Kushindwa mazungumzo ya kuunda serikali jijini Berlin
6 Oktoba 2011Kinyume na Stuttgart ambako washindi wa uchaguzi,Die Grüne walijadiliana na SPD kama mshirika sawia kuhusu mradi unaozusha mabishano wa kujengwa kituo cha kimambo leo cha usafiri wa reli-maarufu kwa jina Stuttgart 21-Wowereit tangu mwanzo alionyesha kutafuta ugomvi pamoja na walinzi wa mazingira-Die Grüne.Hakujali ridhaa ambazo,pengine wamefikia kwa kuzingatia masilahi yao ya kisiasa. Kwasababu Wowereit anatambua vilivyo kwamba nusu ya wafuasi wa chama chake cha SPD wanapinga mradi wa kupanuliwa njia kuu katika jiji la Berlin.Anaweza pengine kusawisha hali hiyo katika mazungumzo pamoja na CDU na kujihakikishia wingi mkubwa wa viti katika bunge la jiji hilo...
Gazeti la "Flensburger Tageblatt linahisi kupanuliwa njia kuu sio sababu halisi ya kuvunjika mazungumzo kati ya SPD na walinzi wa mazingira-Die Grüne.Gazeti linaendelea kuandika:
Kilomita tatu za njia kuu sio sababu ya kuvunjika mazungumzo.Yamevunjika kutokana na upinzani wa walinzi wa mazingira dhidi ya miradi mengine ya usafiri mfano kupanuliwa kiwanja cha ndege.Katika wakati ambapo chama cha walinzi wa mazingira kinaonyesha kupigania masilahi ya makundi husika,wana social Democratic wao wanatanguliza mbele uwiano uliopo kati ya njia za usafiri na nguvu za kiuchumi.Na hapo ndipo inakokutikana sababu ya kushindikana mazungumzo kati ya SPD na walinzi wa mazingira katika jimbo linalopakana na mto Spree.Ingawa mwenyekiti wa walinzi wa mazingira Claudia Roth anasema kushindwa mazungumzo ya Berlin hakutaathiri mipango yao baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2013.Kwa kuzingatia mivutano isiyokwisha kati ya SPD na Die Grüne katika serikali ya jimbo mjini stuttgart,mtu anaweza kusema yaliyotokea Berlin yanatoa sura ya mvutano kati ya wana SPD wanaotoa kipa umbele kwa nafasi za kazi na Die Grüne wanaopigania usafi wa mazingira.
Na kuhusu mgogoro wa fedha,gazezi la "Braunschweiger Zeitung" linaandika:
Kana kwamba mgogoro wa madeni hautoshi kubainisha umuhimu wa kupunguza matumizi,wengi katika miji mikuu mingi tu wangali bado wanaamini madeni yanaweza kulipwa kwa kutolewa mikopo zaidi .Bila ya ridhaa katika serikali kuu ya shirikisho na bunge la shirikisho,na zaidi kuliko yote bila ya maridhiano barani ulaya,mgogoro huu hautaweza kutatuliwa.
Mwandishi:Hamidou Oumilkhheir/Inlandspresse
Mhariri: Abdul-Rahman