1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kupungua kwa misaada kwadhoofisha mapambano ya Ebola DRC

30 Mei 2026

Kupunguzwa kwa misaada ya maendeleo kumechangia kushindwa kudhibiti mlipuko wa Ebola nchini DR Congo. Mashirika ya Ujerumani yanataka kuongezwa kwa fedha za dharura ili kuzuia ugonjwa huo kuenea zaidi.

DR Kongo Rwampara 2026 | Wahudumu wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakifanya usafishaji wa hospitali kwa dawa za kuua vijidudu kutokana na mlipuko wa Ebola
icha ya hatua za kudhibiti ugonjwa huo, Ebola inaendelea kusambaa ndani ya DRCPicha: Gradel Muyisa Mumbere/REUTERS

Mlipuko wa Ebola unaendelea kuongezeka katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa na vifo 220 vikiripotiwa hadi sasa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lina hofu kwamba virusi hivyo vitaendelea kusambaa nchini DRC.

"Tunakabiliwa na mlipuko mkubwa na mgumu sana. Hali itazidi kuwa mbaya kabla ya kuanza kuimarika," alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, mapema wiki hii.

Shirika hilo linataka kutoa msaada wa haraka katika maeneo yaliyoathirika kwa kutuma vifaa na wataalamu wa afya.

Hata hivyo, fedha za WHO ni chache, hasa baada ya Marekani kujiondoa katika shirika hilo. Marekani ilikuwa mfadhili wake mkubwa zaidi. Upungufu huo wa fedha umeilazimisha WHO kupunguza au hata kusitisha baadhi ya programu zake, ikiwemo nchini DRC.

Ingawa kwa sasa Ujerumani ndiyo mfadhili mkubwa zaidi wa WHO, nayo imepunguza michango yake. Aidha, imepunguza bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ) kwa mwaka huu.

"Bajeti ya mwaka 2026 inaonyesha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa Wizara ya Afya na Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ) zimepunguzwa," amesema Julia Stoffner, mtaalamu wa sera za afya katika shirika la misaada la Kiprotestanti la Ujerumani, Brot für die Welt.

Kupunguzwa huku kwa bajeti kunajumuisha pia michango ya hiari kwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kwa mujibu wa Julia Stoffner, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ) imekuwa ikipunguza ufadhili wa programu za afya kwa miaka kadhaa.

Akizungumza na DW, Stoffner amesema: "Mifumo ya afya katika nchi za Kusini mwa Dunia inapodhoofika zaidi na zaidi au inapokosa kuungwa mkono, hali hiyo huchangia milipuko kama huu wa DRC kutogunduliwa kwa muda mrefu kabla ya kubainika."

Mtaalamu wa afya duniani, Julia Stoffner, amesema kupunguzwa kwa bajeti za misaada kunadhoofisha juhudi za kukabiliana na milipuko ya magonjwa kama EbolaPicha: Bernd Riegert/DW

Shirika la misaada ya kibinadamu la CARE pia limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uwekezaji katika misaada na elimu ili kukabiliana na changamoto hizo.

Nalo shirika la ustawi la Kikatoliki la Caritas limechapisha wito kama huo, likitaka kuongezwa kwa msaada wa kimataifa ili kusaidia kukabiliana na mlipuko wa Ebola na kuimarisha huduma za msingi za jamii zilizoathirika.

Fedha hazitoshi kupambana na Ebola

Josue Ibulungu anaongoza ofisi ya shirika la misaada la Kijerumani la Diakonie Katastrophenhilfe mjini Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Anajaribu kuratibu msaada kwa watu walioathiriwa na mlipuko wa Ebola, lakini anasema ni asilimia 30 tu ya mahitaji yanayoweza kufikiwa kwa sasa.

"Hali ni ngumu sana kwa wafanyakazi wote wa misaada ya kibinadamu. Kupunguzwa kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili wengi kumefanya hali kuwa mbaya zaidi. Mashirika mengi yanahangaika hata kupata fedha za kuwezesha chanjo dhidi ya Ebola," ameiambia DW.

Ibulungu ameongeza kuwa hospitali nyingi zimeharibiwa kutokana na vita.

"Hii inafanya iwe vigumu kwa madaktari na wauguzi kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kwa sababu wanakosa vifaa muhimu vya matibabu," amesema.

Kwa miongo kadhaa, eneo la mashariki mwa DRC limekumbwa na mapigano kati ya jeshi la serikali, wanamgambo, waasi na makundi ya uhalifu yanayowania udhibiti wa eneo hilo. Migogoro hiyo inachochewa na ushindani wa rasilimali za asili, migogoro ya kikabila pamoja na maslahi ya kisiasa ya Rwanda na Uganda.

Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ) imesema serikali ya DRC imepokea takribani euro milioni 160 za misaada ya maendeleo kwa miaka ya 2026 na 2027. Kiasi hicho ni kidogo kuliko kilichotolewa katika miaka iliyopita kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa miaka kadhaa mfululizo.

Msemaji wa BMZ, Benedikt Schöneck, amesema kuzuia magonjwa si kipengele kimoja maalumu katika bajeti ya wizara hiyo, bali hushughulikiwa kupitia programu mbalimbali.

"Kwa kuangalia siku zijazo, ni wazi kwamba kupunguzwa kwa fedha za kuzuia magonjwa kutakuwa na athari zake," amesema.

Josue Ibulungu asema wahudumu wa afya na madaktari walioko mstari wa mbele wanakabiliwa na shinikizo kubwaPicha: Kerem Uzel/Diakonie Katastrophenhilfe

Aidha, Schöneck amesema Ujerumani inaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha mipango ya kimataifa inapata uhakika wa kifedha katika miaka ijayo, ingawa hakutaja kiwango halisi cha fedha hizo.

Amesisitiza kuwa licha ya kupungua kwa bajeti, BMZ imejizatiti kuendelea kutoa msaada wa kuaminika katika juhudi za kuzuia milipuko ya magonjwa. Wizara hiyo pia inapanga kutuma kundi la wataalamu mashariki mwa DRC au kuanzisha timu ya kudumu katika eneo hilo kwa lengo la kuwafundisha wahudumu zaidi wa misaada.

Wito wa kuongeza msaada

Shirika la misaada la Kiprotestanti la Ujerumani Brot für die Welt linataka kuongezwa kwa kiasi kikubwa kwa ufadhili wa kupambana na mlipuko wa Ebola. Julia Stoffner amesema mavazi 500 ya kujikinga yaliyoahidiwa na BMZ hayatoshi kukabiliana na hali iliyopo.

"Ufadhili wa juhudi za afya duniani kwa ujumla unapaswa kuongezwa," amesema.

Ameongeza kuwa mashirika ya kiraia yanayofanya kazi katika maeneo husika yanapaswa kuimarishwa kwa sababu ndiyo yanayofahamu vizuri zaidi mahitaji ya wananchi na mazingira ya maeneo hayo.

Bajeti ya Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Reem Alabali Radovan, imepunguzwa kwa kiasi kikubwaPicha: Ronka Oberhammer/DW Images

"Yana uhusiano wa karibu na jamii na yanaaminiwa na wananchi. Ushirikiano wa wananchi wa maeneo yaliyoathirika ni muhimu sana katika kudhibiti mlipuko huu, hasa kwa kuwa hakuna chanjo inayopatikana kwa sasa," amesema.

Aina ya virusi vya Ebola ya Bundibugyo, ambayo haina chanjo wala tiba maalumu, ndiyo inayosababisha mlipuko huo mashariki mwa DRC. Gisela Schneider wa Taasisi ya Ujerumani ya Misheni za Tiba amesema juhudi za chanjo dhidi ya aina hiyo ya virusi zitachukua angalau miezi tisa.

Kwa sasa, amesema, kuna uhaba mkubwa wa vifaa vya kupima kwa haraka pamoja na maabara za kufuatilia na kubaini maambukizi ya virusi hivyo.

Kituo cha kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kilichomwa moto mjini Rwampara mashariki mwa DRC baada ya ndugu wa marehemu kutaka kumzika mwanafamilia waoPicha: Xinhua/IMAGO

Waziri wa zamani wa Afya wa Ujerumani, Karl Lauterbach, ambaye alikuwa madarakani wakati wa janga la COVID-19, pia ametaka kuongezwa kwa misaada ya maendeleo ili kusaidia kupambana na milipuko ya magonjwa.

Amesema kudhibiti kuenea kwa magonjwa barani Afrika si wajibu wa kibinadamu pekee, bali pia ni jambo lenye maslahi kwa Ulaya.

"Mifumo ya afya inapoendelea kudhoofika, hali hiyo inaweza kusababisha ongezeko kubwa la wakimbizi kutoka nchi za Afrika kuelekea Ulaya," ameliambia gazeti la Rheinische Post.

Lauterbach ameongeza kuwa wito wa baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa kulia wa kupunguza zaidi misaada ya maendeleo ni wa makosa na unaweza kuleta madhara makubwa baadaye.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW