1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini mataifa ya Kiarabu yanakataa mahusiano na Israel

31 Agosti 2020

Ilikuwa ni misheni isiyowezekana kwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo: kuyashinikiza mataifa ya Kiarabu kurejesha mahusiano na Israel. Lakini ni machache yaliyo tayari kuchukua hatua hiyo

Bahrain | Besuch US-Außenminister Mike Pompeo
Picha: Reuters/Handout Bahrain News Agency

Ilikuwa ziara tofauti kabisa na nyingine. Pompeo alikuwa kwenye misheni ya kuhakikisha kurejeshwa kwa mahusiano kati ya mataifa ya Kiarabu na Israel, jambo ambalo kwa muda mrefu lilizingatiwa lisilowezekana kutokana na mkwamo wa kisiasa wa mgogo wa Israel na Palestina.

Lakini wiki chache kabla, kile ambacho kilionekana kutowezekana kikafanikishwa na kuanza kufanya kazi: Umoja wa Falme za Kiarabu - UAE ulikubaliana kurejesha mahusiano na Israel chini ya Muafaka uliosimamiwa na Marekani. Mpango huo ulisitisha unyakuzi wa ardhi ya Wapalestina inayokaliwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi na kufungua mlango wa mahusiano mapana kati ya nchi hizo mvili, ikiwemo - siku moja - mahusiano kamili ya kidiplomasia.

Kwenye orodha ya nchi alizotembelea Pompeo, hakuna iliyokuwa muhimu zaidi kuliko Bahrain. Taifa hilo la kisiwa kwa muda mrefu lilishirikiana na Israel katika maeneo mengi ya manufaa kwa pande zote na ilikuwa moja ya nchi za kwanza katika kanda hiyo kuukaribisha mpango huo. Kwa wataalamu wengi, ilikuwa ya pili kwenye orodha ya nchi zinazorejesha mahusiano na Israel.

Kiongozi wa UAE Sheikh Khalifa bin Said al-NahyanPicha: picture-alliance/Photoshot

Hata hivyo, matumaini hayo yalififia wakati Mfalme Hamas bin Isa al-Khalifa wa Bahrain alimwambia Pompeo nchi yake haitasonga mbele na pendekezo hilo la Marekani. Badala yake, Mfalme huyo alisema Bahrain inaendelea kuunga mkono Mpango wa Amani ya Uarabuni unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao unatoa wito wa kuungwa kwa taifa huru la Palestina ndani ya mipaka yake ya kihistoria kwa kubadilishana na kurejesha mahusiano na mataifa ya Kiarabu.

Kuna mengi ya kupoteza

Kwa Bahrain, yapo mengi sana ya kupoteza kama itarejesha mahusiano na Israel bila makubaliano mapana ya kikanda na hasa kutoka kwa mshirika wake wa karibu Saudia.

Mtafiti wa masuala ya Ghuba katika ofisi ya Mambo ya Kigeni ya Baraza la Ulaya - ECFR Cinzia Bianco anasema kusitasita huenda kukachangiwa na sababu kadhaa, ikiwemo wasiwasi wa Saudia kuwa wataonekana kuwa na makosa kama Bahrain itarejesha mahusiano na Israel.

Anasema kama dola kubwa la kikanda na kiongozi wa kidini, Saudia haina uwazi wa kubadilika ambao nchi nyingine ndogo zinao. Kwa hiyo hata kujihusisha kwa karibu na Bahrain kutazusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya makundi ya Kisunni yenye mafungamano na makundi ya itikadi kali, kisiasa wakiongozwa na Uturuki na Qatar, ambao ni mahasimu wa kikanda wa Saudia.

Nani anayefuata?

Wakati harakati za Wapalestina zikiendelea kutengeneza sehemu muhumu katika vuguvugu la umoja wa Kiarabu, watalaamu wanaamini kuwa wengine wachache wanapanga kuufuata mkondo wa UAE.

Bianco wa ECFR anasema haamini kama muafaka wa UAE na Israel unapisha njia ya kuundwa mahusiano rasmi kati ya Israel na Saudi Arabia, Oman, Qatar au Kuwait. Anasema katika mataifa hayo, licha ya kuwepo kwa uungwaji fulani mkono kwa suala la Palestina kutoka ndani ya vijana wa Kiarabu, hasa Saudi Arabia, upinzani kuelekea kurejeshwa mahusiano bado upo juu. Kutokana na hilo, mafanikio ya ujumbe wa Pompeo bado hayapatikani, angalau kwa sasa.