1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini wawekezaji wa Kijerumani wanaona Hatari Afrika?

Daniel Gakuba Keith Walker
2 Desemba 2024

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck yuko ziarani nchini Kenya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika.

Waziri wa Uchumi wa Shirikisho Habeck nchini Afrika Kusini | Picha ya maktaba 2022
Majadiliano na wataalam wa Afrika: Robert Habeck akiwa Afrika Kusini wakati wa ziara yake ya mwaka 2022.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Safari ya Habeck inafanyika wakati wawekezaji wengi wa Ujerumani wakiwa bado wanasitasita, wakitaja mazingira hatarishi kibiashara.

Akiwa nchini Kenya Waziri Robert Habeck atafungua Mkutano wa Biashara wa Ujerumani na Afrika (GABS), ambao hufanyika katika nchi tofauti za Afrika kila baada ya miaka miwili. Hii ndio shughuli kubwa zaidi ya kibiashara ya Ujerumani linayolilenga bara hilo, ikiwaleta pamoja viongozi wa biashara na serikali kutoka Ujerumani na Afrika.

Kulingana na Serwah Prempeh, mtafiti mwandamizi katika programu ya uchumi na jamii ya Taasisi ya Utafiti wa Sera za Afrika (APRI) yenye makao yake mjini Abuja, Nigeria, uwekezaji barani Afrika unakwamishwa na fikra sisizo sahihi na zenye kutiwa chumvi, juu ya mazingira ya kibiashara barani Afrika.

''Katika vyombo vya habari vya Ujerumani, Afrika inapewa sura ya bara lenye misukosuko, lililojaa rushwa na lenye miundombinu duni, lenye vikwazo vya ukiritimba, na la hatari kubwa kwa wawekezaji. Hali hii bila shaka inawaogofya wenye mitaji kutoka Ujerumani, hasa wale wa makampuni madogo na ya kati, ambao kwa kawaida huwa na tahadhari zaidi,'' amesema Prempeh.

Unaweza kusoma pia:

 Mataifa 14 ya Afrika yaanza biashara huria

EU yazindua mkakati wa kibiashara na Afrika

Katika kitabu chake kipya kiitwacho ''Uhuru - Kumbukumbu kutoka 1954 hadi 2021, Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel alizungumzia ugumu wa kuwashawishi wakurugenzi wakuu wa kampuni kubwa za Ujerumani kuandamana naye katika safari zake za nchi za Afrika, akisema wengi wao hawakuona fursa za kuridhisha kwenye masoko ya Afrika.

Ujerumani yaanza kuwafunza wafanyakazi kutoka Kenya

01:43

This browser does not support the video element.

Serikali ya Ujerumani kwa miaka ya nyuma imejaribu mara kadhaa kuzishawishi kampuni ndogo na za kati za Ujerumani kuongeza uwekezaji Afrika. Mipango kama vile Compact with Africa — iliyoanzishwa wakati wa urais wa Ujerumani wa kundi la mataifa yaliyoendelea kiviwanda na zinazoinukia, G20 mwaka 2017 — iliazimia  uwekezaji wa ziada wa kibinafsi katika mataifa ya Afrika ili kukuza uchumi wa nchi za bara hilo.

APRI: Ujerumani haijafanya shughuli nyingi za kisiasa na kiuchumi barani Afrika

Hata hivyo, kulingana na taasisi ya APRI, Ujerumani haijafanya shughuli nyingi za kisiasa na kiuchumi barani Afrika katika miongo ya hivi karibuni. Takwimu za uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje zinadhihirisha hali hii. Ujerumani ilishika nafasi ya tisa kati ya nchi 10 bora kwa uwekezaji Afrika mwaka 2022 na dola bilioni 13  — ni bilioni 2 tu zaidi ya mwaka 2018, kulingana na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD).

Mtafiti Prempeh aliiambia DW kwamba wawekezaji wa Ujerumani kwa ujumla hawako tayari kurusha karata zao bila uhakika wa kupata faida.  Anasema wengi wanangojea msaada wa serikali kuongezeka kabla ya kuwekeza Afrika, msaada ambao yumkini, hauji kirahisi.

Mwaka wa 2022, Habeck alitoa wito wa kuanzisha mbinu mpya za mahusiano kati ya Ujerumani, Ulaya na Afrika kabla ya safari yake ya kwanza barani humo, ambapo alitembelea Afrika Kusini na Namibia.

Unaweza kusoma pia: Rais Xi Jinping wa China ameahidi msaada wa dola bilioni 50 kwa Afrika

Nchini Kenya, Ujerumani inafanya kazi kama mshirika wa kifedha kwa upanuzi wa kituo kikubwa zaidi cha nishati ya jotoardhi barani Afrika kilichopo Olkaria. Alipokitembelea kituo hicho mnamo Mei 2023, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz alitangaza mkopo mpya wa euro 45 milioni. Habeck pia anapanga kutembelea kituo hicho cha nishati, ambacho uwezo wake unatarajiwa kuongezeka mara mbili hadi megawati 2,000 ifikapo mwishoni mwa muongo huu.

Uwekezaji ya Ujerumani kuelekea Afrika na Kenya inakabiliwa na migogoro

Kulingana na mchumi wa Kenya James Shikwati, mbinu ya uwekezaji ya Ujerumani kuelekea Afrika na Kenya inakabiliwa na migogoro ya aina mbili. 

''Mgogoro wa kwanza ni ndani ya Ujerumani yenyewe, ambapo tunafahamu kuwa uchumi wa nchi hiyo unakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na mizozo barani Ulaya, na wa pili unahusu Afrika, ambako Ujerumani inakabiliwa na ushindani mkali kutoka China na nchi nyingine zinazoinukia kiuchumi,'' amesema Chikwati.

Soma pia: Ujerumani kufanya biashara ya nishati na Nigeria

Kwa maoni ya mtaalamu huyu, Wajerumani wanapaswa kushirikiana na wenzao wa Kenya na Afrika badala ya kudhani wao ni wataalamu zaidi. Anasema Afrika inatoa fursa kubwa kwa kampuni za Ujerumani, hasa katika sekta za nishati ya kijani, miundombinu na teknolojia ya mawasiliano.

Hata hivyo, janga la COVID na migogoro mipya barani Afrika zimeathiri uchumi, na wataalamu wanaonya kuwa kupunguza hatari hizi ni muhimu kwa uwekezaji wa baadaye.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW