Kushner azuru Israel na Palestina
24 Agosti 2017Ziara ya Kushner inafanyika wakati wachambuzi wakisema Netanyahu na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, wakiwa hawajakuwa tayari kukubaliana. Hakuna taarifa zozote zilizofichuka kuhusu jinsi timu ya rais Trump, itakavyouondoa mkwamo huo na matumaini ni finyu.
Kushner alimwambia Netanyahu kwamba Trump amejitolea kwa dhati kuafikia mkataba utakaoleta maendeleo na amani kwa watu wote wa eneo hilo.
"Tunashukuru kwa juhudi za waziri mkuu Netanyahu na timu yake kujihusisha kikamilifu kwa kutafakari na kwa heshima kulingana na jinsi rais Trump alivyomuagiza. Uhusiano baina ya Israel na Marekani umeimarika zaidi kuliko hapo awali na tunamshukuru sana Netanyahu kwa uongozi na ushirikiano wake."
Netanyahu kwa upande wake alimshukuru Kushner na ujumbe wake akisema wana mengi ya kujadili kuhusu jinsi ya kuendeleza amani, uthabiti na usalama wa kanda hiyo, pamoja na maendeleo.
"Nadhani mambo haya yamo katika uwezo wetu. Nafurahi kukuona na kwa juhudi unazoziongoza kwa niaba ya rais Trump ukiwa pamoja na Jason. Nafikiri hii ni ishara ya ushirikiano muhimu kati yetu na malengo makubwa muhimu yanayotuongoza," alisema Netanyahu.
Kushner kuzuru Ramallah
Kushner alitarajiwa kuelekea mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan kukutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, leo jioni.
Trump alitwaa madaraka akiwa na matumaini ya kupata kile alichokiita mkataba muafaka kati ya Waisraeli na Wapalestina. Lakini hajatoa muelekeo kuhusu vipi anavyotaka kulifikia lengo hilo na hakujawa na ufanisi wowote hadi sasa. Maafisa wa Palestina wameanza kutoa kauli za kukata tamaa na kutokuwa na uvumilivu kwa kukosekana ufanisi.
Mustafa Barghouti, mwanachama wa kamati ya utendaji ya chama cha Ukombozi wa Wapalestina, PLO, alisema, "Haturidhishwi kabisa kwamba utawala wa Marekani haujaishinikiza Israel ikomeshe ujenzi wa makazi ambao unaondoa uwezekano wowote wa kupatikana amani, ingawa ujenzi uliongezeka kwa asilimia 70 tangu rais Trump alipochaguliwa."
Barghouti aidha amesema hawakubali kwamba utawala wa sasa wa Marekani ndio wa kwanza kutambua haki ya Wapalestina kuwa na taifa lao na mpaka sasa umejiepusha na hata kutaja suluhisho la mataifa mawili.
Washauri wa Rais Trump wamefanya mikutano na viongozi wa Israel na Palestina, kwa lengo la kuyasikiliza maoni yao kabla kuamua muelekeo wa kuchukua. Rais Trump mwenyewe aliitembelea Israel na maeneo ya Wapalestina mwezi Mei mwaka huu.
Awali afisa wa Marekani amesema Trump bado ana matumaini ufanisi unaweza kupatikana katika kuafikia makubaliano. Ziara ya Israel na maeneo ya Wapalestina ni sehemu ya ziara ya Kushner, mpambe wa rais Trump, Jason Greenblatt na makamu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa la Marekani, Dina Powell. Wameshafanya mazungumzo na maafisa nchini Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Jordan.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe/dpae
Mhariri: Mohammed Khelef