1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiMarekani

Kwanini Marekani iliingia katika mkwamo wa madeni?

6 Juni 2023

Licha ya wajumbe wa vyama vya Republican na Democratic nchini Marekani kufikia makubaliano ya kuondoa ukomo wa kukopa, wachambuzi wanasema muafaka huo haukumaliza mkwamo wa kifedha na kisiasa uliopo.

US-Kapitol | Senat verhandelt Schuldenobergrenze
Picha: J. Scott Applewhite/AP Photo/picture alliance

Wabunge kutoka Republican na wale wa Democratic wameikwamua kwa sasa nchi yao kuondokana na uwezekano wa kushindwa kukopa zaidi kwa kuipa serikali kuu mamlaka ya kukiuka ukomo wa dola trilioni 50 za mkopo, lakini wachambuzi wa bajeti wanasema walichofanikisha hasa ni kubana matumizi ya mambo yasiyo ya ulinzi na usalama, sawa na dola trilioni 6.4 kwa mwaka huu.

Lakini panapohusika malengo ya muda mrefu, makubaliano hayo yameshindwa kulitatuwa tatizo sugu la Marekani, ambalo ni nakisi kwenye mapato yake, yanayohusishwa moja kwa moja na matumizi makubwa kwa huduma za afya na pensheni kwa idadi kubwa ya Wamarekani wanaozeeka na pa kushindwa kwa bunge kupandisha kodi.

Soma: Ahuweni yarejea Marekani baada ya Baraza la Seneti kuuidhinisha mswada kuhusu ukomo wa deni.

"Ikiwa unahofia nakisi na matatizo ya madeni, makubaliano haya hayana maana yoyote," anasema Dennis Ippolito, profesa wa sera za umma na fedha kwenye Chuo Kikuu cha Southern Methodist nchini Marekani.

Wafanyabiashara katika soko la hisa la New York (NYSE)Picha: Angela Weiss/AFP

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kilichopo hasa ni ushindani wa mafahali wawili - upande mmoja Democratic waking'ang'ania sera ya matumizi na upande mwengie, Republican wanang'ang'ania sera ya kodi. Katikati yao hapana chochote kinachoashiria mabadiliko yoyote yale.

Makubaliano ya kusitisha ukomo wa kukopa wa dola trilioni 31.4 hadi Januari 2025unayaweka matumizi kwenye sekta ya ulinzi kusalia mfuto mwaka mzima, na ongezeko la asilimia 1 kwa mwaka wa kifedha wa 2024. Ofisi ya Bajeti ya Bunge la Marekani, CBO, inakisia kuwa hatua hiyo itaweza kuokowa dola trilioni 1.3 kwa muongo mmoja ujao.

Hata akiba hiyo nayo inaweza kutokuwa ya uhakika, kwani Congress inaweza kuachana na kiwango ilichojiwekea cha matumizi ndani ya kipindi cha miaka miwili. Juu ya hayo, makato ya kodi yaliyopitishwa na Republican mwaka 2017 yanafikia ukomo wake mwaka 2025, lakini chama hicho kinapigania yaongezewe muda.

Kibaya zaidi, viwango vya juu ya vya riba vinapandisha gharama ya huduma za deni la serikali, ambazo CBO inakisia zitaongezeka mara tatu zaidi na kufikia dola trilioni 1.4 ifikapo mwaka 2033.

Kwenye majadiliano yao ya ukomo wa deni, Rais Joe Biden na Spika Kevin McCarthy wa Baraza la Wawakilishi walikubaliana kutokigusa kichocheo kikuu cha deni la Marekani, ambacho ni kuongezeka kwa pensheni ya mfuko wa jamii na gharama za mafao ya huduma za afya.

Spika Kevin McCarthy wa Baraza la Wawakilishi Picha: Mandel Ngan/AFP

Gharama za Mfuko wa Jamii zinakisiwa kuongezeka hadi asilimia 67 ifikapo mwaka 2032, huku mpango wa huduma za afya kwa wastaafu zikipanda maradufu, kwani idadi ya Wamarekani wenye umri wa miaka 65 kwenda juu watakuwa wamefikia asilimia 46 ya watu wote, kutoka asilimia 34 ya sasa.Bado kuna vizingiti makubaliano ya ukomo wa deni la Marekani

Programu hizi mbili kwa pamoja zinakula takribani asilimia 37 ya matumizi ya serikali na ndani ya muongo mmoja zitakuwa haziwezi kuendesheka. Programu nyengine zinazohusu wanajeshi wa zamani na watu wa kipato cha chini zinachukuwa nusu ya bajeti ya kawaida.

Kinyume na programu nyengine ambazo fedha zake huwa zimetengwa makhsusi kila mwaka, programu hizi za lazima hutoa mafao kwa wote wanaostahiki kulipwa. CBO inakisia kuwa serikali ya Marekani itatumia dola trilioni 6 kwenye programu hizi kufikia mwaka wa kifedha wa 2033, kutoka trilioni 4.1 mwaka huu.Biden: Majadiliano kuhusu deni la Marekani yamepiga hatua

Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, linaishauri Marekani kupunguza gharama za Mfuko wa Jamii na Huduma za Afya kwa kupandisha umri wa wanaostahiki kupata mafao hayo na kuweka vikwazo mbalimbali, lakini watunga sera wa Washington hawajadili mapendekezo hayo, hasa wakati huu uchaguzi wa 2024 ukikaribia.

Chanzo: Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW