1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kwanini migogoro kadhaa ya kibinaadamu imesahaulika Afrika?

16 Januari 2024

Migogoro barani Afrika imesahaulika na kutoangaziwa hasa kutokana na tahadhari ya kimataifa kupungua. Shirika la misaada la kimataifa la Care limeorodhesha jumla ya majanga 10 ya kibinadamu yaliyosahaulika mwaka 2023.

Watoto wawili wakitembea huko Bor nchini Sudan Kusini
Watoto wawili waliotambuliwa kuwa wakimbizi wakitembea huko Minkaman kusini mwa mji wa Bor nchini Sudan Kusini. Picha ya Februari 27 mwaka 2014Picha: imago images/ZUMA Press

Ripoti ya mwaka 2023 ya shirika la Care International imebainisha kuwa migogoro barani Afrika imekuwa ikipuuzwa, huku habari kuhusu dharura za kibinadamu katika bara hilo zikiwa hazipewi tena umuhimu  katika vyombo vya habari ambavyo vimeelekeza macho yao mahali pengine.

Hii ina maana kwamba masuala kama vile njaa nchini Angola, utapiamlo sugu nchini Burundi na vifo vingi vya watoto katika Jamhuri ya Afrika ya Kati vimekuwa haviangaziwi. Mchambuzi Fredson Guilengue kutoka Wakfu wa Rosa Luxemburg mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini anaelezea kinachosababisha hali hii:

" Ninaamini kwamba umakini huu mdogo unasababishwa kwanza na kuendelea kwa mzozo wa Urusi na Ukraine ambao unapewa umuhimu mkubwa ulimwenguni, haswa katika bara la Ulaya kwa sababu hii inaashiria kurejea kwa vita Ulaya. Hii ina maana kwamba vyombo vya habari vya kimataifa vinajielekeza zaidi Ulaya kuliko barani Afrika. Sababu nyingine mbali na mzozo huo, ni mzozo mwingine wa Israel na Gaza ambao ulizidisha muktadha huu wa kwamba yanayoendelea katika maeneo mengine ya ulimwengu kupewa umuhimu mdogo."

Mchambuzi wa masuala ya kimataifa Fredson Guilengue kutoka Wakfu wa Rosa Luxemburg uliopo mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini: 08.10.2023Picha: Fredson Guilengue

Katika ripoti ya sasa iliyopewa jina "Kuvunja Ukimya", shirika hilo la misaada limeangazia kwa mara ya nane kile ilichokiita "migogoro iliyosahaulika." Kila mwaka, Shirika la Care huorodhesha matukio 10 ya dharura za kibinadamu duniani ambayo hayajaripotiwa. Mnamo mwaka 2022 na 2023, matukio yote hayo yaliripotiwa barani Afrika, na kwa mwaka wa pili mfululizo Angola ikiwa kileleni.

Soma pia: WHO: Watu 130,000 wanakabiliwa na njaa Pembe ya Afrika

Kulingana na shirika hilo, migogoro mbalimbali imesahaulika katika mataifa ya Burundi, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Burkina Faso, Senegal na Mauritania.

Msemaji wa shirika la Care katika bara la Afrika David Mutua, amesema nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa katika orodha hii ya kusikitisha kila mwaka.

Vyombo vya habari kutoangazia migogoro muhimu barani Afrika

Mwanamke ambaye alikuwa akikabiliwa na utapiamlo huko Baidoa nchini Somalia akielekea kwenye kituo cha kutoa msaada wa chakula: Picha ya mwaka 1992Picha: Robert Caputo/Aurora Photos/IMAGO

Care International iliagiza shirika la ufuatiliaji wa vyombo vya habari ya Meltwater kuchunguza makala milioni tano mtandaoni zilizoandikwa kwa lugha ya Kiarabu, Kijerumani, Kiingereza, Kifaransa na Kihispania kuanzia Januari 1 hadi Septemba 30 mwaka 2023.

Kwenye jumla ya orodha ya majanga 48 ya kibinadamu yaliyowathiri zaidi ya watu milioni moja, migogoro kumi ambayo imeangaziwa kwa kiwango kidogo na vyombo vya habari iligunduliwa.

Soma pia: WFP: Sudan hatarini kukumbwa na baa kubwa la njaa

Wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo, Mutua anasema ni makala 77,000 pekee kati ya yaliyofanyiwa uchunguzi huo ndio yaliyoshughulikia majanga ya kibinadamu barani Afrika, huku mada kama filamu mpya ya Barbie, ikiongoza kwenye orodha hiyo kwa kuchapishwa mara 273,279.

Mutua amesema nchi kama Angola iliangaziwa kwa machapisho yasiyozidi 1,000, ingawa inakabiliwa na ukame, mafuriko na njaa ambavyo vimesababisha zaidi ya watu milioni saba kuhitaji misaada ya kibinadamu mnamo mwaka 2023.

Mabadiliko ya hali ya hewa husababisha pia migogoro

Mwanamke Febbie Muleya akimwagilia maji miti aliyopanda kwenye kitalu katika Kijiji cha Limbuwa B, nchini Zambia. Shirika la misaada la kimataifa la CARE limetoa mafunzo kwa wakazi ya namna ya kupanda miti ili kutunza mazingira na kukuza uchumi.Picha: Peter Caton/CARE

Zambia imechukua nafasi ya pili katika orodha hiyo ambapo watu milioni 1.35 wameathiriwa na njaa hasa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hali kama hiyo imeripotiwa pia nchini Burundi ambapo watu hupambana mara kwa mara na mafuriko na ambako takriban watu 70,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na kadhia hiyo. Pia karibu watoto milioni 5.6 katika nchi hiyo ndogo ya Afrika Mashariki wanakabiliwa kwa muda mrefu na utapiamlo. Wakati huo huo, watu wengi katika nchi za Senegal na Mauritania wanakabiliwa pia na tatizo la njaa.

Soma pia:Je viongozi wa Afrika wanatosha kusuluhisha migogoro yao?

Shirika la Care International limeonya kuwa mwaka huu wa 2024, karibu watu milioni 300 duniani kote watahitaji misaada ya kibinadamu, huku karibu nusu ya watu hao wakiwa ni kutoka barani Afrika. Shirika hilo limesisitiza pia kuwa kuna ukosefu wa fedha za kutosha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu ili kuokoa maisha ya watu.

Pembe ya Afrika yakumbwa na ukame mbaya zaidi

02:15

This browser does not support the video element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW