Kwanini India inaongeza mahusiano ya kidiplomasia na Taliban
11 Januari 2025Kwa kuongeza juhudi zake za kuwasiliana na watawala wa Taliban wa Afghanistan, Katibu wa Mambo ya Nje wa India, Vikram Misri, alikutana na waziri wa mambo ya nje wa muda wa utawala huo, Amir Khan Muttaqi, huko Dubai siku ya Jumatano.
Kulingana na taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Taliban, mazungumzo yalihusu masuala kama vile changamoto za kiusalama Afghanistan, haja ya India kushiriki katika miradi ya maendeleo na kutoa msaada wa kibinadamu, na matumizi ya bandari ya Chabahar nchini Iran kuleta biashara katika nchi hiyo yenye migogoro.
"Kulingana na sera ya kigeni ya Afghanistan inayolenga usawa na uchumi, Dola ya Kiislamu inalenga kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na India kama mshirika muhimu wa kikanda na kiuchumi,” taarifa hiyo ilisema.
Mkutano huo ulikuwa mazungumzo ya ngazi ya juu zaidi kati ya India na Taliban tangu kundi hilo lilipochukua Kabul mnamo Agosti 2021.
"Kutokana na ombi la upande wa Afghanistan, India itatoa msaada zaidi wa vifaa, hasa kwa sekta ya afya na kwa ajili ya ukarabati wa wakimbizi. Pande mbili pia zilijadili kuimarisha ushirikiano wa michezo (kriketi),” Wizara ya Mambo ya Nje ya India ilisema baada ya mkutano huo.
Je, ni hatua ya kuikabili China?
Shanthie Mariet D'Souza, mtaalam wa masuala ya Afghanistan anayefuatilia matukio ya hivi karibuni, alikubali kuwa mkutano huo ni hatua muhimu kwani India inaonekana kufanya kazi kufikia mahitaji ya kidiplomasia yatakayoiwezesha kushirikiana kikamilifu na Taliban.
Soma pia: Jeshi la Uingereza liliuwa kwa makusudi Afghanistan - Uchunguzi
"Katikati ya sera ya India ni lengo la kurejesha ushawishi wake uliopotea na kuimarisha uhusiano wake na Kabul,” D'Souza, mwanzilishi wa Taasisi ya Mantraya kwa Mafunzo ya Kistratejia, aliambia DW.
"Zaidi ya hayo, India inalenga kurejesha ushawishi wake katika eneo ambalo China imeongeza uwepo wake kwa kiasi kikubwa tangu Agosti 2021,” aliongeza.
Gautam Mukhopadhyay, balozi wa zamani wa India nchini Afghanistan, aliambia DW kwamba India inatafakari tena msimamo wake wa kidiplomasia na kufanya kazi kuimarisha uhusiano wake na uongozi wa sasa wa Taliban.
"India haina shinikizo la kuitambua rasmi Taliban, hasa ikizingatiwa kuwa kuna dalili za migawanyiko ya ndani kati ya viongozi wa Taliban, ambao wanaendelea kuwanyanyasa wanawake vikali na kuwanyima haki yoyote,” alisema.
"Lakini kuna sababu nyingine za msingi za kushirikiana, ikiwa ni pamoja na biashara, uhusiano wa kihistoria, Chahbahar na Mradi wa Usafiri wa Kimataifa wa Kaskazini-Mashariki, pamoja na China,” aliongeza Mukhopadhyay.
Kuweka msingi
Mnamo Novemba, afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje, JP Singh, alifanya mikutano kadhaa na wawakilishi wa Taliban, ikiwemo mkutano muhimu na Waziri wa Ulinzi wa muda, Mullah Mohammad Yaqoob.
Mnamo Juni 2022, India ilituma "timu ya kiufundi" Kabul kuratibu utoaji wa msaada wa kibinadamu na kuangalia jinsi New Delhi inaweza kusaidia watu wa Afghanistan.
Soma pia:UN: Waandishi wa habari zaidi ya 250 wamekamatwa tangu Taliban ilipoingia madarakani
Tangu kufunguliwa kwa ujumbe wa kiufundi, Taliban wamekuwa wakitaka kupeleka mwakilishi wao mwenyewe Delhi. India tangu wakati huo imewaruhusu mwakilishi wa Taliban, Ikramuddin Kamil, kufanya kazi katika ubalozi wa Afghanistan huko Mumbai.
Baadaye, Taliban waliomba kurahisisha taratibu za visa kwa wanafunzi wa Afghanistan, wagonjwa na wafanyabiashara.
"Mkutano huu wa ngazi ya juu ni hatua ya kimantiki baada ya kufungua ujumbe wa kiufundi na umefuatiwa na mikutano mingine kadhaa katika ngazi ya maofisa. Diplomasia ni njia ya pande mbili,” Amar Sinha, balozi wa zamani wa Afghanistan, aliambia DW.
"Sidhani kama taifa lolote limefikia hatua ya kuitambua rasmi Taliban. Mkutano huu utaonekana kuwa wa manufaa sana kwa utawala wa Taliban, ambao uko chini ya shinikizo la kijeshi na changamoto nyingine kutoka Pakistan kwa sasa,” alisema Sinha.
Mahusiano yaliyovurugika na Pakistan
Ajay Bisaria, balozi wa zamani wa India nchini Pakistan, aliiambia DW kuwa ushirikiano wa kivitendo wa India ni sehemu ya mpango mkubwa na Taliban ambapo India inadai kuwa ardhi ya Afghanistan isitumike kwa shughuli yoyote ya kuipinga India, na badala yake India itarushu ushiriki wenye mipaka na kutoa msaada wa kibinadamu.
"Kwa upande mwingine, Pakistan inaiangalia Afghanistan kama eneo la kijiografia la kujipatia ushawishi wa kimkakati, hasa baada ya Marekani kujiondoa mwaka 2021,” alisema Bisaria.
Soma pia: Taliban yaiomba dunia kuisaidia
Uhusiano wa Taliban na Pakistan umedorora hasa kutokana na masuala yanayohusiana na ugaidi wa mpakani na mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya Pakistan kwenye ardhi ya Afghanistan dhidi ya wanamgambo wa Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP), kundi la wanamgambo ambalo limekuwa likishambulia mara kwa mara vikosi vya usalama vya Pakistan. India imekemea mashambulizi hayo ya anga.
"Hatua hizi kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya sera mbovu ambazo Pakistan imechukua katika kushughulikia majirani zake, kwa kuzingatia malengo madogo ya kijeshi badala ya malengo ya kidiplomasia,” aliongeza.
"India na Taliban wameunda uelewa wa kivitendo. Kwa Waafghani, tofauti kati ya mbinu hizo mbili ni dhahiri,” aliongeza Bisaria.