1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaUlaya

Kwanini juhudi za EU kujitenga na gesi ya Urusi ni ngumu?

8 Mei 2025

Tume ya Ulaya imetangaza mpango wa kumaliza utegemezi wa mafuta ya kisukuku kutoka Urusi ifikapo mwaka 2027. Lakini wataalamu wanatahadharisha kuwa utegemezi mpya na migawanyiko ya zamani vinaweza kuvuruga mpango huo.

Ujerumani Rügen 2024 | Meli maalum ya LNG “Energos Power” yafika katika bandari ya Mukran.
Gesi ya LNG kutoka Marekani sasa ndiyo chanzo kikuu cha ugavi wa EU, lakini wataalamu wanatilia shaka uaminifu wake.Picha: Stefan Sauer/dpa/picture alliance

Baada ya miezi kadhaa ya uchelewaji na ukosoaji mkubwa kutokana na ongezeko la uagizaji wa gesi ya LNG kutoka Urusi, Tume ya Ulaya hatimaye imetangaza mpango wake wa kuondoa kabisa nishati ya kisukuku kutoka Urusi kwenye mchanganyiko wa nishati wa Umoja waUlaya kufikia mwaka 2027.

Jumanne, Kamishna wa Nishati Dan Jorgensen aliwasilisha mpango huo mjini Strasbourg na kueleza kuwa hatua hiyo inalenga kutimiza ahadi za kisiasa kwa hatua halisi za kisheria.

"Tumeweza kuandaa mpango wa kisheria utakaotuwezesha kuondoa kabisa gesi ya Urusi katika nishati yetu,” aliambia DW.

Mpango huo una awamu mbili: Kwanza, kupiga marufuku mikataba mipya ya gesi na Urusi kufikia mwisho wa 2025, na pili, kusitisha kabisa uingizaji wowote uliosalia kufikia 2027. Hata hivyo, kwa kuwa bado Urusi inasambaza kiasi kikubwa cha mafuta ya kisukuku, wataalamu wanabaki kuwa na mashaka.

LNG kutoka Urusi yaendelea kupanda

Ingawa kwa ujumla uagizaji wa nishati ya kisukuku kutoka Urusi umepungua tangu uvamizi wa Ukraine mwaka 2022, uagizaji wa LNG kutoka Urusi uliongezeka kwa asilimia 18 mwaka 2024. EU ilitumia euro bilioni 23 kwa nishati hiyo mwaka huo, kiasi kinachochangia moja kwa moja bajeti ya vita ya Kremlin.

Kamishna wa Nishati Dan Jorgensen ndiye mbunifu mkuu wa mpango wa EU wa kusitisha mtiririko wa gesi kutoka Urusi kuingia katika jumuiya hiyo.Picha: DW

Pawel Czyzak kutoka taasisi ya Ember, anautazama mpango huo kama jaribio la kurejesha kasi ya kisiasa ya kujitegemea katika nishati, ingawa changamoto zimekuwepo tangu mwanzo. Alisema bado gesi ya Urusi ilichangia asilimia 17.5 hadi 19 ya uagizaji wote wa gesi barani Ulaya mwaka 2024.

LNG kutoka Urusi haijajumuishwa kwenye vikwazo rasmi vya Umoja wa Ulaya. Machi 2025, EU ilipiga marufuku usafirishaji wa LNG ya Urusi kupitia bandari zake kwenda nchi zisizo wanachama wa EU, lakini si kwa matumizi ya ndani.

Soma pia:Urusi yataka EU kuiondolea vikwazo ili kurejesha makubaliano

Uagizaji mkubwa wa LNG ya Urusi unaingia Ulaya kupitia Ufaransa, Ubelgiji, na Uhispania. Ufaransa pekee iliongeza uagizaji huo kwa asilimia 81 mwaka 2024, ikiilipa Urusi euro bilioni 2.68.

Kwa mujibu wa Ana Maria Jaller-Makarewicz, kutoka Mfumo wa Ufuatiliaji wa LNG Barani Ulaya wa Taasisi ya Uchanganuzi wa Uchumi wa Nishati na Fedha, IEEFA, gesi hiyo ikishafika kwenye mtandao wa usambazaji haiwezi kufuatiliwa chanzo chake, jambo linalofaidisha wauzaji na wanunuzi.

Changamoto kwa mpango wa REPowerEU

Hali hii inazidi kuathiri mpango wa REPowerEU uliozinduliwa mwaka 2022, uliolenga kupunguza utegemezi kwa Urusi, kuongeza nishati mbadala na kubadili wasambazaji. Lakini Czyzak anaonya kuwa EU sasa inabadilisha mtoaji mmoja hatarishi kwa mwingine – hususan Marekani, ambayo inaishinikiza Ulaya kununua gesi na hata kutishia vikwazo vya kibiashara.

Ujerumani kupunguza tozo ya gesi asilia

01:21

This browser does not support the video element.

Pamoja na juhudi hizi, bei ya nishati Ulaya bado iko juu. Mwaka 2024, bei ya gesi barani Ulaya ilipanda kwa asilimia 59. Ingawa bei zimeanza kushuka baada ya msimu wa baridi kuisha, bado ziko juu sana ikilinganishwa na kabla ya vita — hali inayozidisha mzigo wa gharama kwa viwanda na kaya.

Soma pia: Mzozo wa Urusi na Ukraine waendelea kusababisha matatizo ya kiuchumi

Jaller-Makarewicz anapendekeza badala ya kutegemea waagizaji wapya, EU ipunguze kabisa matumizi ya gesi, hasa kwa kaya za kawaida. Anasema nyumba zilizo na ujenzi bora wa kuzuia upotevu wa joto na matumizi ya paneli za jua zinaweza kusaidia kupunguza mahitaji ya gesi.

Hatua Zinazofuata: Umoja wa Ulaya au migawanyiko?

Mpango wa Tume sasa unaelekezwa kwa nchi wanachama wa EU, ambapo kupitishwa kwake kunahitaji wingi maalum wa kura. Lakini upinzani kutoka kwa nchi kama Hungary, Slovakia na Austria — zinazotegemea sana gesi ya Urusi — unaweza kukwamisha hatua hiyo.

Zaidi ya hayo, kuna hofu kuwa mazungumzo ya siri ya amani ya Ukraine yanayowezeshwa na Marekani yanaweza kuhusisha kupunguzwa kwa vikwazo dhidi ya Urusi — jambo linaloweza kudhoofisha msimamo wa EU.

Kwa sababu hiyo, Jaller-Makarewicz anasisitiza mshikamano: "Ni kwa kusimama pamoja tu ndipo EU itaweza kuimarisha usambazaji salama wa nishati na umoja wake.”

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW