1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya Maoni: Chama cha AfD kuingia bungeni

18 Septemba 2017

Kura ya maoni ya hivi karibuni inaonesha kuwa AfD itapata asilimia 12. Uwezekano wa chama hicho kuingia bungeni umeibua wasiwasi miongoni mwa vyama vingine. AfD inapinga wahamiaji.

Deutschland Alexander Gauland von der der AfD in Potsdam
Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Baada ya zaidi ya  nusu karne, chama cha siasa kali cha mrengo wa kulia nchini Ujerumani AFD kinatarajiwa kuingia bungeni. Chama hicho kimesema kitashinikiza adhabu kali kutolewa dhidi ya Kansela Angela Merkel kwa kuwafungulia milango wakimbizi na wahamiaji. Kura ya maoni ya hivi karibuni imeonesha kuwa chama cha AFD kimeimarika kwa asilimia 12.

Huenda chama kinachoitwa chama mbadala kwa Ujerumani AFD, kikawa chama cha tatu kwa ukubwa katika bunge la Ujerumani kwa asilimia 12 ya kura zitakazopigwa Septemba 24. Hayo ni kwa mujibu wa kura ya maoni ya hivi karibuni ya Sonntagstrend iliyofanywa na taasisi ya Emnid.

Takwimu hiyo ni chini ikilinganishwa na vyama vingine vyenye misimamo mikali katika nchi za Ulaya. Mfano nchini Ufaransa, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachoongozwa na Marine Le Pen kilipata asilimia 34 ya kura katika uchaguzi uliofanywa mwezi Mei na nchini Uholanzi, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachoongozwa na Geert Wilders kilipata asilimia 13 katika uchaguzi uliofanywa mwezi Machi.

Leif-Erik Holm, ambaye ni mbgombea wa chama cha AfD katika eneo bunge la Merkel akiwa na wanachama wengine wa AfDPicha: DW/K.-A. Scholz

AfD yatengwa na vyama vingine

Uwezekano wa kuingia bungeni chama ambacho waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amekitaja kuwa ni sawa na Wanazi kuingia katika kitovu cha demokrasia ya Ujerumani yaani bunge, umeibua wasiwasi miongoni mwa vyama. Vyote vimekataa kushirikiana na AfD, na hakuna hata mbunge mmoja anayetaka kukaa karibu na wawakilishi wao bungeni. Christian Lindner mwenyekiti wa chama cha FDP kinachowania pia nafasi ya tatu dhidi ya AFD amesema watafanya bidii kuwa chama cha tatu kiushawishi bungeni. "Ni kinyang'anyiro cha nafasi ya tatu katika nchi yetu kati ya wanademokrasia huru na AfD. Tutapigana kuwa chama katika nafasi ya tatu, kwa sababu haikubaliki kwa chama kinachotambuliwa na maamuzi ya kiimla nchini kuwa suluhisho kwa muungano mwingine mkuu."

Mgombea mkuu wa AfD Alexander Gauland amepinga kuitwa Wanazi. Ameongeza kuwa watu wanatumia jina hilo kwa sababu ya umaarufu wa chama. Chama hicho kimepata uungwaji mkono kufuatia wito wake wa kutaka Ujerumani kufunga mipaka yake, kuanzisha mfumo wa kuwarejesha wakimbizi makwao na kukomesha wakimbizi kuleta familia zao Ujerumani.

Pingamizi dhidi ya wahamiaji

Akiuhutubia mkutano wa hadhara katika mji ulioko mpakani mwa Poland wa Frankfurt Order, huku wimbo wenye ujumbe wa "Tutatarudisha furaha katika nyumba zenu ukiimbwa" Gauland aliuambia mkutano huo kuwa "Tunazidi kuwa wakimbizi katika nchi yetu" Mwanasheria  huyo mwenye umri wa miaka 76 aliongeza kusema Ujerumani ni ya Wajerumani, Uislamu hauna nafasi  katika nchi hii na ongezeko la wahamiaji litamfanya kila mmoja kuwa mbaya zaidi.

Wafuasi wa AfD wakiandamana dhidi ya Merkel katika kampeni eneo la Bitterfeld-WolfenPicha: picture-alliance/dpa/H. Schmidt

Katika hafla nyingine, Gauland alisababisha ghadhabu aliposema kuwa Wajerumani hawapaswi tena kuzungumziwa kwa msingi wa Unazi wa kale, bali wanapaswa kuwa na fahari kuhusu mafanikio ya wanajeshi wake wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza na Pili  vya dunia.

Wanazi waliitawala Ujerumani kati ya mwaka 1933 na 1945 wakati ambapo waliwaua Wayahudi milioni sita katika mauaji ya kimbari ya Holocaust kando na kuvamia nchi nyingine za Ulaya.

Shinikizo la adhabu kali kwa Kansela Merkel

Huenda chama cha AfD ambacho pia kimemtaka waziri wa uhamiaji kufukuzwa Ujerumani na kupelekwa Uturuki ambako ni chimbuko la wazazi wake, kikawa chama kikubwa zaidi cha upinzani katika bunge la taifa endapo kutakuwa na marudio ya muungano wa sasa kati ya chama cha Merkel CDU na washirika wake wa Kisosholisti SPD.

Itamaanisha kuwa AfD itasimamia kamati muhimu ya bajeti, itaanzisha mjadala mkuu katika mashauriano ya bajeti, na itatoa kipaumbele katika sera zake kama sera mbadala dhidi ya sera za serikali.

Gauland ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa akishachaguliwa atataka kamati ya kumchunguza Kansela Merkel kwa kuwaruhusu watu milioni moja humu nchini na aadhibiwe vikali.

Mwandishi: John Juma/RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu