1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwanini bara la Afrika ni muhimu kimkakati ?

13 Desemba 2022

Wakati viongozi wa Afrika wakihudhuria wiki hii mkutano kati ya Marekani na Bara la Afrika huko mjini Washington, utawala wa Biden umedhihirisha ushindani wake wa kiuchumi na China juu ya bara hilo.

US-Afrika Gipfel in Washington/Ankunft
Picha: Saul Loeb/AFP

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele wa siku tatu kati ya Marekani na Afrika Jumanne hii, Naibu Waziri wa Biashara Don Graves alikiri kwamba China imeipiku Marekani ambayo imerudi nyuma katika masuala ya uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, lakini akasema Marekani inasalia kuwa "mshirika bora" barani Afrika na kwamba makampuni na wawekezaji wa Marekani wanapaswa kurekebisha hali hiyo.

Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh akiwasili nchini Marekani kuhudhuria mkutano huo.Picha: Mandel Ngan/AFP

Wakuu wa nchi kutoka mataifa 49 ya Afrika na viongozi wa Umoja wa Afrika wamealikwa kushiriki katika mkutano huo wa kilele ambao unachukuliwa na utawala wa Biden kama fursa ya kuwahamasisha tena viongozi wa bara hilo.

Soma zaidi:Marekani yaahidi dola bilioni 55 kwa Afrika katika miaka mitatu ijayo 

Bara la Afrika, ambalo viongozi wake mara nyingi wamekuwa wakihisi kupewa kisogo na kupuuzwa na Mataifa yenye uchumi mkubwa, bado ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kutokana na idadi ya watu wake inayokua kwa kasi, utajiri muhimu wa maliasili, na idadi kubwa ya wapiga kura katika Umoja wa Mataifa.

Umuhimu wa bara la Afrika kimkakati

Rais wa Senegal na Rais wa Umoja wa Afrika Macky Sall akiwasili mjini Washington kuhudhuria katika mkutano huo.Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Afrika inabaki kuwa na umuhimu mkubwa wa kimkakati katika kipindi ambacho Marekani ikiwa inarekebisha sera yake ya kigeni kwa kuzingatia zaidi ushawishi wa taifa la China, ambalo linachukuliwa na utawala wa Biden kama mshindani mkuu wa kiuchumi na kijeshi wa Marekani.

Hata kabla ya mkutano huo kuanza rasmi, Ikulu ya White House ilitangaza kuwa Biden anaunga mkono hatua ya Umoja wa Afrika kuwa mwanachama wa kudumu wa Kundi la mataifa 20.

Mshauri wa usalama katika Ikulu ya Marekani Jake SullivanPicha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumatatu, Mshauri wa usalama katika Ikulu ya Marekani Jake Sullivan alisema kuwa utawala wa Biden umeafiki kutumia dola bilioni 55 barani Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, huku fedha hizo zikielekezwa katika sekta mbalimbali ili kukabiliana na changamoto kuu za wakati huu.

Uhusiano wa China na Afrika wakosolewa

Marekani imekuwa ikiukosoa ushirikiano wa Afrika na China. Wakati wa ziara yake nchini Nigeria mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema kuwa "mara kwa mara, mikataba ya kimataifa ya miundombinu kati ya sehemi hizo mbili, imekuwa ikigubikwa na usiri mkubwa na kwamba umekuwa na dhamira ya kile kilichotajwa kuwa ni "kuzibebesha nchi za Afrika madeni yasiyoweza kudhibitiwa."

Wachambuzi wanabaini kuwa kwa muda mrefu sasa Marekani imekuwa ikiiona China kama tishio katika maeneo mengi duniani ikiwa ni pamoja na maeneo ya India na Pasifiki, Amerika Kusini, Mashariki ya Kati na hata barani Afrika ambako wamekuwa wakilenga kuimarisha ushawishi wao wa kijeshi na kiuchumi.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW