1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kwanini usitishaji vita Kongo hauheshimiwi?

28 Agosti 2024

Mapigano yanaendelea mashariki mwa DRC licha ya serikali kusaini makubaliano ya kusitisha vita na waasi wa M23. Raia wamenasa katika msururu wa vurugu zinazohusisha waasi hao wa M23, vikosi vya SADC na makundi mengine.

DR Kongo Goma 2024 | Watu baada ya mlipuko kwenye kambi ya wakimbizi
Raia ndiyo wanateseka zaidi katika mzozo wa Kongo Mashariki.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mapambano kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya Kongo na kundi la waasi wa M23 yanaendelea mashariki mwa Kongo na yanasogea zaidi karibu na maeneo yenye msongamano wa watu kati ya Ziwa Edward na kaskazini mwa Ziwa Kivu, maeneo yalio karibu na mipaka ya Rwanda na Uganda. Mnamo Jumapili, Agosti 25, baadhi ya ripoti zilionesha kuwa M23 ilikuwa imeuteka mji wa Kirumba, ambao ni kitovu muhimu cha kikanda.

Hiyo ilifuatia M23 kuiteka miji kadhaa, baadhi ya wakati bila hata mapigano, tangu usitishaji mapigano ulivyokubaliwa mwezi Julai. M23 imeyateka maeneo makubwa tangu ilipoibuka tena mwaka 2021. Kundi hilo lililojihami vyema linaaminika kufadhiliwa kijeshi na kivifaa na Rwanda.

''Goma imetengwa kama mji mkuu wa Kivu Kaskazini. Hakuna njia ya kwenda kaskazini kwa sababu Nyiragongo, M23 tayari wameteka eneo hilo," mchambuzi wa kisiasa mwenye makao yake Goma Jack Kahorha aliiambia DW. Alisema njia ya usafiri ambayo imekuwa ikitumiwa kwa ugavi wa mahitaji muhimu imevurugwa.

Tshisekedi: Amani imo mikononi mwa rais atakayemrithi Kagame

07:56

This browser does not support the video element.

Mahusiano ya M23 na Rwanda

Kinshasa inaishutumu Rwanda kuendelea kuwaunga mkono kwa siri waasi wa M23, kuanzia kwenye silaha na risasi hadi wanajeshi. Rwanda inakanusha madai hayo lakini, mwezi wa Februari, ilikiri kwamba ina wanajeshi na mifumo ya makombora mashariki mwa Kongo ili kulinda usalama wake, ikitoa sababu ya kulundikwa kwa vikosi vya Kongo karibu na mpaka wake.

Waangalizi wa mambo wanasema Rwanda inataka kuwa na ushawishi katika eneo kubwa la mashariki mwa DRC kwa sababu za kiuchumi na kiusalama. Eneo hilo lina maliasili muhimu kama vile mbao, madini adimu na dhahabu. Eneo hilo pia lina wanamgambo wa Kihutu wenye itikadi kali, ambao Kigali inawatuhumu kuhusika na mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi.

Soma pia: Mzozo wa DR Kongo wavutia idadi inayoongezeka ya washiriki

Ukiutazama utawala wa rais wa Rwanda Paul Kagame tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, kwa sehemu kubwa umeegemea kujenga itikadi kumhusu yeye mwenye na kukabiliana na kanuni ya kupinga mauaji ya kimbari ambayo Kagame ndiyo mlinzi wake," Daniel van Dalen, mchambuzi wa hatari mwenye makao yake nchini Afrika Kusini aliiambia DW.

Rwanda na DRC zinataka amani

Vurugu za Kongo Mashariki zilizoanza miaka ya 1990, zimesababisha vifo karibu milioni sita. Zaidi ya makundi 120 ya wanamgambo na waasi yanarandara katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tanganyika. Wengi wa waasi hawa wanatenda ukatili na ukiukaji dhidi ya raia, kulinga na Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mapigano yamewahamisha zaidi ya watu milioni 1.7 kutoka makwao huko Kivu Kaskazini, na kusababisha jumla ya Wakongo walioyakimbia makazi yao kutokana na migogoro mingi kufikia rekodi ya watu milioni 7.2.

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda, ambaye alianza muhula mpya hivi karibuni, wameelezea shauku ya kuwepo amani na utulivu mashariki mwa DRC, lakini Kahorha hana matumaini. "Namna hali inavyoendelea sasa, hakuna matumaini ya suluhisho ikiwa amani haitahusishwa," Kahorha alisema, na kuongeza kuwa upande wa mashariki mwa Kongo umekumbwa na mgogoro kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita. "Umekuwa mgogoto usiyoisha.

Waasi wa M23 wamejihami vyema na wana uzoefu wa mazingira ya Kongo Mashariki.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Vikosi vya SADC vyapambana na M23

Lakini mashambulizi ya sasa ya M23 na kutozingatia kwao usitishaji mapigano kunawatia hofu waangalizi. Mashambulizi ya M23 yanakuja licha ya kupelekwa kwa ujumbe wa kijeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, mashariki mwa Kongo ili kupambana na kundi la M23.

Mnamo Desemba 2023, Jumuiya ya SADC ilituma kikosi cha kijeshi kuisaidia serikali ya Kongo kuwaondoa waasi. Hadi sasa, wanajeshi wa SADC wameshindwa kuwazuia waasi wa M23, ambao wanaendelea kuyateka maeneo zaidi.

Soma pia: Kagame aapishwa aksiema amani ya kanda ni 'kipaumbele' cha Rwanda

Akizungumza katika mahojiano maalumu na DW kuhusu kutumwa kwa kikosi cha SADC, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera alisisitiza kuwa kipaumbele cha wanajeshi hao ni kulinda maisha ya watu wasio na hatia.

''Amani ni sharti la maendeleo. Iwe ni vita vya uwakala au kuhusiana na nani aliye na mamlaka juu ya rasilimali hii au rasilimali ile, ni uamuzi unaosema, 'hakikisha kwamba tunalinda jamii zilizo hatarini'.''

Lakini, kikosi cha SADC si cha kulinda amani. Mamlaka ya ujumbe wa SADC ni kupambana kikamilifu na M23," Daniel van Dalen alisema. "Ni sadfa au siyo sadfa kwamba ulikuwa na wanachama wachangiaji kwenye kikosi cha SADC ambao sasa ni walewale waliokuwa sehemu ya kikosi cha Brigedi ya uingiliaji ya Umoja wa Mataifa mwaka 2012, ambacho kimsingi kiliishinda M23. Lakini sasa wanafanya kwa namna yao wenyewe.

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

02:01

This browser does not support the video element.

Huku SADC ikikabiliana na wakala wa Rwanda kwa ombi la serikali ya Kongo (mwanachama wa SADC), ugumu zaidi ya siasa za kieneo unaweza kuibuka. Vikosi vya SADC na Rwanda viliunganisha nguvu kwa mafanikio, kuwafurusha wapiganaji wa itikadi kali kutoka kaskazini mwa Msumbiji.

Hata hivyo, kwa mujibu wa van Dalen, ujumbe wa kijeshi wa SADC mashariki mwa DRC unaweza kuwa mtihani kwa ushirikiano wa baadae. "Havipambani tu (vikosi vya SADC) na waasi. Vinapambana na moja ya majeshi yenye uwezo zaidi barani, kupitia Rwanda, na kundi la waasi ambalo linapatiwa silaha za kisasa," alisema van Dalen, na kuongeza kuwa ukosefu wa msaada wa anga kwa SADC umekwamisha ufanisi wake.