Yaliyomo Magazetini
23 Februari 2016Tuanzie Uingereza na kizungumkuti cha kura ya maoni kama nchi hiyo iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya au la. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Kambi ya wanaopigania Uingereza itoke katika Umoja wa ulaya,ikitanguliwa na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Ukip,kinaeneza hofu dhidi ya wahamiaji wasiodhibitiwa. Waziri mkuu David Cameron anataka kujaribu kutuliza jazba katika majadiliano yanayoendelea na kwa namna hiyo kuwatanabahisha wapiga kura wenye misimamo wa wastani,juu ya umuhimu wa Uingereza kuendelea kuwa mwanachama wa Umoja wa ulaya. Anatahadharisha dhidi ya ya hatari inayoweza kutokea pindi Uingereza ikijitoa katika umoja huo. Anategemea waengereza watamwelewa. Mbinu hizo zilisaidia pia katika kura ya maoni iliyopita kuhusu suala kama Scotland ijitenge au iendelee kuwa sehemu ya Umoja wa Ufalme wa Uingereza.
Hisia za chuki dhidi ya wageni katika jimbo la mashariki la Saxony
Vituko vilivyotokea wiki iliyopita katika jimbo la mashariki la Saxony ambako moto ulioripuka katika kituo cha kuwapokea wakimbizi ulishangiriwa na baadhi ya wakaazi na hata askari wa zima moto kufungiwa njia,pamoja pia na ghadhabu za waandamanaji dhidi ya basi lililokuwa likiwasafirisha wahamiaji,vinaendelea kugonga vichwa vya habari; kuna wanaohoji visa hivyo vinakumbusha yaliyotokea zamani na kuna wanaofika hadi ya kuwanyoshea kidole cha lawama wakaazi wa ile iliyokuwa zamani ikijulikana kama jamhuri ya kidemokrasi ya Ujerumani-au GDR. Gazeti la "Thüringischen Landeszeitung" linaandika": "Hasha,chuki dhidi ya wageni haziko pekee katika eneo la mashariki. Hilo si kweli. Pengine huku linakuzwa. Na kuna wanaojidanganya wakisema eti ni raia walioingiwa na hasira,wanaotaka kuutumia uhuru wa kutoa maoni yao. Hasha,walioshuhudiwa mjini Clausnitz,Bautzen na kwengineko ni wahubiri chuki na wahalifu wanaotia moto majumba na ambao wako tayari kwa lolote lile ovu. Nnapata kichefu chefu nnapowasikia watu wakizungumzia kuhusu eti "malalamiko ya umma" wanaotaka wimbi la wakimbizi lisitishwe.
Kumbukumbu za Hoyerswerda
Na gazeti la "Reutlinger Generali Anzeiger linaandika:" Kwa mara nyengine tena eneo la mashariki mwa Ujerumani linagonga vichwa vya habari kwa ripoti kuhusu chuki dhidi ya wageni. Safari hii vichwa mchungu wametokea Clausnitz,Löbau na Bautzen. Lakini wilaya hizo tatu sio peke yao. Kuna pia vichwa mchcungu katika wilaya za Freital,Heidenau na Meissen wanaohisi matamshi ya chuki dhidi ya wageni hayatoshi. Wamefikwa na nini walioko Saxony,ambako tangu katika miaka ya 90 wamekua wakigonga vichwa vya habari kwasababu ya visa vya chuki dhidi ya wageni? Ndo kusema yaliyotokea hivi karibuni Saxony ni mwanzo wa machafuko dhidi ya wageni kote nchini Ujerumani-kama ilivyokuwa Hoyerswerda?
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman