Mataifa masikini yaidai G7 yuro trilioni 13.
18 Mei 2023Kundi la mataifa ya kidemokrasia yaliyoendelea kiviwanday, G7 yanadaiwa na nchi maskini zaidi ya Euro trilioni 13 za misaada yaliouahidi katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, hayo yakiwa ni kulingana na makadirio ya shirika la Oxfam.
Soma pia:Viongozi wa Kundi la Nchi saba tajiri duniani wanakusudia kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusi
Kabla ya mkutano wa kilele wa G7 uliofanyika Ijumaa mjini Hiroshima nchini Japan, shirika la Oxfam limesema kuwa badala ya mataifa hayo tajiri ya G7 na benki zao kutimiza wajibu wao, zimegeukia kudai kulipwa madeni kwa kiasi cha Euro milioni 232 kwa siku.
Kaimu mkurungenzi mtendaji wa shirika la Oxfam Amitabh Behar anasema mataifa hayo tajiri yanapenda kujionesha kama waokoaji lakini ukweli ni kuwa utendaji wao ni wa undumilakuwili, kwa kujiwekea aina ya mfumo zinaoutumia zenyewe, na kulazimisha mfumo tofauti kwa mataifa ambayo yalikuwa makoloni yao.
Madeni hayo ni ya muda mrefu
Mataifa hayo tajiri yanadaiwa na mataifa yanayoendelea ya kusini mwa dunia msaada yalioahidi miongo kadhaa iliyopita lakini hawakutoa gharama hizo zinazotokana na uharibifu wa hali ya hewa kufuatia utoaji wa hewa chafu ya ukaa na utajiri mkubwa uliopatikana wakati wa utumwa.
Soma Zaidi:Mawaziri wa G7 wajadili namna ya kuepusha athari iwapo Marekani itashindwa kulipa deni lake la taifa
Shirika hilo la Oxfam linaeleza kuwa mkutano unafanyika wakati ambapo kuna punguzo kubwa la mishahara ya wafanyakazi, kupanda kwa kasi kwa bei ya chakula na ongezeko la njaa duniani. Oxfam inaongeza kuwa ni kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 25 ambapo utajiri umeongezeka maradufu na umaskiri ulokithiri ukiongezeka kwa wakati mmoja.
Mataifa ya G7 yalivunja ahadi yao wenyewe ya kutoa bilioni 100 kwa mwaka kusaidia nchi maskini katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kuongeza uzalishaji wao wa Kaboni unaokadiriwa kusababisha hasara na uharibifu wa Euro trilioni 8.7 katika nchi za kipato cha chini na kipato cha kati.
Mwaka 1970 nchi tajiri duniani ziliahidi kutoa asilimia 0.7 ya pato la kiuchumi kila mwaka kwa misaada ya maendeleo lakini trilioni 4.49 hazijatolewa ambayo ni zaidi ya nusu ya ahadi hiyo.
Mkurungenzi mtendaji wa Oxfam anasema pesa hizo zingeweza kuleta mabadiliko ikiwemo kuboresha elimu, afya, maji , kilimo,usalama na mambo mengine zaidi hivyo ni lazima nchi hizi tajiri duniani zilipe madeni hayo.
Chanzo: DPA