1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kurz ashinda uchaguzi wa Austria

30 Septemba 2019

Kansela wa zamani wa Austria ambaye pia ni kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Peoples, Sebastian Kurz ameshinda uchaguzi wa bunge kwa asilimia 37.1.

Wahl Österreich Sebastian Kurz
Picha: picture-alliance/dpa/G. Hochmuth

Matokeo ya awali yaliyotolewa jana Jumapili yanaonyesha chama cha People's ama ÖVP kimejiimarisha kileleni kwa ushindi wa asilimia 5.7 zaidi, ikilinganishwa na mwaka 2017 hii ikiwa ni kulingana na matokeo yaliyochapishwa na shirika la habari la umma la nchini humo, likizingatia kura zote zilizohesabiwa, lakini pia matarajio ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta ambazo zitahesabiwa siku ya Alhamisi.

Mnamo mwezi Mei, Kurz aliuvunja muungano na washirika wake wa mrengo wa kulia na kuitisha uchaguzi wa mapema, kufuatia kashfa kubwa ya rushwa iliyofichuliwa kwenye mkanda wa video dhidi ya kiongozi wa FPÖ Heinz-Christian Strache.

FPÖ kilichokuwa mshirika mdogo wa serikali ya muungano na ÖVP, imeambulia asilimia 16.1 tu ya kura, wakati watetezi wa mazingira, chama cha Kijani wakijiongezea ushindi wa pointi 10.2 na kupanda hadi asilimia 14.

Wafuasi anaomuunga mkono Sebastina Kurz aliyeshinda kwa ushindi mkubwa wa uchaguzi wa bungePicha: Reuters/L. Foeger

Na baada ya matokeo hayo Kurz akasema "Ninapenda kuwashukuru wapiga kura wote, serikali yetu ilichaguliwa tangu mwezi Mei na miezi hii minne imekuwa migumu sana, na sasa watu wametupigia tena kura.. nawashukuru sana kwa kutuamini."

Wiki moja kabla ya uchaguzi, chama cha FPÖ kilikabiliwa na madai mengine ya matumizi mabaya ya fedha ambayo pia yanamwelekea Strache, hatua iliyosababisha chama hicho hata kushindwa zaidi kwenye uchaguzi huu.

Mmoja ya waandamizi wa FPÖ Harald Vilimsky ambaye pia ni mbunge wa bunge la Ulaya alisema jana kwamba chama chao hakitaunda serikali ya muungano na chama hicho cha Kihafidhina cha Kurz kutokana na kashfa hizo.

Kurz atalazimika kusaka uungwaji mkono kutoka kwa chama cha kijani ili kuunda serikaliPicha: Reuters/L. Foeger

Muungano wa ÖVP na FPÖ uliosifika sana kote barani Ulaya, ikiwa ni pamoja na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban hivi sasa hauonekani kushiriki kwenye serikali ya muungano, huku viongozi wake wakisema wataendelea kusalia kwenye upinzani.

Ni kwa maana hiyo sasa, Kurz mwenye miaka 33 atakabiliwa na kibarua kigumu cha kusaka washirika wanaoweza kuungana naye ili kuunda serikali, licha ya ushindi huo mkubwa. Na huenda akalazimika kukigeukia chama cha Kijani.

Norbert Hofer aliyechukua uongozi wa chama cha FPÖ kutoka kwa Strache amesema hatua za kukijenga upya chama hicho zitatangazwa katika siku zijazo, lakini hakuzungumzia kuhusu iwapo itamtimua Strache, kama madai hayo ya matumizi mabaya ya fedha yatakuwa ni ya kweli.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW