Kuteuliwa Kramp-Karrenbauer kuwa katibu mkuu wa CDU
20 Februari 2018Tunaanzia Berlin ambako wahariri wanakubaliana , uamuzi wa kansela Merkel wa kumteuwa waziri mkuu wa jimbo la Saarland awe katibu mkuu mpya umelengwa kuendelea kukifanya chama hicho cha kihafidhina kifuate siasa za wastani. Gazeti la Südkurier linaandika: "Kansela amefichua karata zake. Katibu mkuu mpya wa chama chake cha Christian Democratic Union-CDU atakuwa waziri mkuu wa jimbo la Saarland, bibi Annegret Kramp-Karrenbauer. Uamuzi huo unabainisha nani Merkel anamuamini awe mrithi wake. Pindi mteule huyo akifanikiwa katika jukumu lake jipya, basi hakuna kitakachomzuwia mwanasiasa huyo wa jimbo la Saarland, kumrithi siku moja Angela Merkel kama mwenyekiti wa chama na pia atakapostaafu. Uamuzi huo ni muongozo pia chama cha CDU kitafuata mkondo gani. Kramp-Karrenbauer anatetea mkondo wa kiliberali chini ya maadili ya kikristo na kidemokrasia. Anapigania chama kitakacholeta mageuzi Ujerumani badala ya kungang'ania ya zamani. Mageuzi ya kihafidhina, kama anavyopigania mpinzani wake Jens Spahn au kuelemea zaidi mrengo wa kulia, anasema, si pamoja nae. Mnamo miezi ya hivi karibuni Jens Spahn amekuwa mara kwa mara akipaza sauti dhidi ya kansela Merkel na jibu lake sasa amelipata."
Luteka kubwaa za NATO
Jumuia ya kujihami ya NATO inajiandaa kwa luteka za kijeshi za kutunisha misuli dhidi ya Urusi. Wahariri hawaziangalii kwa jicho zuri luteka hizo. Gazeti la "Nordkurier" linaandika: "Jumuia ya kujihami ya NATO inapanga mwaka huu kutunisha misuli yake karibu na mpaka wa Urusi. Jeshi la Ujerumani Bundeswehr pekee linapanga kutuma wanajeshi 12.000 katika zoezi hilo la vita, idadi ambayo ni kubwa mara tatu ikilinganishwa na mwaka jana. Na kauli mbiu ya luteka hizo zitakazoigharimu Ujerumani Euro milioni 90, nayo pia inatisha; Ncha ya upanga, Radi ya moto au mbwa mwitu aliyevaa chuma, ni miongoni mwa kauli mbiu. Yadhihirika kana kwamba kutuliza mambo sio jambo walitakalo viongozi wa NATO mjini Brussels kama luteka hizo ambazo hazina maana yoyote, zinavyoonyesha. Eti ndo kusema ni mbinu za kujihami au za kuchochea mashambulio? Rais Vladimir Putin anachekelea. Haijawahi kuwa rahisi kwake kuwaonyesha NATO cha mtema kuni na wakati huo huo kujizidishia umashuhuri nchini mnamo wakati huu ambao uchaguzi unakurubia.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef