Ufaransa imejikwaa wapi kwa makoloni yake ya zamani Afrika?
31 Agosti 2023Hatua hiyo inafuatia yaliyotukia nchini Niger hivi karibuni ambako wanajeshi pia wametwaa madaraka.
Rais wa Gabon, Ali Bongo alikuwa anajiweka sawa kuuongeza muda wake wa miaka 14 madarakani baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi iliyopita.
Kwa usemi mwingine familia ya akina Bongo ingelikuwa madarakani kwa muda wa miaka 55 nchini Gabon.
Lakini wanajeshi waliotwaa madaraka wamesema uchaguzi haukutimiza vigezo, haukuwa wazi na wala haukuwa wa kuaminika kama jinsi watu wa Gabon walivyotumai.
Soma pia:Burkina Faso yaidhinisha muswaada wa kutuma kikosi Niger
Wanajeshi hao waliojitambulisha kuwa kamati ya mpito na ya ujenzi mpya wa taasisi, wameeleza kuwa nchi yao ilikuwa inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa.
Wamesema waliokuwamo madarakani hawakuwa wamewajibika na kwamba walisababisha mfarakano wa jamii uliohatarishha kuitumbikiza Gabon kwenye vurumai.
Wamesema wametwaa madaraka ili kulinda usalama wa nchi.
Wachmbuzi: Muundo wa democrasia haukuwa na tija
Mwandishi habari, Bram Posthumus aliyebobea katika masuala ya nchi za Afrika magharibi amesema hatua hiyo inadhihirisha wazi juu ya hatua zinazochukuliwa na wanajeshi za kuangusha serikali katika nchi hizo ni kwamba muundo wa demokrasia katika nchi za magharibi kwenye eneo la Sahel umeshindikana kabisa.
"Kwa sababu muundo huo umeleta faida kwa wachache na si kwa kila mtu.”
Mwandihsi huyo Posthumus amefafanua kuwa demokrasia haikuyazingatia matatizo ya kimsingi ya wananchi juu ya usalama, umasikini na fursa za kiuchumi.
Watu katika nchi ambako wanajeshi wametwaa madaraka wanaamini kwamba wanajeshi hao wataweza kuyatatua matatizo yao.
Soma pia:Gabon: Jeshi lamtangaza Brice Nguema kuwa rais wa mpito
Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Gabon, Nathalie Mezo amesema hatua iliyochukiliwa na wanajeshi nchini Gabon ilikuwa jambo la hatma.
Ameeleza kwamba kwa muda mrefu watu wa Gabon walikuwa wanataka mabadiliko, na ndiyo sababu wengi wamepata faraja kuona mwisho wa utawala wa karibu miaka 60 wa ukoo wa akina Bongo.
Mwanaharakati huyo anaamini, hatua iliyochukuliwa na wanajeshi nchini Gabon ilipangwa tangu siku nyingi.
Nathalie Mezo ameeleza kwamba matokeo ya uchaguzi nchini humo yalikuwa yanajulikana hata kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.
Amesema, imekuwa tangu mwaka 1993. Na mnamo miaka 14 iliyopita dhulma ilionekana dhahiri.
Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi kuugeukia ukoo wa akina Bongo.
Ukoloni unachangia Jeshi kutwaa madaraka?
Mchambuzi wa masuala ya Afrika, hususan ya jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, Emmanuel Bensah amesema sababu ya wanajeshi kuugeuka ukoo wa akina Bongo zinahusiana na historia ya ukoloni.
Alisema changamoto hapa inatokana na ukoloni. Lakini haina maana kwamba nchi zote zimepita njia hiyo ya kutumia mabavu.
Hali inatofautiana kati ya nchi na nchi ingawa tupo katika eneo moja."
Watu katika eneo la Sahel wamekata tamaa juu ya demokrasia, na ndiyo sababu haijaota mizizi kwenye eneo hilo.
Soma pia:Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Afrika walaani mapinduzi ya kijeshi Gabon
Watu wengi wanahisi kwamba wafaransa wakati wote wamekuwa wanasimama upande wa wale wenye mamlaka katika makoloni yake ya zamani.
Na wamekuwa wanafanya hivyo bila ya kujali iwapo viongozi hao walikuwa wanaungwa mkono na wananchi wao.
Nchini Niger, maalfu ya wananchi walishangilia kuangushwa kwa utawala wa rais Mohammed Bazoum.
Mchambuzi wa masuala ya utawala kutoka Nigeria, Ovigwe Egeugu amesema katika nchi ambazo hapo awali zilikuwa makoloni ya wafaransa, viongozi hawajachukua hatua thabiti ili kuboresha maisha ya wananchi wao.
Amesema ikiwa wananchi hawaoni faida ya kuwapigia kura,viongozi hao bila shaka hawawaungi mkono, endapo panatokea migogoro.