Agosti 9 ni Siku ya Wazawa wa Asili duniani
9 Agosti 2023Siku ya Kimataifa ya Watu wa Kiasili Duniani huadhimishwa tarehe 9 Agosti kila mwaka; tarehe hiyo ilichaguliwa kwa kutambua mkutano wa kwanza wa Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wa Kiasili, uliofanyika Geneva mwaka 1982.
Kwa jamii ya watu hao na makundi ya haki za binadamu duniani kote, siku hii ni fursa ya kusherehekea mila na maarifa yao, lakini pia kukemea unyonyaji haramu wa maliasili pamoja na kutengwa kisiasa na kiuchumi kwa watu wa kiasili.
Mashirika ya Ujerumani pia yanaadhimisha siku ya watu wa asili
Eliane Fernandes wa Shirika lisilo la Kiserikali la Ujerumani la Society for Threatened Peoples (STP) aliliambia shirika la utangazaji la DW kuwa kumekuwa na kesi zenye kuihusu jamii hiyo ya watu katika kila bara kuanzia Amerika ya Kaskazini, Amerika Kusini, Amerika ya Kati, Australia, Asia, hata kaskazini mwa Ulaya au Urusi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuna takriban watu milioni 476 wa jamii za Wenyeji wanaoishi katika nchi 90 duniani kote. Kwa idadi hiyo wanafanya takribani asilimia 5 ya idadi jumla ya watu duniani. Kwa mujibu wa asasi hiyo yenye kulinda ustawi wa jamii hiyo ya watu STP ni kwamba watu wa asili au wazawa ni warithi na watekelezaji wa tamaduni kwa vitendo na kwa njia ya kipekee za mahusiano ya watu na mazingira.
Kuzilinda haki za watu wa kiasili au wazawa.
Takriban nusu ya watu wote wa kiasili wanaofanya kazi duniani hawana elimu rasmi. Watu wa kiasili wana uwezekano wa karibu mara tatu zaidi wa kuishi katika umaskini uliokithiri kuliko wenzao wasio wazawa. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Watu wa kiasili huzungumza idadi kubwa ya lugha takriban 7,000 duniani na huwakilisha tamaduni 5,000 tofauti.
Mwaka 2007, Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio la Haki za Watu wa Kiasili (UNDRIP). Tamko linafafanua haki za watu wa kiasili, linalaani ubaguzi na kubainisha haki za ushiriki. Tamko hilo linanuiwa kusaidia nchi kufanya kazi pamoja na watu wao wa kiasili. Lengo kuu ni kuhifadhi urithi wao wa kitamaduni - utamaduni wao, utambulisho, lugha, kazi, afya na elimu.
Mwanaharakati wa asili kutoka Brazil nchini Ujerumani.
Mfumo wa Kitaalam wa Haki za Watu wa Kiasili (EMIP), chombo cha ushauri cha Umoja wa Mataifa, kimekuwa kikiwaleta pamoja wawakilishi wa watu wa kiasili katika mikutano ya mara kwa mara tangu 2007. EMIP imetoa ushauri kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, ambalo mkutano wake wa hivi karibuni ulifanyika Julai 2023 Geneva Uswisi.
Mmoja wa washiriki alikuwa Beto Marubo, ambaye anawakilisha Muungano wa Watu Wenyeji wa Bonde la Javari la Brazil (UNIVAJA), na sasa amealikwa kushiriki katika hatua ya haki za binadamu huko Hamburg mnamo Agosti 9. Marubo anatetea watu wanaoishi katika jamii za mbali za Wenyeji katika msitu wa Amazon. Hali yao ilikuwa mbaya zaidi chini ya utawala wa Rais wa zamani Jair Bolsonaro.
Soma zaidi: Wahadzabe: Tunapenda na kulinda utamaduni wetu wa jadi
Ukataji miti holela umeharibu makazi ya watu wengi wa kiasili. Lakini hata serikali mpya chini ya Rais Lula da Silva lazima kwanza ijidhihirishe yenyewe katika ukwamuzi wa maisha ya watu wa jamii hiyo. "Hatutaipa serikali mpya sifa ya bure," anasema Marubo. "Tutatoa madai yetu na tutakuwa madhubuti." Alisema mwanaharakati huyo.