1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini Daraja la Kerch ni muhimu kwa Urusi na Ukraine?

10 Oktoba 2022

Mlipuko uliharibu sehemu za daraja linalounganisha Urusi na rasi ya Crimea. Katika ripoti ifuatayo, DW inaangazia kwa nini daraja hilo la Kerch ni muhimu kwa juhudi za vita vya Moscow nchini Ukraine.

Ukraine Krieg Krim-Brücke
Picha: AFP/Getty Images

Mlipuko mbaya ulizua moto Jumamosi ya Oktoba 08,2022 na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye daraja la Kerch linalounganisha Urusi na rasi ya Crimea.

Maafisa wa Urusi walisema moto huo ulisababishwa na mlipuko wa lori na hawakumlaumu yeyote mara moja. Wachambuzi wamedokeza kuwa huenda ikawa ni matokeo ya shambulio la Ukraine. Wizara ya Usafiri ya Urusi ilisema shughuli ndogo za usafirishaji wa barabara zilianza tena kwenye upande mmoja wa njia moja wa daraja.

Maafisa wa Ukraine hawataja kuhusika moja kwa moja na mlipuko huo lakini mara kwa mara wamekuwa wakidokeza nia yao ya kutaka kuharibu daraja hilo na wamechapisha kwenye mitandao ya kijamii kusherehekea mlipuko huo.

Soma zaidi: Urusi: Daraja muhimu la Krimea laharibiwa na mlipuko wa lori

Kiev imeapa kutwaa tena eneo la Crimea, ambalo Urusi ililitwaa kinyume cha sheria mnamo mwaka 2014.

Unalifahamu Daraja la Kerch?

Helikopta ikijaribu kuzima moto katika Daraja la Kerch, Oktoba 8,2022Picha: REUTERS

Moscow ilijenga Daraja la Kerch ili kuunganisha rasi ya Crimea na eneo la Urusi la Krasnodar Krai kaskazini mwa Caucasus.

Wakati huo, daraja hilo liligharimu dola bilioni 3.6. Likiwa na urefu wa kilomita 19, mradi huo kabambe ulioundwa kusaidia kuimarisha miundombinu ya Crimea na kuimarisha uhusiano wake na Urusi, ndio daraja refu zaidi barani Ulaya.

Wakati wa ujenzi wa daraja hilo linalovuka Mlango wa Bahari wa Kerch na kuunganisha Bahari ya Azov na Bahari Nyeusi, Kiev iliishutumu Urusi kwa kuharibu mazingira na kuzuia usafiri wa meli kubwa.

Soma zaidi: Watatu wafa kwenye mlipuko wa daraja la Crimea

Daraja hilo ni muhimu kwa usafirishaji wa vifaa kwa vikosi vya Urusi katika mkoa wa Ukraine unaokaliwa wa Kherson. Mwishoni mwa mwezi Septemba, Moscow iliinyakuwa kinyume cha sheria mikoa ya kusini ya Kherson na Zaporizhzhia, ambayo inalenga kuiunganisha Crimea na mikoa ya Donetsk na Luhansk, ambapo kundi la wanaotaka kujitenga na wanaounga mkono na Urusi wamekuwa wakianzisha uasi dhidi ya serikali ya Kiev tangu mwaka 2014.

Wachambuzi wa maswala ya siasa wanasema mlipuko katika daraja hilo unadhaniwa kwa kiasi kikubwa kusababishwa na vikosi vya Ukraine kwa kuwa kitendo hicho kina manufaa ya kimkakati kwa Kiev, na kwamba wanajeshi wa Urusi waliopo Ukraine wanategemea mno daraja hilo kwa usafirishaji wa vifaa na bidhaa zingine muhimu.

Maafisa wa Ukraine waikashifu Moscow kwa mlipuko huo

Sehemu ya Daraja la Kerch ikiwa imeharibiwa.Picha: Moya Feodosiya/Tass/IMAGO

Uharibifu wa Daraja la Kerch una maana kubwa kwa Kiev, ambayo imeahidi kuikomboa rasi ya Crimea kutoka kwa Urusi, pamoja na maeneo mengine yote ya Ukraine yanayokaliwa kwa sasa na vikosi vya Urusi.

Mkuu wa Baraza la Usalama na Ulinzi wa Ukraine, Oleksiy Danilov, alichapisha video kwenye ukurasa wake wa mtandao waTwitter inayoonyesha Daraja la Kherson likiungua na wakati huo huo kukiwa na video ya mwimbaji Marilyn Monroe akiimba "Heri ya Kuzakiwa Bwana Rais." Mlipuko huo ulitokea siku moja baada ya Rais Putin kusherehekea miaka 70 ya kuzaliwa kwake.

Soma zaidi: Zelensky aapa kuikomboa Crimea kutoka mikononi mwa Urusi

Shirika la posta la Ukraine lilisema kuwa litachapisha muhuri maalum kuadhimisha mlipuko huo, huku mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak akisema kwamba huo ulikuwa "ni mwanzo tu."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, alisema kuwa kauli za maafisa wa Ukraine kufuatia uharibifu wa daraja hilo "zinathibitisha azma ya kigaidi ya Kiev."