1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwanini Iran na Israel ni maadui?

18 Aprili 2024

Iran na Israel zimegeuka kutoka kuwa washirika hadi kuwa maadui wakubwa, hasa baada ya mapinduzi ya Iran. Mahusiano hayo yameingia doa zaidi baada ya Iran kuishambulia Israel hivi karibuni.

Iran/Israel
Bendera ya dola la Iran na Israel Picha: H. Tschanz-Hofmann/IMAGO

Mnamo Aprili 13 Iran iliishambulia Israel kwa droni pamoja na kuifyetulia makombora ambayo yalifanikiwa kudunguliwa na Tel Aviv kwa asilimia 99. Iran ilisema ilikuwa inajibu shambulizi lililodaiwa kufanywa na Israel katika ubalozi wake mdogo mjini Damascus, Syria yaliyotokea Aprili mosi.

Tangu Israel ilipoanzisha vita vyake na Hamas katika ukanda wa Gaza Oktoba 7, pia ilianzisha mashambulizi kwa makundi yanayofadhiliwa na Iran nchini Lebanon na Syria. Shambulio la moja kwa moja la vikundi vinavyofadhiliwa na Iran lilifanyika mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili katika ubalozi huo mdogo wa Iran na kusababisha vifo vya watu 13 wakiwemo makamanda 7 wa ngazi za juu wa Iran.

G7 yalaani mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel

Iran moja kwa moja iliilaumu Israel kwa shambulio hilo japokuwa Israel haikutoa tamko lolote kuhusu tukio hilo. Nchi hizo mbili zimekuwa maadui kwa miongo kadhaa, Iran ikisema inataka kuiondoa israel nje ya ramani na kutishia kuisambaratisha kabisa. Israel nayo kwa upande wake inamuona Iran kama adui na mpinzani wake mkuu.  Lakini hali katika nchi hizi mbili haikuwa hivyo hapo awali.

Ni lini hasa Iran na Israel walikuwa washirika?

Rais wa Iran Ebrahim Raisi Picha: Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Israel na Iran walikuwa washirika hadi pale yalipotokea mapinduzi ya Iran mnamo mwaka 1979. Iran ilikuwa moja ya madola ya kwanza kuitambua Israel baada ya kuanzishwa kwake mwaka 1948.

Israel iliitambua Iran kama mshirika dhidi ya mataifa ya kiarabu. Iran ikaikaribisha vizuri nchi hiyo inayoungwa mkono na Marekani. Wakati huo Israel ikawa inatoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo wa Iran, kutoa usaidizi wake wa kiufundi na kusaidia kuimarisha treni na jeshi la Iran. Na lilipokuja suala la malipo Iran iliishukuru Israel kwa kuipa mafuta maana uchumi wa taifa hilo ulihitaji mno nishati hiyo muhimu.

Israel yakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu vita vyake Gaza

Na sio hayo tu Iran ilitoa hifadhi kwa jamii ya Wayahudi nje ya Israel. Lakini baada ya mapinduzi ya Iran Wayahudi wengi wakaondoka nchini humo. Licha ya hilo hadi leo hii zaidi ya Wayahudi 20,000 wanaishi nchini Iran.

Mahusiano ya nchi hizo yalibadilika lini?

Viongozi wa Baraza la mawaziri linaloshughulikia masuala ya vita Israel likiongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, waziri wa Ulinzi Yoav Galant na kiongozi wa zamani wa pinzani Benny Gantz wote kutoka chama cha Netanyahu cha Likud.Picha: Abir Sultan via REUTERS

Baada ya mapinduzi hayo ya Iran kuiweka serikali ya Ayatollah Ruhollah Khomeini na wanamapinduzi wenzake, Iran iliondoa makubaliano yote ya awali na Israel. Khomeini akaanza kuikosoa vikali Israel kwa kuchukua maeneo ya Wapalestina. Taratibu Iran ikaanza kuwa na matamshi makali dhidi ya Israel kwa nia ya kuwa na mahusiano mazuri na nchi za kiarabu au raia wa mataifa hayo. Utawala wa Iran ulikuwa na nia ya kutanua ushawishi wake katika kanda hiyo.

Iran kuwekewa vikwazo zaidi kufuatia shambulizi lake Israel

Wakati Israel ilipotuma wanajeshi wake Kusini mwa Lebanon mwaka 1982 kuingilia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, Khomeini akatoa jeshi lake la mapinduzi mjini Beirut, Lebanon, kuwaunga mkono wanamgambo wa kishia wa Hezbollah nchini humo. Kundi hilo hadi sasa linaungwa mkono na Iran na limekuwa likijulikana kama moja ya mawakala wa Iran.

Israel, Hamas zakomalia misimamo yao vita vya Gaza

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalianza na machafuko makubwa dhidi ya utawala wa Shah Mohammad Reza Pahlavi aliyeiikimbia Iran Januari 1979 na serikali yake kuondolewa Februari 11 mwaka huo, na hivyo Ayatollah Khomeini kurejea nchini kutoka uhamishoni

Lakini si raia wote wa Iran wanaunga mkono uadui wa nchi hiyo kwa Israel. Baadhi ya wataalamu nchini humo wanasema msimamo wa Iran umeifanya itengwe kimataifa.

Iran inaweza kumudu vita na Israel?

02:02

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW