Kundi la Taliban laudhibiti mji mkuu wa kwanza
7 Agosti 2021Roh Gul Khairzad, naibu gavana wa jimbo la Nimroz amenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa AFP akisema anathibitisha mji mkuu wa jimbo hilo wa Zaranj, upo katika udhibiti wa Taliban.
Amesema mji huo ulio kusini/magharibi mwa Afghanistan, karibu na mpaka wa Iran umedhibitiwa bila ya kutokea mapigano yoyote na katika mitandao ya kijamii kuna video zisizokuwa na uthibitisho zikiwaonesha wanamgambo wa kirandaranda mitaani.
Mji wa Zaranj umetajwa kuwa katika kitisho kwa muda mrefu.
Ingawa mji huo sio muhimu kimkakati, lakini kuanguka kwake kunatajwa kuwa ni hatua ya kuikatisha tamaa serikali, ambayo kwa kiasi kikubwa imevurugwa na harakati za wanamgambo hao katika jitihada yake ya kulinda miji mikuu. Khairzad amesema jiji hilo limekuwa katika kitisho kwa muda mrefu, lakini hakuna yeyote katika serikali kuu ambae alikuwa akiwasikiliza walipokuwa wakieleza wasiwasi wao.
Katika ujumbe wake wa Twitter wa awali, Taliban iliandika imedhibiti majengo ya kimkakati, likiwemo la utawala na makao makuu ya polisi.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan asema hali ilivyo inatishia janga.
katika hatua nyingine, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Afghanistan, Deborah Lyons ametoa wito kwa Taliban kusitisha mashambulizi yake mara moja dhidi ya miji mikubwa akionya hali ilivyo inalipeleka taifa hilo katika janga zaidi.
Akizungumza na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye mataifa 15 wanachama kwa njia ya video mjumbe huyo amesema baraza hilo lazima litoe kauli isiyo na mashaka mashambulizi hayo lazima yasitishwe kwa wakati huu.
Mapigano ya muda mrefu nchini Afghanistan yameongezeka zaidi, tangu Mei, pale ambapo majeshi ya kigeni yalipoanza hatua ya mwisho ya kujindioa nchini humo,ambayo inataeajiwa kukamilika baadae mwezi huu.
Chanzo: AFP