RSF yadai kuudhibiti kikamilifu mji wa El-Fashir
27 Oktoba 2025
Taarifa ya kundi hilo imetolewa Jumapili saa kadhaa baada ya kutangaza kuwa linaidhibiti kambi kuu ya jeshi katika mji huo ambao liliuzingira tangu mwezi Mei mwaka 2024.
Taarifa iliyotolewa na kundi la RSF imesema imeutwaa mji huo kutoka mikononi mwa mamluki na wanamgambo, likimaanisha jeshi la Sudan ambalo limekuwa likipambana nao tangu mwaka 2023.
Mji huo mkubwa ndio wa mwisho ambao haukuwa mikononi mwa RSF huko magharibi mwa Darfur na umekuwa haufikiki kwa urahisi kutokana na mapigano makali.
Taasisi inayohusika na kulinda afya na usalama wa watu walioathiriwa na mizozo ya Chuo kikuu cha Yale HRL imethibitisha kupitia picha za satelaiti kuwa wanamgambo wa RSF walisonga mbele kwenye mji huo, hadi katika kambi kubwa ya jeshi na mapigano makali yalitokea.
Video zilizochapishwa Jumapili na wanamgambo hao zimewaonesha wapiganaji wakisherehekea kando kando ya bango lililoandikwa kikosi cha sita wakati picha nyingine za video ziliyaonesha makundi ya watu wakishangilia sambamba na wapiganaji wa RSF.
Wakati kukiwa na mapambano makali, Shirika la kitabibu la Sudan Doctor Network, limesema vikosi vya RSF vimewaua makumi ya watu na kuharibu vituo vya afya jana Jumapili.
Baada ya taarifa za kutwaliwa kwa mji huo , Gavana wa Darfur mwenye mafungamano na jeshi la Sudan Minni Minnawi ametoa wito wa kuhakikishiwa "ulinzi kwa raia" muda mfupi baada ya wanamgambo wa RSF kudai kuwa wameudhibiti mji huo. Minawi ametaka pia hatma ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao iwekwe wazi.
Amedai pia ufanyike uchunguzi huru kuhusu ukiukwaji na mauaji ya kimbari yaliyofanywa kwa kificho na makundi ya wanamgambo ambao wamekuwa kwenye mapambano makali na jeshi tangu mwezi Aprili mwaka 2023
Guterres aonya hali itazidi kuwa mbaya Sudan
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuhusu kuendelea kuchochewa kwa mapigano katika mji El Fasher na kuongeza kwamba hali inayoshuhudiwa Sudan haivumiliki.
Nayo Ofisi ya uratibu wa misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa OCHA imeripoti kuwa maelfu ya watu wamekwama katika eneo lenye machafuko la El Fasher huku wakikabiliwa na njaa bila huduma za afya chakula na hawana usalama.
Zaidi, mratibu wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa Tom Fletcher ametahadharisha kwamba ameshtushwa na kiwango kikubwa cha majeruhi na raia waliolazimika kuyahama makazi yao. Ametoa wito wa kusitisha haraka mapigano na kuruhusu njia salama ili wapate misaada.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 300,000 wanaishi katika mazingira hatari kwenye mji wa El-Fasher ambako haufikiki kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.