Ujerumani hatarini kukosa wafanyazi wa kigeni wenye ujuzi
6 Julai 2023Serikali ya Ujerumani kwa sasa inapambana na changamoto mbili kubwa zinazoikabili nchi hiyo, na zimeonekana kuwa na uhusiano: ukuaji wa itikadi za mrengo mkali wa kulia na upunguaji wa muda mrefu wa idadi ya watu.
La kwanza ni la haraka zaidi: Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD), chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachopinga uhamiaji, kwa sasa ndicho chenye nguvu kubwa zaidi ya kisiasa katika majimbo kadhaa ya mashariki mwa Ujerumani na sera yake ya kutafuta umaarufu inawafikia wapiga kura wapya.
La pili ni la muda mrefu na la vitendo zaidi, na kulingana na wanauchumi linaweza kutishia ustawi wa nchi: Pengo la idadi ya watu linalokuja katika nguvu kazi ya nchi, ambayo viongozi wa biashara wanasema itahitaji uhamiaji zaidi.
Soma pia: Scholz asema umaarufu wa AfD ni "moto wa mabua"
Hivi karibuni serikali ya Ujerumani ilianzisha sheria iliyokusudiwa kupunguza vikwazo vya ukiritimba vya kuomba kazi nchini Ujerumani, lakini hali ya kisiasa ni ngumu kudhibiti.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner alitoa muhtasari wa suala hilo mapema wiki hii: "Hatari kubwa ya eneo la biashara kwa Ujerumani mashariki ni AfD," alisema katika hafla katika eneo hilo. "Chama ambacho kinataka kujitenga na nchi na kutumikia maneno ya chuki dhidi ya wageni ni mchanga katika gia za uchumi."
Habari kuhusu mrengo wa kulia hupamba vichwa India
Ukweli kwamba ubaguzi wa rangi ni tatizo nchini Ujerumani ni vigumu kuupinga: Ripoti iliyoagizwa na serikali kuhusu chuki dhidi ya Uislamu, iliyochapishwa mwezi uliopita, ilihitimisha kuwa ubaguzi dhidi ya Waislamu "umeenea katika maeneo mengi ya jamii na ukweli wa kila siku."
Ni kwa kiasi gani wasiwasi kama huo huwakatisha tamaa watu kuhamia Ujerumani ni swali lililo wazi.
Ulrich Kober, mkurugenzi wa programu ya Demokrasia na Uwiano wa Kijamii katika Taasisi ya Bertelsmann Foundation, anaamini kuna ukweli fulani kwa onyo la Lindner, lakini alikuwa na tahadhari: "Tunajua kutokana na utafiti kwamba maamuzi ya kuhama ni magumu sana," aliiambia DW.
Soma pia:Misimamo mikali ya mrengo wa kulia yaongezeka Ujerumani
"Kamwe hakuna sababu moja tu: Watu wana vipaumbele tofauti wakati wanachagua mahali pa kuhamia."
Kober alibainisha kuwa ripoti kuhusu chuki dhidi ya Uislamu na mafanikio na kashfa za AfD viliangaziwa na vyombo vya habari nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na Times of India.
"Makundi ya mrengo mkali wa kulia yakiongezeka nchini Ujerumani, au wakati wanasiasa wa mrengo wa kulia wanaposhinda uchaguzi, hilo ni suala la habari katika nchi za kigeni," Kober aliiambia DW. "Watu wanafahamu kinachoendelea Ujerumani."
Hayo yanasisitizwa na Shivam Mehrotra, meneja Mhindi wa TEHAMA ambaye ametumia miaka mitano iliyopita akifanya kazi katika kampuni ya Brandenburg (mojawapo ya majimbo ambayo AfD inaongoza kwa kura za maoni kwa sasa).
Mehrotra, ambaye anawashauri wahamiaji wengine jinsi ya kutumia urasimu wa Ujerumani, alisema Wahindi ambao wanafikiria kuhamia nje ya nchi wanazingatia simulizi kama hizo.
"Sidhani kama itakuwa sababu ya kuamua kuja au kutokuja Ujerumani, lakini mwelekeo ambao nchi inachukuwa utazingatiwa," aliiambia DW.
Soma pia: Maoni: Manifesto ya AfD ni hatari kwa Ujerumani
Mehrotra alisema hakuwa amekumbana na ubaguzi wa rangi wakati wake hapa ("Labda nimekuwa na bahati") lakini kuongezeka kwa siasa kali za mrengo wa kulia kunamsumbua. "Inaniathiri," kijana huyo mwenye umri wa miaka 33 alisema. "Ni mgawanyiko popote duniani lakini hasa Ujerumani, ambayo naiita nchi yangu sasa. Ninapenda kuamini kwamba Ujerumani inathamini maadili ya usawa na utofauti."
Fursa na ubora wa maisha
Taasisi kadhaa, kuanzia zile zinazofadhiliwa na wafanyabiashara kama vile Bertelsmann Foundation hadi mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), hufanya utafiti wa mara kwa mara juu ya kile kinachofanya nchi kuvutia, na kwa nani.
Wamegundua kwamba mambo muhimu zaidi ni uwezekano wa kipato, matarajio ya kitaaluma, na ubora wa maisha. Katika mambo hayo yote, Kober anasema, Ujerumani iko katika nafasi nzuri. Lakini bila shaka iko katika ushindani na nchi nyingine tajiri zinazohitaji nguvu kazi mpya - na Marekani, Kanada, Australia na Uingereza zote zina faida kubwa kwa sababu sehemu kubwa ya dunia inazungumza Kiingereza.
Utafiti wa OECD uliotolewa mwaka jana uliwauliza wafanyakazi wenye ujuzi kutoka duniani kote kile walichokiona kama vikwazo vikubwa vya kuja Ujerumani: Takriban asilimia 38 walitaja ukosefu wa ujuzi wa lugha ya Kijerumani, wakati karibu asilimia 18 walitaja wasiwasi kuhusu ubaguzi wa kijamii na ubaguzi wa rangi.
"Unachangia, lakini unahitaji kuweka katika muktadha wa mambo mengine makubwa," Kober alisema. "Nadhani hiyo pia inatokana na ukweli kwamba watu wengi wanajua hakuna jamii mahali popote ambayo haina ubaguzi wa rangi."
Soma pia:AfD yajitenga na matamshi ya chuki kwa wahamiaji ya msemaji wake wa zamani
"Nchi nyingine, nchi za uhamiaji za Anglo-Saxon, zimeendeleza utamaduni wa uwazi, na hiyo bado inakosekana katika sekta nyingi za watu nchini Ujerumani," aliongeza. "Na bila shaka, AfD - au tuseme, mawazo ambayo yanaongoza watu kukipigia kura AfD - haiwakilishi hasa utamaduni wa uwazi."
Shivam Mehrotra alisema kwamba, kwake na mke wake, kulikuwa na mambo mawili ambayo yalibadilisha uamuzi huo kwa upande wa Ujerumani: "Moja ilikuwa namna Ujerumani ilivyosimamia janga la Uviko-19 kwa namna ya kiuchumi na kibinadamu. Hiyo ilikuwa ya kushangaza."
Soma pia: OECD: Changamoto ya ajira na elimu kwa watoto wa wahamiaji Ulaya
"Na jambo lingine ambalo lilitusukuma sana ni maadili ya nchi hii: Ninatoka katika nchi ambayo ilikuwa koloni la Uingereza, na ukiangalia utafiti, watu wa kizazi chetu nchini Uingereza bado wanaamini kuwa ukoloni ulikuwa jambo jema.
"Wakiwa shuleni Ujerumani, watoto wanafundishwa kuhusu historia ya Wanazi: Kukubaliana na yaliopita ni jambo la kimaadili. Hilo lilinifanya niipende Ujerumani."
Chanzo: DW