Kutetea ubingwa ngumu Uingereza, Conte
2 Oktoba 2017Kocha mkuu wa Chelsea Antonio Conte anaamini kwamba kutetea ubingwa wa ligi ni jambo rahisi nchini Italia kuliko Uingereza katika Premier League kutokana na sera za uhamisho wa wachezaji katika vilabu vikubwa. Conte ameshinda ubingwa mara tatu katika Serie A nchini Italia akiwa na FC Juventus baada ya mahasimu wao AC Milan kuwauza washambuliaji Zlatan Ibrahimovic, Alexandre Pato na mlinzi Thiago Silva.
Napoli iliwaondoa winga Ezequiel Lavezzi katika kipindi cha nyuma. Baada ya Chelsea kushinda ubingwa wa ligi msimu uliopita mahasimu wao wakubwa Tottenham Hotspurs , Manchester City, Manchester United , Liverpool na Arsenal , wamewekeza pakubwa katika vikosi vyao. Conte alisema ni vigumu kutetea ubingwa katika ligi hiyo. Ni vigumu kushinda mataji mawili mfululizo katika ligi ya Uingereza.
Chelsea ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Manchester City siku ya Jumamosi , ambapo Man City ilipora uongozi wa ligi hiyo kutoka kwa Manchester United licha ya kushinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Crystal Palece siku ya Jumamosi.
Kocha wa Liverpool Juergen Klopp nae ametathmini kushindwa kwa hivi karibuni kwa kikosi chake kushinda katika mchezo wa Premier League baada ya sare ya kufadhaisha ya bao 1-1 dhidi ya Newcastle United kwa kusena , "soka halina usawa."
Kocha huyo raia wa Ujerumani alipata taabu kuukubali ukweli kwamba kikosi chake kiliondoka na pointi moja tu baada ya kumiliki mpira kwa muda mrefu dhidi ya kikosi cha Rafa Benitez cha Newcastle katika uwanja wa St. James Park jana Jumapili.
Wakati huo huo kocha wa Manchester United Jose Mourinho amesema wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza kuwa majeruhi ni fursa kwa wachezaji wengine kujionesha katika kikosi hicho na kupata uzoefu.
Paul Pogba ni mmoja wa wachezaji hao ambao watakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu, na klabu hiyo itakuwa na michezo mitano bila ya kiungo huyo mchezeshaji, ikiwa ni pamoja na mchezo walioshinda kwa mabao 4-0 dhidi ya timu iliyoko mkiani ya Crystal Palace.
Guardiola
Kocha wa zamani wa Barcelona Pep Guardiola ameeleza kushangazwa kwake leo na ghasia ambazo zimechafua kura ya maoni ya kudai kuwa huru kwa jimbo la Catalonia , ambazo amesema ingesababisha klabu ya Barcelona kuahirisha mchezo wake dhidi ya Las Palmas.
Barcelona iliishinda Las Palmas kwa mabao 3-0 katika uwanja ambao ulikuwa tupu wa Nou Camp jana Jumapili.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman