1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kusambaa kwa habari za uwongo tishio kwa uandishi

Reuben Kyama3 Mei 2019

Waandishi wa habari na wasomi nchini Kenya wametamaushwa na kukithiri kwa taarifa za uwongo zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii.

Symbolbild Twitter - Tweet melden
Picha: picture-alliance/dpa/A. Warnecke

Katika hafla maalum iliyofanyika jijini Nairobi kuadhimisha siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombao vya habari, swala la jinsi ya kukabiliana na habari za uongo limepewa uzito wa kipekee. David Omwoyo afisa mkuu mtendaji wa baraza la vyombo vya habari nchini Kenya, amekemea matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kama vile facebook na twitter akisema mitandao hiyo inatumiwa kueneza taarifa za kupotosha.

"Mitandao ya kijamii inachukua nafasi ya kwanza katika utoaji na uenezaji wa taarifa za uongo. Unapojumlisha mitandao yote hii ya kijamii utapata kwamba inachangia zaidi ya asilimia 45 ya habari potofu zinazoenezwa," alisema David Omwoyo.

Habari za uwongo huchochea ghasia na chuki

Picha: Imago/ZumaPress

Wasemaji katika mkutano huo wanahoji kuwa licha ya kuwa teknolojia za kisasa zimebadili jinsi tunavyopokea na kubadilishana taarifa, wakati mwingine inatumika kupotosha maoni ya umma au hata kuchochea ghasia na chuki.

Carolin Herzig, mwakilishi wa Shirika la Ujerumani la Maendeleo na Ushirikiano wa kimataifa, GIZ. amesema wameshuhudia kiwango kikubwa cha kuenea kwa habari za uongo na taarifa potovu, mtindo ambao umetatiza juhudi zao za kuleta amani nchini Kenya. Amesema Ijapokuwa hii ni siku ya kuadhimisha uhuru wa habari na demokrasia, kama shirika wanafanya kila jitihada kuendeleza ujumbe wa amani.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, takribani wanahabari 100 waliuawa mwaka uliopita huku mamia wakitiwa mbaroni kutokana na utendaji kazi wao.

Kwenye ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, "waandishi wa habari wanapolengwa, wanajamii ndio wanaogharamika.”