Kuvamia Reichstag:Shambulio la moyo wa demokrasia Ujerumani
30 Agosti 2020"Vurugu zilizotokea za bendera za Reich na wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia mbele ya jengo la bunge la Ujerumani ni shambulio ambalo haliwezi kuvumilika katika moyo wa demokrasia yetu. Hatutakubali hali hiyo," Steinmeier alisema leo Jumapili (30.08.2020).
Bendera yenye rangi nyeusi, nyeupe na nyekundu, bendera ya kihistoria ya Ujerumani ya enzi za Reich, ama himaya, mara kadhaa hutumiwa na watu wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia wa siku hizi.
"Demokrasia yetu iko hai," Steimeier alisema.
Mtu yeyote ambaye ana hasira juu ya hatua zinazochukuliwa na Ujerumani kudhibiti virusi vya corona au ana shaka na umuhimu wake anaweza kujieleza, hata katika eneo la umma, hata kwa maandamano , alisema.
"Kuelewa kwangu kunafikia kikomo wakati waandamanaji wanakubali kuingizwa katika mkumbo wa maadui wa demokrasia pamoja na wanaohamasisha masuala ya kisiasa."
Steinmeier aliwashukuru maafisa wa polisi," "ambao walichukua hatua kali katika mazingira magumu."
Wavamia bunge
Jumamosi jioni, waandamanaji wanaopinga sera za kudhibiti virusi vya corona nchini Ujerumani walivunja vizuwizi katika jengo la bunge Reichtag, ambalo ni jengo la bunge la Ujerumani katikati ya mji wa Berlin, na kuvamia wakiingia hadi katika ngazi za kuingilia katika jengo hilo.
Maafisa wa polisi waliwasukuma nyuma na kuwapulizia gesi ya pilipili. Kulikuwa na mapambano.
Hapo kabla kulikuwa na maandamano katika jengo la bunge la Reichtag.
Bendera za rangi nyeusi, nyeupe na nyekundu za himaya hiyo ya kifalme inayotumiwa na kile kinachoitwa (wananchi wa himaya hiyo) ambao ni kundi lenye msimamo mkali pia zilikuwapo.
Kiasi ya watu 38,000 walishiriki katika maandamano hayo dhidi ya vizuwizi vya corona mjini Berlin siku ya Jumamosi licha ya juhudi za polisi kuwatawanya kutokana na kitisho cha kuambukizana virusi vya corona.