Jeshi la Israel lazidi kusonga mbele ndani ya Gaza City
23 Septemba 2025
Jeshi la Israel hii leo limeendelea kusogea zaidi katika maeneo yenye wakaazi wengi katika Jiji la Gaza, siku moja baada ya viongozi wa dunia waliokusanyika katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakitangaza kulitambua taifa la Palestina. Utambuzi wa Palestina kama nchi kunaonekana hata hivyo kutoleta matumaini kwa Wapalestina wanaokabiliwa na mashambulizi.
Mabadiliko hayo ya kihistoria ya kidiplomasia baada ya karibu miaka miwili ya vita yanapingwa vikali na Israel na mshirika wake wa karibu Marekani.
Israel inasema hatua hiyo itadhoofisha matarajio ya kumalizika kwa amani kwa vita katika eneo la Palestina, ambalo sehemu yake kubwa imeharibiwa na kuchochea mgogoro mkubwa wa kibinadamu ikiwa ni pamoja na njaa iliyoenea.
Mamlaka za afya katika eneo hilo zimesema kwamba mashambulizi ya Israel ya leo Jumanne yamewaua watu 22 katika Ukanda wa Gaza.