1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la kigaidi la Al Shabaab lavamia kambi ya polisi Kenya

Saumu Ramadhani Yusuf31 Machi 2010

Maafisa kadhaa wa Usalama wajeruhiwa huko Liboi

Wanamgambo wa kiislamu wamekuwa kitisho kikubwa cha usalama pembe ya AfricaPicha: AP

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kisomali wamevamia kambi moja ya jeshi la polisi la Kenya katika eneo  la mpaka kati ya Kenya na Somalia  na kuwajeruhi maafisa kadhaa wa polisi:Taarifa zilizotolewa na afisa mmoja wa ngazi ya juu ambaye hakutaka kutaja jina,zinasema kwamba watu hao wanashukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la Al Shabaab kutoka Somalia na wanaendelea kutafutwa.

Kwa mujibu wa afisa huyo ni kwamba watu hao waliivamia kambi ya kikosi cha polisi wa usalama huko Liboi  karibu na mpaka baina ya Kenya na Somalia wakiwa wamejihami kwa silaha mbali mbali na kuanza kufyetua risasi ambapo waliwajeruhi maafisa kadhaa wa usalama wa Kenya.

Hata hivyo afisa huyo ameongeza kusema kwamba maelezo zaidi kuhusiana na kisa hicho hayajatolewa ingawa wanachofahamu ni kwamba hakuna mtu aliyeuwawa kwa upande wa maafisa wa Kenya.Hatua hiyo ya uvamizi wa wanamgambo wa Al Shabbab katika ardhi ya Kenya imekuja baada ya kundi hilo linalofungamanishwa na mtandao wa kigaidi wa Alqaeda mara kadhaa  kutishia kuishambulia Kenya ambayo inaiunga mkono serikali dhaifu ya Somalia ambayo wanamgambo hao wamekuwa wakiipiga vita kutaka kuiangusha madarakani.

Jeshi la Serikali dhaifu ya Somalia linasaidiwa na Umoja wa Afrika kukabiliana na wanamgambo wenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al QaedaPicha: AP

Mnamo mwezi wa Januari kundi hilo la Al Shabaa lilitoa taarifa za kutishia kuivamia Nairobi kulipiza kisasi hatua iliyochukuliwa na polisi ya kuwavamia waandamanaji wa kiislamu waliokuwa wanapinga kukamatwa kwa kiongozi wa kidini kutoka Jamaica  aliyeingia nchini humo kwa njia za utata.-

Serikali ya Kenya ambayo inapakana na Somalia katika eneo la kaskazini mashariki ambayo imejitolea kuwasaidia wanajeshi wa serikali ya Somalia katika mapambano dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali nchini Somalia,imeshazungumzia mara kadhaa juu ya hofu kwamba wanamgambo hao wa Al Shabaab wanaojitoa muhanga kwa kujiripua mabomu huenda wakaivamia Kenya.

Wakati hayo yakiarifiwa,afisa mmoja wa ngazi ya juu  wa Marekani anayehusika na masuala ya wakimbizi amesema kwamba utawala wa rais Obama unawasiwasi kuhusu ripoti zilizotolewa kwamba makambi ya wakimbizi huko mashariki ya Kenya yanatumiwa kama maeneo ya kuwakusanya wapiganaji katika makundi yanayopambana nchini Somalia.Afisa huyo,Reuben Brigety amesema vitendo kama hivyo vinasababisha kukosekana hali ya kuaminika kwa makambi ya Dadaab huko nchini Kenya.

Al Shabaab latuhumiwa kuchukua mamia ya wakimbizi kutoka kambi ya Dadaab Kenya na kuwaingiza vitaniPicha: AP

Shirika la Habari la AP  mnamo mwishoni mwa mwaka uliopita lilitoa ripoti kwamba maelfu ya watu wakiwemo watoto wamekuwa wakichukuliwa kwa siri  na kupewa mafunzo ndani ya Kenya kwa lengo la kupambana na wanamgambo wa kiismali nchini Somalia. Ingawa ripoi hizo zimekanushwa na maafisa kutoka pande zote mbili Kenya na Somalia.Kutokana na kuzidi kutokota kwa hali ya mapambano nchini Somalia na kitisho cha wanamgambo katika eneo hilo,maafisa wa Marekani wamefahamisha kwamba wizara ya Ulinzi inafikiria kupeleka ndege maalum za uchunguzi  zisizohitaji rubani pamoja na msaada mwingine wa  kijeshi nchini Somalia kwa  ajili ya kuimarisha harakati za serikali ya nchi hiyo za kukabiliana na wanamgambo hao wanaohusiana na Al Qaeda.

Maafisa wa Marekani wanaohusika na masuala ya Ulinzi pamoja na wanadiplomasia wa nchi za magharibi wamefanya mikutano hii leo kuhusiana na hali ya usalama nchini Somalia.

Mwandishi :Saumu Mwasimba/APE

Mhariri :Abdul-Rahman.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW