1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Kura nyingine ya Baraza la Usalama la UN kuhusu Gaza

20 Novemba 2024

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa watapiga kura kwa mara nyingine tena Jumatano juu ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Libanon | Israelischer Luftangriff in Hadath
Picha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura Jumatano kuhusu rasimu nyingine ya azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza katika majaribio yake ya hivi punde ya kuongeza shinikizo la kumaliza vita.

Hata hivyo uteuzi wa maneno katika rasimu hiyo umeighadhabisha Israel na kuzusha hofu kwamba huenda Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel ikatumia kura yake ya turufu kuizuia.

Rasimu ya hivi punde ya azimio hilo inataka "kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti yoyote katika vita kati ya Israel na kundi la Hamas na pia kuachiliwa mateka wote mara moja bila masharti.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon amesema maneno yaliyotumika ni ya "aibu” akiongeza kwamba hawawezi kuuruhusu Umoja wa Mataifa kuifunga mikono ya Israel dhidi ya kuwalinda raia wake, na kwamba hawataacha kupigana hadi mateka waliokamatwa warudi nyumbani.

Mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Gaza

Hayo yakijiri, mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya watu 15 kaskazini mwa Gaza.

Unaweza pia kusoma Israel yatakiwa kutekeleza hatua za kusitisha mapigano Gaza

Hayo yameelezwa na wakaazi pamoja na maafisa wa afya wa ukanda huo unaodhibitiwa na kundi la wanamgambo wa Hamas.

Matabibu wamesema watu wasiopungua 12 wameuwawa baada ya Israel kuishambulia nyumba moja kwenye eneo la Jabalia, kaskazini mwa Gaza na kwamba watu wengine 10 bado hawajapatikana na kazi ya kuwatafuta inaendelea. 

Kwenye kitongoji cha Sabra, Idara ya Huduma za Dharura imesema mfanyakazi wake mmoja ameuawa kufuatia shambulizi la anga la Israel lililoulenga msafara wao. 

Wakaazi wa maeneo ya Jabalia, Beit Lahiya na Beit Hanoun, ambako jeshi la Israel linaendesha operesheni zake tangu mwezi uliopita, wamearifu kwamba vikosi hivyo vimeripua nyumba kadha kwenye maeneo matatu.

Kura ya turufu katika Baraza la Usalama

Tangu mzozo huo uanze, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likitatizika kuzungumza kwa sauti moja kwa sababu kwa mara kadhaa Marekani imekuwa ikitumia kura yake ya turufu dhiid ya baadhi ya mapendekezo, sawa na Urusi na China.

Maazimio machache ambayo Marekani iliruhusu kupitishwa kwa kutopiga kura, hayakutoa wito wa usitishwaji mapigano kabisa bila masharti.

Unaweza kusoma pia: HRW: Israel yalaumiwa kwa kutenda uhalifu wa kivita

Vita vya Gaza vilianza baada ya shambulizi la Oktoba 7, 2023 la wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel na kuua watu 1,200 ambapo pia waliwateka watu 250 na kuwapeleka Gaza. Inakadiriwa kuwa mateka 100 wangali mikononi mwa Hamas, kundi ambalo Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliorodhesha kuwa la kigaidi.

Vita hivyo vilitanuka pia hadi Lebanon ambapo Israel inapambana na wanamgambo wa Hezbollah wanaounga mkono Hamas.

Makubaliano ya usitishaji vita Lebanon yakaribia

Katika tukio jingine, mjumbe wa Marekani Amos Hochstein, amesema wanakaribia kufikia mapatano ya usitishaji vita baada ya mazungumzo kule Lebanon.

Mwakilishi wa Marekani katika mzozo kati ya Israel na Lebanon Amos Hochstein (Kushoto) akizungumza na Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati Novemba 19, 2024 mjini Beirut.Picha: Lebanese Prime Minister's Press Office/AFP

Ufaransa pia imesema kuna matumaini kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano Lebanon yanaweza kafikiwa. 

Hochstein ambaye anauwakilisha utawala wa Rais Joe Biden kutafuta suluhisho la mzozo kati ya Israel na Lebanon, aliwasili Beirut mnamo wakati washirika wa Hezbollah katika serikali ya Lebanon wamesema wanamgambo hao wamejibu vyema pendekezo la usitishaji vita.

Pendekezo hilo linaainisha kwamba wapiganaji wa Hezbollah na wanajeshi wa Israel wataondoka katika eneo la ulinzi la Umoja wa Mataifa, kusini mwa Lebanon.

Eneo hilo litasimamiwa na maelfu zaidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na vikosi rasmi vya jeshi la Lebanon.

Israel imependekeza utaratibu wenye nguvu zaidi, ikiwemo uwezekano wa kufanya operesheni ya kijeshi dhidi ya vitisho vya Hezbollah, wito ambao huenda Lebanon itaupinga.

Mnamo Jumanne, Jeshi la Lebanon lilisema Israel ilifanya mashambulizi ya anga kuilenga kambi ya jeshi lake kusini mwa mji wa Sarafand ambalo wanajeshi watatu waliuliwa.

KWa mengi zaidi, bofya hapa: Mzozo wa Israel na Hamas

(Vyanzo: RTRE, AFPE, APE)