1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujio wa Trump wazidisha mtanziko wa makampuni ya Ulaya,Urusi

22 Januari 2025

Wakati Donald Trump akirejea ikulu ya White House, mamia ya makampuni ya magharibi yaliyoendelea na shughuli zao huko Urusi, yamekuwa katika sintofahamu kuhusu mustakabali wao nchini humo.

USA Washington 2025 | Rais Trump atangaza uwekezaji wa dola bilioni 500 katika miundombinu ya AI.
Rais Trump akitangaza uwekezaji wa dola bilioni 500 katika miundombinu ya AI.Picha: Aaron Schwartz/Pool via CNP/Consolidated News Photos/picture alliance

Kurejea madarakani kwa Donald Trump, ambaye hapo awali aliahidi kumaliza vita nchini Ukraine, kumeibua hali mpya ya wasiwasi miongoni mwa makampuni ya Magharibi ambayo bado yanaendelea kufanya shughuli zake nchini Urusi.

Hali hii inatokea wakati serikali ya Urusi ikiendelea kuimarisha sheria na masharti yanayoongeza gharama za kujiondoa kwenye soko lake, pamoja na kutoa vivutio finyu kwa wanaotaka kuendelea kufanya biashara nchini humo.

Tangu Moscow ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022, makampuni makubwa kama Renault, McDonald's na Heineken yaliondoka Urusi, yakiuza hisa na mali zao kwa hasara kubwa kufuatia sheria kali zilizowekwa.

Baadhi ya makampuni mengine, hususan yale ya vyakula na bidhaa za usafi — kama PepsiCo, Procter & Gamble na Mondelez — bado yanaendelea kufanya shughuli zake nchini Urusi kwa kile wanachokiita "sababu za kibinadamu.”

Benki kadhaa za Ulaya kama Raiffeisen Bank International na UniCredit nazo zinajikuta katika mtanziko huohuo, zikikabiliwa na ugumu wa kurejesha mali zao zilizozuiliwa nchini Urusi.

Tayari, serikali ya Moscow inadai punguzo la angalau asilimia 60 wakati wa miamala ya kuondoka, sambamba na ‘mchango wa hiari' wa asilimia 35 kwenye bajeti yake, ambao Marekani imeuita "kodi ya kuondoka.”

Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Je, Trump atafanya nini?

Wadau mbalimbali wa kibiashara na kisheria, akiwemo Ian Massey, mtaalam wa biashara, wanasema ushindi wa Trump unaongeza sintofahamu kwa mashirika yenye mali au vitegauchumi nchini Urusi.

Kremlin inatarajiwa kuendelea kuongeza gharama za kujiondoa ili kufidia hasara, huku Trump akitabiriwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa makampuni yanayopendelea kuwekeza au kurejea Marekani.

"Inatarajiwa itachukua miezi kadhaa kuumaliza mzozo wa Urusi na Ukraine, hata kama Trump ataingilia kati,” anasema Massey. "Hivyo, makampuni yatakuwa yakitathmini mikakati yao kwa umakini zaidi.”

Soma pia: Gumzo la ushirikiano na Trump latawala Jukwaa la Uchumi Duniani

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kurejea kwa Trump kunaweza kuwapa uwezekano mpya makampuni yanayotaka kuendelea na biashara zao Urusi, ikiwa vikwazo vya kimataifa vitaregezwa. Kwa upande mwingine, huenda yakatokea mazingira yatakayoharakisha makampuni mengine kukamilisha mpango wao wa kujiondoa kabisa.

Sheria za Moscow zinavyozidi kuwa kali

Kwa mujibu wa Alexei Yakovlev, mkurugenzi katika Wizara ya Fedha ya Urusi, mazungumzo ya mikataba ya kuondoka kwa makampuni fulani bado yanaendelea.

Hata hivyo, hakufafanua ikiwa kurejea kwa Trump kunaweza kuzuia hatua za makampuni hayo au kusaidia mengine kurejea nchini Urusi.

Serikali ya Urusi imesisitiza kuwa mpango wowote wa kujiondoa unaohusisha dola milioni 488 au zaidi, lazima upitishwe na Rais Vladimir Putin.

Picha: Newscom World/IMAGO

Aidha, wanunuzi wa ndani wanaotaka kununua mali za makampuni ya nje, wanapaswa kuonyesha mkakati mahsusi, likiwemo jinsi gani kununua au kutonunua biashara husika kunavyoweza kuathiri uchumi wa Urusi.

Mustakabali uliojaa sintofahamu

Mengi yamebadilika tangu mwaka 2022, wakati makampuni mengi yalianzisha mazungumzo ya kujiondoa. Kwa sasa, mchakato huo ni mgumu zaidi kutokana na:

Tathmini ya Thamani: Thamani ya makampuni inahitajika kuthibitishwa na wataalam huru wanaoteuliwa na Wizara ya Uchumi ya Urusi.

Minada ya Uwazi: Serikali inaendesha minada ili kuwapa wanunuzi wote wa ndani fursa sawa, jambo linalowapa makampuni ya Magharibi hofu ya kushindwa kupata bei nzuri.

Kurejea kwa Trump madarakani kumebadili kabisa ramani ya kisiasa na kiuchumi, na huenda kukabadilisha mwelekeo wa makampuni ya Magharibi yanayoyumba kati ya kuondoka au kuendelea kubaki Urusi.

Soma pia:Scholz azuru Kazakhstan kuimarisha biashara, ugavi wa mafuta 

Hata hivyo, mwelekeo huu unatabiriwa kuambatana na mifumo mipya ya kisheria inayodhibiti mtiririko wa rasilimali na fedha.

Trump: Ushindi huu ni mageuzi makubwa ya kisiasa

02:15

This browser does not support the video element.

Bado hakuna uhakika juu ya lini vita vya Ukraine vitakoma, au jinsi Trump atakavyoshughulikia mgogoro huo na vikwazo dhidi ya Urusi.

Wakati uamuzi wa mwisho ukisubiriwa, makampuni ya Magharibi yanajikuta kwenye maamuzi magumu zaidi kuliko wakati wowote ule.

Je, yatadumu Urusi, kuondoka sasa, au kusubiri kuona iwapo sera za Trump zitapunguza gharama zao za uendeshaji na athari za vikwazo?

Ni wazi kuwa mustakabali wa uchumi wa kimataifa unazidi kugubikwa na hali ya kutokuwa na uhakika, huku macho ya wachumi na wafanyabiashara wengi yakielekezwa kwenye Ikulu ya Marekani na Kremlin.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW