Kura ya "ndio " ya SPD
15 Desemba 2013Kura hiyo ya maoni ilioshirikisha asilimia 78 ya wanachama wa chama hicho na ambayo ni ya kwanza kutaka ridhaa ya wanachama wa kawaida kwa maamuzi makubwa ya chama imetowa ushindi mkubwa usiostahiki kwa Mwenyekiti wa chama hicho Sigmar Gabriel ikiwa takriban miezi mitatu baada ya chama kushindwa vibaya na chama cha Merkel cha CDU.
Gabriel akiwa mwenye furaha amewaambia waandishi wa habari hakuwahi kushuhudia chama hicho kikiwa katika harakati kubwa za kisiasa katika kipindi cha miaka 36 ambapo amekuwa mwanachama
Fahari kuwa mwana SPD
Amesema "Ni muda mrefu umepita tokea aone fahari kuwa mwanachama wa Social Demokratik."
Amesema anaamini chama chake hicho kimeanzisha hatua isio na kifani kwa demokrasia ya moja kwa moja ambayo inaweza kuzipa taswira mpya serikali za kipindi kijacho.Ameongeza kusema kwamba siku hii sio tu itaingia kwenye historia ya chama cha SPD bali anaamini itaingia pia kwenye historia ya demokrasia ya Ujerumani.
Gabriel amewaambia wafuasi 400 wa SPD waliokuwa wakishangilia na ambao walijitolea kuhesabu kura 369,680 katika ghala lililokuwa na baridi mjini Berlin kwamba chama chao sio tu kikongwe kabisa nchini Ujerumani bali pia ni chama cha kisasa kabisa.
Chama cha CDU kimeyakaribisha matokeo hayo na mshirika wao mdogo katika serikali ya mseto. Katibu Mkuu wa chama cha CDU Hermann Gröhe amesema wanataka kulinda na kuimarisha misingi ya ustawi na mshikamano nchini mwao.Ameongeza kusema "Tuna furaha kwamba sasa kazi yetu kama serikali inaweza kuanza kwa haraka."
Kura ya hapana ingemaanisha nini?
Kura ya "hapana" ingeliweza kuitumbukiza Ujerumani kwenye mgogoro na kukwamisha juhudi za Umoja wa Ulaya za kufanya mageuzi ya umoja wa mabenki ambayo yangeliwezesha Benki Kuu ya Ulaya kusimamia sekta ya mabenki kwa kuyafunga mabenki dhaifu panapokuwa na haja.
Kura ya "hapana" pia ingeliwalazimisha mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel na wasaidizi wake wakuu kujiuzulu. Licha ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani wamefanya juhudi kubwa za kuwashawishi wanachama wenye mashaka wa chama hicho kuwaunga mkono baada ya kufanikiwa kujumuishwa kwa ilani zao za kampeni ya uchaguzi kweye makubaliano ya kuunda serikali ya mseto. Pia ingelikuwa kura hiyo ya SPD imeshindwa juhudi za Merkel za kuunda serikali mpya ingelibidi zianze upya na angelikuwa hana chaguo isipokuwa kukikaribisha chama cha watetezi wa mazingira cha Kijani kujiunga na serikali ya mseto licha ya chama hicho kutokuwa tayari kufanya hivyo Chaguo jengine ilikuwa ni kuitisha uchaguzi mpya ili kukwamuwa mkwamo uliopo.
Tetesi kuhusu baraza la mawaziri
Katika mojawapo ya taarifa zinazoonekana kuwa ni za kushangaza kuhusiana na baraza jipya la mawaziri ni kwamba kuna uwezekano kwa Ujerumani kuwa na waziri wa kwanza wa ulinzi ambaye ni mwanamke. Tetesi zilizozagaa Berlin Jumamosi zinadokeza kwamba Ursula von der Leyen ambaye ana tamaa ya kurithi nafasi ya Merkel atakuwa waziri wa ulinzi au wa mambo ya ndani baada ya kutumikia nyadhifa za waziri wa kazi na waziri wa masuala ya familia.
Naye Ronald Pofalla Katibu Mkuu wa Merkel ametangaza ghafla kujiuzulu. Akiwa kama mratibu wa mashirika ya ujasusi nchini Pofalla amedhihakiwa sana kutokana na namna alivyoshughulikia kashfa ya udukuzi wa mawasiliano ya wananchi kulikofanywa na Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA na kuja kuhitimishwa na taarifa za kufadhaisha hapo mwezi wa Oktoba kwamba shirika hilo pia lilikuwa likiitegesha simu ya mkono ya Kansela Merkel.
Repoti za vyombo vya habari zinasema anaacha wadhifa huo kutokana na sababu za kibinafsi na nafasi yake itachukuliwa na waziri wa mazingira Peter Altmeir ambaye ni msiri wa karibu wa Merkel.
Viongozi wa vyama vitatu vinavyounda serikali mpya ya mseto nchini Ujerumani chama cha Merkel cha CDU na chama ndugu cha CSU na kile cha SPD wanatazamiwa kutangaza baraza la mawaziri Jumapili.Makubaliano ya serikali hiyo ya mseto yatasainiwa Jumatatu na serikali mpya ya Merkel inatazamiwa kuapishwa Jumanne.
Mwandishi: Mohamed Dahman/DW/Reuters/dpa/AFP
Mahriri : Abdul Mtullya