1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutwaliwa kwa mji wa Sirte ni pigo kwa serikali ya Libya

9 Januari 2020

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kutwaliwa kwa mji wa kimkakati wa Sirte nchini Libya na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar ni pigo kubwa kwa serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa iliyoko mjini Tripoli.

Italien 2018 | Chalifa Haftar, Warlord Libyen
Picha: Getty Images/AFP/F. Monteforte

Kusonga mbele kwa kikosi cha Libyan National Army (LNA) cha mbabe wa kivita, Jenerali Khalifa Haftar, kumekuja wakati Uturuki ikipeleka wanajeshi wake 35 kusaidia kutoa mafunzo ya kijeshi ili kuvipiga jeki vikosi vya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa. 

Juhudi za kidiplomasia za kujaribu kuuzuwia mzozo huo wa Libya kusambaa zaidi zimesababisha Uturuki na Urusi hivi karibuni kutoa wito wa kusimamishwa mapigano licha ya mataifa hayo mawili kuunga mkono pande tofauti katika mzozo huo. Lakini pande hasimu nchini humo bado hazijaitikia mwito huo.

Mji wa Sirte ulikuwa unadhibitiwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali inayoungwa mkono kimataifa, baada ya kuliondoa kundi la wanamgambo wa Dola la Kiislamu (IS) katika mji huo mwaka 2016.

Lakini baada ya vikosi vya wanamgambo vya Kisalafi kuuondoka, mji huo uliingia mikononi mwa vikosi vya Haftar bila ya mapigano. Vikosi vyake vimekuwa vikijaribu kuutwaa mji mkuu, Tripoli, kutoka vikosi vya serikali tangu mwezi Aprili.

Mji wa Sirte, alikozaliwa aliyekuwa rais wa muda mrefu nchini humo Muammar Gaddafi, umepitia vipindi vigumu sana baada ya kiongozi huyo kuondolewa madarakani na kisha kuuwawa mwaka 2011 na vikosi vya waasi vikisaidiwa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Mji wa Sirte unadhibitiwa wakati Uturuki ikituma wanajeshi wake Libya

Mpiganaji wa kikosi cha Libya Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Brabo

Wakaazi wengi wa mji huo walivikaribisha vikosi vya Haftar, maana hawakukiunga mkono kikosi cha serikali, ambacho kwa kiasi kikubwa kiliwajumuisha waasi wasio watiifu kwa Gaddaffi kutoka Misrata, mji uliopo kati ya Sirte na Tripoli.

Tangu Haftar alipoanzisha kampeni yake ya kuitwaa Tripoli, hatimaye vikosi vyake pia vimeweza kuzuia mashambulizi yote katika mji wa Sirte wenye utajiri mafuta, kaskazini mashariki mwa Libya. Jenerali huyo alihofia kuwa vikosi vya serikali vingelitumia kambi ya kijeshi ya Sirte kuanzisha mashambulizi kwa eneo analolishikilia upande wa mashariki, kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya Libya, Jalel Harchaoui, ambaye anasema kutwaliwa kwa mji wa Sirte kunaweka shinikizo kwa serikali inayojaribu kulinda mji mkuu Tripoli na vitongoji vyake.

Kulingana na Emad Badi, mchambuzi katika taasisi moja iliyoko Mashariki ya Kati, Haftar anataka kuviunganisha vikosi vya Misrata na Sirte ili kuudhoofisha ulinzi wa Tripoli. Vikosi vyake huenda vikataka kuanzisha uwanja wa mapambano dhidi ya Misrata kilomita 200 mashariki mwa Tripoli.

Kuchukuliwa kwa mji wa Sirte na vikosi vya Haftar kunakuja wakati Uturuki ikituma vikosi kukiunga mkono kikosi cha serikali dhidi ya Haftar anayeungwa mkono na maadui wa Uturuki - Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri. Kutwaliwa kwa huo kunaufanya uungaji mkono huo wa Uturuki kuwa muhimu zaidi.

Chanzo: Reuters/afp

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW