1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuyumba kwa uchumi kwa viathiri vilabu vya soka Ulaya

Liongo, Aboubakary Jumaa24 Septemba 2008

Vilabu vya soka Barani Ulaya ambavyo havimilikiwi na watu au makampuni yenye uwezo mkubwa kifedha vimeanza kuguswa na machungu ya mzozo wa kiuchumi unaoikumba dunia hivi sasa.

Manchester United wakishangilia ubingwa wa Ulaya Mjini Moscow tarehe 21 May mwaka huu.Picha: picture-alliance/ dpa

Mauzo ya tiketi pamoja na ufadhili vimeshuka msimu huu tofauti na msimu uliyopita.


Kwa mfano msimu huu nchini Uingereza mapato kutokana na udhamini kwa vilabu ambapo makampuni huweka majina yao kwenye jezi za timu hizo, yameshuka ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 16, kutoka paundi millioni 75 mwaka jana hadi paundi millioni 67 mwaka huu.


Makampuni kadhaa yamepunguza bajeti ya matangazo, huku, kupanda kwa bei ya tiketi na kuongezeka kwa gharama ya maisha kukiwafanya washabiki wengi kuamua kubakia majumbani mwao.


Roy Miller kutoka kitengo cha biashara ya michezo katika chuo kikuu cha Liverpool anasema kuwa hali kama hiyo haijawahi kuonekana kwa muda mrefu na ni ishara ya kwamba uchumi uko katika hali mbaya.


Wachambuzi wanaamini hata hivyo kuwa vilabu vikubwa kama vile mabingwa wa Uingereza Manchester United, Real Madrid na kadhalika siku zote zitaendelea kuwavutia wafadhili na washabiki wengi, lakini kwa vilabu vidogo hali ni tofauti.


Gary Leih ambaye ni mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa kampuni linalojishughulisha na matangazo nchini Uingereza la Ogilvy Group anasema kuwa tatizo hilo si kwa vilabu kama Chelsea Arsenal, Manchester United na vilabu vingine vinavyotamba katika ligi kuu, lakini anasema kwa vilabu vilivyoko madaraja ya chini kupata ufadhili ni kazi kubwa.


Anasema kuwa pengine njia pekee ni kutegemea zaidi wazalishaji wa bidhaa za ndani kuwadhamini.


Ligi kuu ya Uingereza ndiyo ligi yenye kuingiza fedha nyingi kabisa ambapo mwaka jana mapato yake yalifikia kiasi cha paundi billioni 1.5.Lakini ni vilabu vinane tu kati ya 20 vya ligi hiyo vinavyojiendesha kwa faida.


Maswali yameibuka juu ya majaaliwa ya udhamini wa kampuni ya kimarekani ya AIG kwa timu ya Manchester United wa dhamani ya paundi millioni 56.5 ambayo ni rekodi nchini Uingereza.Kampuni hiyo ya kimarekani imelazimika kuokolewa na serikali iliyonunua hisa kubwa za asilimia 80 baada ya kuwa katika hali mbaya ya kuelekea kuwa mufilisi.


Timu nyingine ya ligi kuu ya Uingereza ya West Ham Unitd hivi sasa haina udhamini katika jezi zao baada ya kampuni iliyokuwa ikiidhamini ya XL Leasure Group kufilisika.Nayo West Bromwich Albion iliyopanda daraja imeshindwa kupata ufadhili kufuatia kujiondoa kwa aliyokuwa mfadhili wake kampuni ya simu ya Ujerumani ya T-Mobile.


Newcastle United nayo ilikaribia kuwa katika hali hiyo baada ya mfadhili wake benki ya Northen Rock kuokolewa na serikali ya Uingereza kufilisika ambapo huko Italia timu ya Lazio kwa sasa inacheza bila ya kuwa mfadhili .


Hata hivyo kwa mujibu wa wachambuzi na watalaam wa masuala ya ufadhili katika michezo, timu kama Manchester Uinted haitopata shida kupata ufadhili mwengine iwapo serikali ya Marekani itaamua kuondoa ufadhili wake baada ya kuwa imechukua hisa kubwa katika kampuni ya AIG.


Pippa Collet ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayohusika na udhafili kwenye sekta ya michezo anasema kuwa udhamini katika kandanda kwa muda mrefu umekuwa ukipewa thamani kubwa kuliko inavyostahili, na kwamba hivi sasa kunafanyika marekebisho katika soko la udhamini.


Bei ya tiketi nayo katika miaka ya hivi karibuni imepanda sana, hali inayolazimu wakati mwengine kwa baadhi ya timu kucheza katika viwanja vyenye idadi chache ya watazamaji.


Malcolm Clarke ambaye ni mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya washabiki wa kabumbu nchini Uingereza, anatahadharisha kuwa sekta ya soka ni lazima iwe macho kwani kupanda kwa bei ya tiketi, kupanda kwa bei ya mafuta pamoja na gharama za usafiri kuongezeka, kunatishia sekta hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW