Kutambuliwa kwa nchi ya Wapalestina kutakuwa na maana gani?
22 Septemba 2025
Canada, Uingereza na Australia, tayari zimelitambua taifa huru la Palestina huku Ufaransa, Ubelgiji Luxemburg na Malta zikitarajiwa kuungana leo hii na wanachama zaidi ya 145 wa Umoja wa Mataifa ambao tayari wanalitambua taifa la Palestina.
Uamuzi wa nchi hizo umetokana na matukio yanayojiri kwenye Ukanda wa Gaza ambapo kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas, wapalestina zaidi ya 65,000 wameshauliwa na wanajeshi wa Israel. Hata hivyo watafiti huru wa kimataifa wanakadiria idadi hiyo kuwa ya juu zaidi.
Pamoja na taarifa hizo, tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imebainisha kwamba Israel inafanya mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza.
Israel na mshirika wake mkuu, Marekani, zimekataa ripoti hiyo na nyinginezo ambazo zimefikia hitimisho sawa na hilo na zimelaani mipango yoyote ya kuitambua Palestina kama taifa, zikidai kuwa kufanya hivyo itakuwa sawa na "kuwazawadia magaidi", zikirejelea shambulio la Oktoba 7, 2023, dhidi ya Israel lililoongozwa na Hamas, ambapo karibu watu 1,200 waliuawa na hilo ndilo jambo mahsusi la kuanzishwa operesheni ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Lakini wengi wanajiuliza, Je kutambuliwa kwa nchi ya Wapalestina kutautatua mgogoro wa Mashariki ya Kati?
Hugh Lovatt, mwanazuoni mwandamizi kwenye kitengo cha Umoja wa Ulaya kinachoshuhgulikia masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini anaeleza:
" Kama watu wanavyosema hatua hiyo itakuwa ni ishara tu. Lakini nafikiri kutoa ishara si jambo baya. Ni hatua ya kusisitiza haki ya Wapalestina ya kujiamulia mambo yao wenyewe katika nchi yao huru. Tumeyajua hayo siku nyingi, lakini sasa ni muhimu zaidi kwa sababu Ufaransa na Uingereza nazo zinalizungumzia suala hilo.”
Hata hivyo inafaa kutilia maanani kwamba hata washirika wa ndani wa Wapalestina wanatambua kwamba uamuzi wa kulitambua eneo la Wapalestina hautatosheleza endapo hautaandamana na hatua madhubuti ikiwa pamoja na kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.
Mkurugenzi wa kutetea haki za Wapalestina kwenye chuo cha kidiplomsia kilichopo kwenye mji wa Ramallah, Ines Abdel Razek amesema wakati nchi za magharibi zinacheza tamthilia za ishara, Wapalestina wanaendelea kuteseka, hawana haki wala eneo huru.
Wanadilomasia watiwa wasiwasi na kauli ya Netanyahu
Mbali na hayo inafahamika kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anafahamika kuwa mtu anayepinga maamuzi yanayopitishwa na jumuiya ya kimataifa. Wanadiplomasia wameingiwa wasi wasi juu ya kauli iliyotolewa na Netanyahu juu ya Ukanda wa Gaza akisema hapatakuwapo nchi ya Wapalestina.
Katika upande mwingine kutambuliwa kwa nchi ya Wapalestina kutaimarisha juhudi zenye lengo la kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.
Kwa upande wake, mwandishi wa habari Gideon Levy kwenye nakala yake ya mwezi Agosti katika gazeti la Israel la Haaretz alisema kutambuliwa kwa taifa la Palestina ni hatua mbadala za kufunika makosa na kubabaisha hatua za adhabu zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya nchi inayoendeleza mauaji ya kimbari.
Amesema huko ni kutambuliwa kwa mdomo tu kusiko na maana yoyote na kwamba ni jambo la muhimu kujua wazi kwamba kutambuliwa kwa taifa la Palestina peke yake hakutazuia vita vya Israel huko Gaza na wala hakutasimamisha mauaji ya kimbari. Gideon Levy amesisitiza jumuiya ya kimataifa ichukue hatua za kivitendo.