizo la afya ya akili, amekuwa akishikiliwa na Hamas tangu mwaka 2015.
Raia mwingine wa Israel ambaye pia ana tatizo kama hilo amekuwa akizuiliwa kizuizini katika Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2014. Ripoti hiyo imesema, wanaume hao hawakutekwa wakati wa shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023, lakini walivuka mipaka hadi pwani ya ukanda huo
Israel imechapisha picha za mateka huyo wa kwanza aliyelala kitandani huku akiwa amevaa kifaa cha kumsaidia kuvuta Oksijeni. Picha hiyo ilipigwa mwaka 2022 na picha ya mateka wa pili ilipigwa mwaka 2023 ambazo kwa pamoja ziliibua ghadhabu nchini Israel.
Soma pia:Mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya vita vya Gaza yako hatua za mwisho
Makubaliano ya jana Jumatano yaliyotangazwa na Qatar yanasema mateka 33 kati ya 98 waliosalia mikononi mwa Hamas wanatarajiwa kuachiliwa katika awamu ya kwanza ya wiki sita.
Umoja wa Ulaya watoa msaada mpya kwa ajili ya Ukanda wa Gaza
Mjini Brussels, Umoja wa Ulaya umetangaza kupeleka yuro milioni 120, katika msaada mpya kwa Gaza. Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Eva Hrncirova amewaambia waandishi wa habari kwamba msaada huo unaloenga kushughulikia mzozo wa kibinaadamu kwenye eneo hilo la Palestina.
Soma piaRais Biden azisifu sera zake za nje akijiandaa kuondoka madarakani:
"Leo hii tunaidhinisha kifurushi cha yuro milioni 120 kwa ajili ya Gaza ili kushughulikia mzozo wa kibinadamu unaoendelea huko. Tunajua kuwa hali huko ni ya kusikitisha. Tunajua kuwa Wapalestina wanahitaji haraka lishe, vifaa vya matibabu, malazi na ulinzi. Tunatumai tutaweza kuwasilisha kifurushi hiki, kwa kushirikiana na washirika wetu, tunataka kushughulikia dharura muhimu zaidi na kusaidia Wapalestina."
Msemaji mwingine wa Halmashauri hiyo Anouar El Anouni amesema umoja huo unatarajia makubaliano ya kusitishwa mapigano yaliyofikiwa yatachochea pakubwa misaada hiyo kufikishwa Gaza na kufikishwa kikamilifu kwa wahitaji.
Waziri Mkuu wa Palestina Mohammed Mustafa yuko mjini Brussels kwa ajili ya mikutano na maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Antonio Costa, aliyekuzungumza naye hii leo na mkuu wa sera za kigeni Kaja Kallas, atakayekutana naye kesho.
Na huko mjini Moscow, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Maria Zakharova amezungumzia makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na kusema Urusi inataraji yatasaidia kuleta utulivu wa kikanda. Urusi inakuwa taifa la karibuni zaidi lenye nguvu kuzungumzia makubaliano hayo. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, ameongeza kuwa hatua hiyo itakuwa msingi wa kuanzishwa kwa mchakato wa utatuzi wa kina wa kisiasa wa tatizo la Palestina.
Shirika la ndege la Lufthansa limetangaza kurejesha safari zake mjini Tel Aviv kuanzia Febriari Mosi. Shirika hilo lilisitisha safari zake mjini humo kutokana na mzozo kati ya Hamas na Israel.