1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kushindwa kwa mazungumzo ya biashara ya Geneva kwazusha utata

Nijimbere, Gregoire30 Julai 2008

Baada ya mazungumzo ya Shirika la bishara duiniani WTO ya mjini Geneva kushindwa, maoni yamegawanyika juu ya hoja kwamba mazungumzo yamevunjika kutokana na utaratibu wa mazungumzo hayo.

Wajumbe kwenye mkutano wa mjini Geneva UsuisiPicha: AP

Siku 9 za mazungumzo magumu hazikuweza kuwaleta pamoja wajumbe kwenye mkutano huo wa mjini Geneva Usuisi ili kufikia maridhiano juu ya maswala nyeti yahusuyo masoko duniani kwa kuviondoa vizingiti vinavyovuruga biashara duniani.

Baadhi ya wajumbe kwenye mazungumzo hayo, wamependekeza mikataba midogo midogo ingaliweza kuyaokoa mazungumzó juu ya mkataba wa Doha, ambao uliandaliwa kwa lengo la kufikia kufunguliwa masoko kwa ajili ya bidhaa za kilimo na viwanda pamoja na huduma nyingine kati ya nchi.

Lakini kuna wengine wanaosema kuwa utaratibu wa kuyajadili maswala yote kwa pamoja uliyotumiwa ulikuwa bora kuweza kuyajibu mahitaji ya kila moja.

Muakilishi wa Marekani kwenye mazungumzo hayo ya mjini Geneva Susan Schwab ambae nchi yake iko katika kundi la kwanza linalopendelea kulijadili kila swala kwa zamu yake, amesema yeye hajawahi kuona mazungumzo magumu kiasi hicho katika historia ya mazungumzo juu ya biashara.

Susan Schwab ameelezea kwamba kuna baadhi ya maswala katika mkataba mzima wa Doha ambayo yalionekana tayari kufikia makubaliano ingawaje wajumbe wa nchi 153 wanachama wa Shirika la biashara duniani WTO walishindwa kufikia mwafaka juu ya mkataba mzima ambao ungeondoa vikwazo vya kibiashara juu ya bidhaa kama chakula, gari, nguo na simu. Kwa nini maswala yote hayo yaliwekwa pamoja? Aliuliza Susan Schwab kutoka Marekani.

Kuna namna ya kuweza kusonga mbele kwa kuzingatia sehemu za mkataba huo kwani tukisema hakuna kitakachofanyika bila hichi kingine kufanyika, basi itachukuwa muda mrefu, alimalizia kusema muakilishi huyo wa Marekani kwenye mazungumzo hayo ya mjini Geneva.

Waziri wa biashara wa India Kamal Nath kwa upande wake, amesema mkataba wa Doha bora uzingatiwe kwa pamoja ili nchi masikini ziweze kupata mkataba mzuri wakati mazungumzo yatakapofanyika tena. Shirika la biashara duniani sio tafrija ambapo unachukua kile unachokitaka na unakwenda zako, amemalizia kusema waziri Kamal Nath kutoka India.

Makamu wa waziri mkuu wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema, kuchukuwa sehemu za mkataba kutakuwa na hatari ya kuziacha nyuma baadhi ya nchi na mkondo mzima wa kibiashara duniani. Hatuwezi kuyatenganisha maswala ameongeza kusema Uhuru Kenyatta katika mkutano na waandishi wa habari.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la biashara duniani WTO, Pascal Lamy, amesema kuendeleza mazungumzo juu ya mkataba wa Doha kutategemea kujenga utaratibu ambapo maswala kama vile kiwango cha uagizaji bidhaa kuenda nje, kukata ruzuku za kilimo na ushuru yatakuwa ndio maswala ya kimsingi ambapo maswala mengine yatakuja kujiongezea. Na pengine ndio sababu muakilishi wa Marekani kwenye mazungumzo hayo ya mjini Geneva Susan Schwab akasema kwamba utaratibu wa mazungumzo hayo ndiwo umeyakwamisha.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW