HRW lataka uchunguzi wa mauaji baada ya mapinduzi, Kongo
27 Mei 2024Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeelezea hofu yake leo juu ya "madai ya mauaji ya kiholela" yaliyofanyika baada ya jaribio la mapinduzi lililotibuliwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Shirika hilo lililo na makao yake mjini New York, Marekani, sasa limetoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kufanya uchunguzi kuhusiana na madai hayo.
Human Rights Watch linasema limepata mkanda wa video uliochukuliwa na majeshi ya Kongo unaoonesha watu wanaodhaniwa kuhusika katika jaribio hilo la mapinduzi wakifyatuliwa risasi karibu na makao makuu ya rais.
Kulingana na msemaji wa jeshi Jenerali Sylvain Ekenge, karibu watu 40 walikamatwa huku wengine 4 waliuwawa. Ekenge alisema kwamba njama hiyo iliongozwa na Christian Malanga, raia wa Kongo mzaliwa wa Marekani, ambaye ni mmoja wa waliouwawa.