1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

“Kwenye ujasusi, jambo gumu kabisa ni kumsaka mtu mmoja“: Mahojiano na Naibu Mkurugenzi wa zamani wa CIA

9 Agosti 2011

Katika mahojiano na Deutsche Welle, naibu mkurugenzi wa zamani wa CIA anaeleza kazi ngumu ya kumsaka Osama bin Laden. Anazungumzia pia mabishano yanayoendelea juu ya kile kilichotokea Tora Bora.

Picha: DW / AP

John McLaughlin alifanyakazi kama Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kuanzia Julai hadi Septemba 2004 na kama Naibu Mkurugenzi kuanzia mwaka 2000 hadi 2004. Kwa muda wa miaka 30 amekuwa akifanya kazi kwenye shirika hilo akishikilia nyadhifa mbalimbali za juu chini ya wakurugenzi 11 waliowahi kuiongoza CIA.

Mwaka 2010, McLaughlin alitakiwa na utawala wa Rais Barack Obama kuongoza kundi la wataalamu wa usalama wa taifa kuchunguza changamoto za kijasusi kutokana na njama mbili za kigaidi zilizoilenga Marekani hapo mwaka 2009. Kwa sasa McLaughlin ni mstahiki mtendaji wa kituo cha Philip Merrill kinachojihusisha na mitaala ya mkakati katika Chuo Kikuu cha John Hopkins mjini Baltimore.

Deutsche Welle:

Ni lini katika miaka 30 uliyofanya kazi pamoja na CIA, ambapo kwa mara ya kwanza ulisikia kuhusu Osama bin Laden?

McLaughlin:

Binafsi nilianza kumfahamu Bin Laden katikati ya miaka ya 1990. Takriban katika mwaka 1996 tuligundua kuwa Bin Laden alikuwa mtu muhimu anayetoa fedha kwa shughuli za al-Qaida pamoja na harakati za kigaidi.

Kwa wakati huo, alikuwa akisafiri baina ya Sudan na Afghanistan, nami nilikuwa natayarisha tathmini kwa ajili ya serikali ya Marekani. Katika tathmini yetu kubwa ya mwaka 1997, tulimtaja Bin Laden kuwa kitisho kikubwa kwa Marekani. Na baadaye al-Qaida walifanya mashambulizi ya mabomu dhidi ya balozi zetu mwaka 1998 na mashambulizi dhidi ya meli ya kivita ya USS Cole mwaka 2000 na kisha shambulio la Septemba 11.

Deutsche Welle:

Marekani imejaribu na ikashindwa kumpata Bin Laden kabla ya Septemba 11, 2001. Ni kwa njia gani msako dhidi ya Bin Laden ulibadilika baada ya mashambulizi ya Septemba 11?

Aliyewajibika kukumatwa kwa Bin Laden: John McLaughlinPicha: AP

McLaughlin:

Mashambulizi ya Septemba 11 yalikuwa ni mshtuko mkubwa kwa Marekani na kusababisha msako kupata kasi kwa kiasi kikubwa. Kabla mashambulizi hayo, Bi Laden alifanya mashambulizi, lakini yalikuwa dhidi ya maslahi madogo ya Marekani mbali na nyumbani, lakini yalichukuliwa kwa mtazamo wa dhati na serikali ya Rais Clinton. Wakati huo kulikuwa na matatizo kadhaa mengine ambayo Marekani ilikuwa ikiyashughulikia.

Na licha ya kuwa hili lilikuwa na umuhimu, halikuwa na umuhimu wa juu kabisa kama ilivyokuwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11. Baada ya mashambulizi hayo, nguvu nyingi zaidi zilipelekwa kwa mashirika ya kijasusi, ikiwa na maana fedha na watu na tuliweza kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wanaofanyia kazi tatizo hili.

Baada ya tukio la Septemba 11, viongozi wa ngazi ya juu wa al-Qaida walikimbilia milimani katika eneo la Tora Bora baada ya Marekani kuingia nchini Afghanistan.

Deutsche Welle:

Ni vipi Bin Laden aliweza kulikwepa jeshi la Marekani nchini Afghanistan na ulichukua hatua gani baada ya kugundua hilo?

McLaghlin:

Nafikiri hisia za kawaida ni sahihi. Kulikuwa na ripoti za alipo Bin Laden pamoja na udhaifu wake katika mara kadhaa kuanzia 2001 hadi 2011. Kuna wakati tulihisi kuwa tuna taarifa nzuri zinazoelekeza mahala alipo, ingawa sio mahala mahsusi hasa. Na tuliangalia na hatukumpata. Na kwa hiyo taratibu tuliondoa maeneo ambayo yanachunguzwa. Nafikiri katika kipindi hicho hata kama nguvu ya kumtafuta Bin Laden iliendelea, kimsingi lengo lilikuwa ni kuvunja na kuharibu mtandao ambao unamsaidia Bin Laden.

Mtazamo ulikuwa tunapaswa kumtafuta, lakini iwapo tunngeweza kuharibu mtandao wake wa mawasiliano, usafirishaji, maeneo anapojihifadhi, watu wanaotafuta fedha kwa ajili yake, wanaotoa fedha za kumsaidia, sio tu tungekuwa tumemdhoofisha na kupunguza nafasi za mashambulizi ya kigaidi, lakini tungelikuwa tumemtenga na kufanya kuwa rahisi kumpata. Na nafikiri kwa jumla hicho ndicho kilichotokea.

Kwa maneno mengine, naamini hivi sasa kuwa huo ulikuwa mkakati sahihi. Iwapo tungelenga tu kumtafuta Bin Laden bila kitu kingine, huenda tungempata Bin Laden lakini bado tungekuwa na mtandao wa kigaidi wenye nguvu na imara ambao ungekuwa unaendelea. Pamoja na kwamba nafikiri mkakati huu haujapelekea kuuawa tu kwa Bin Laden, lakini pia al-Qaida nzima sasa imekuwa dhaifu.

Deutsche Welle:

Unaweza kutusaidia kuelewa kwa nini ilikuwa vigumu kwa Marekani, pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa taarifa za siri na kijasusi pamoja na kijeshi, kuweza kutambua mahali alipo gaidi mkubwa kabisa duniani?

Baada ya kutafutwa kwa kuda mrefu kulipatikana mahali alipojificha Bin LadenPicha: picture alliance/Ton Koene

McLaughlin:

Katika uzoefu wangu katika mambo ya ujasusi, kitu kigumu sana kufanya ni kumtafuta mtu mmoja. Turejee katika wakati wa vita baridi. Katika vita baridi, kazi yetu katika ujasusi ilikuwa kutafuta mambo makubwa duniani. Ilikuwa kutafuta zilipo silaha za kinyuklia za Urusi ya zamani, nyambizi na mabomu ama vikosi vyenye uwezo wa kuhama vyenye silaha katika mpaka wa Ujerumani.

Katika vita dhidi ya ugaidi, ambavyo vimetushughulisha tangu Septemba 11, kazi yetu ilikuwa kugundua vitu vidogo sana. Bomu katika sanduku ama mtu mmoja katika mji wenye watu milioni kadhaa. Hii ni kazi ngumu sana, hususan wakati mtu huyo anatumia kila njia zote ambazo mtu binafsi anaweza kuzitumia. Kwa mfano, nchini mwetu kulikuwa na mashambulizi katika tukio la michezo ya Olimpiki mjini Atlanta miaka kadhaa iliyopita na iliwachukua maafisa wa Marekani takriban miaka mitatu hadi minne kuweza kumpata mtu huyo katika nchi yetu ambayo ina uwazi wa hali ya juu na udhibiti wa mfumo wa sheria pamoja na nguvu kubwa za kisheria.

Pia kulikuwa na mtu aliyeuwa maafisa wa CIA nje ya makao makuu mwaka 1993 na ilituchukua miaka minne kumpata mtu huyo nchini Pakistan na kumfikisha mahakamani nchini Marekani. Ujumbe hapa ni kwamba nafikiri sio kwamba ilituchukua muda mrefu, lakini ni kwamba hatukukata tamaa.

Deutsche Welle:

Mlitumia muda mrefu ndani ya CIA kuweza kwa mafanikio kumpata mtuhumiwa. Ulijisikiaje wakati unaondoka katika shirika hilo mwishoni mwa mwaka 2004?

McLaughlin:

Nilijisikia vizuri sana, kwa sababu tayari tulishalidhoofisha kundi la al-Qaida kwa kiasi kikubwa. Lengo lilikuwa kuhakikisha hakuna mashambulizi mengine dhidi ya Marekani na hakukuwa na mashambulizi yoyote yaliyofanikiwa dhidi ya Marekani tangu wakati huo. Kwa hiyo tumefanikiwa katika lengo letu kuu kwa mtazamo huo.

Lakini kwa kawaida mtu anaweza kuvunjika moyo iwapo hujamkamata gaidi mkuu. Kwa hiyo, ni kweli kila mmoja alifurahi wakati operesheni hii ilipokuwa imefanya kazi kwa mafanikio. Nafikiri utulivu wa roho kwetu sote kutokana na hilo. Kama watu wengi walivyogundua, ikiwa ni pamoja na viongozi wa CIA, kampeni ya "kamata ama uwa" ilikuwa ya mafanikio kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya taarifa za kijasusi zilizokusanywa katika kipindi cha takribani miaka 15.

Katika operesheni kama hii ni katika kigezo cha utaratibu ulioendelezwa katika muda ambao ushahidi wa binafsi ulianza kuonekana kuwa muhimu. Kwa hiyo tulijihisi kuwa sehemu ya operesheni hiyo.

Deutsche Welle:

Kabla ya kuuawa kwa Bin Laden mwaka huu, hapo mwaka jana mashirika ya kijasusi ya Marekani yalifanikiwa kupata ushahidi muhimu kuhusu alipo Bin Laden. Japokuwa hukuwa tena kwenye CIA, lakini kwa kuwa ulihusika na Shirika hili na unaufahamu ulimwengu wa kijasusi na masuala ya usalama kwa undani, unaweza kutoa maelezo kuhusu kile hatimaye kilichosababisha Marekani kuweza hasa kujua alipo Bin Laden?

McLaughlin:

Hatukufahamu mengi ya kutosha na binafsi sifahamu vya kutosha kuweza kutoa mtazamo sahihi kwa hilo. Inawezekana kulikuwa na mambo mengi ambayo ni siri. Nafikiri huenda kulikuwa na taarifa chache zilizojulikana kuhusu operesheni hii. Nafikiri ni kutokana na kukusanywa ushahidi mwingi katika miaka mingi. Mtu mmoja alisema wakati fulani kwamba ujasusi ni kama kujaribu kutegua kitendawili bila ya kuwa na picha kamili.

Kwa maneno mengine unakuwa na vipande vya taarifa ulivyoviweka pamoja, lakini hujuwi jinsi picha kamili inavyopaswa kuonekana. Na hivi ndivyo kwa kiasi fulani ilivyotokea hapa. Wakati tulipoanza msako, tulikuwa na taarifa nyingi ndogo ndogo, lakini hatukujua jinsi ya kuziunganisha. Baada ya muda, picha inajitokeza wakati ukianza kupata taarifa zaidi. Kwa hiyo, wakati hatua hizi zinafikia mwisho, wakati unapata ushahidi mdogo, unaweza kujaza pengo lililopo na kuweza kupata picha pana zaidi na inaanza kueleweka.

Moja ya vitu muhimu kwa ujasusi ni mara tu ukipata taarifa mpya, unarejea katika hazina yako na kuangalia taarifa za zamani ambazo hazikuwa zinaleta maana kwako na ghafla zinakuwa za manufaa, kwa sababu ushahidi wa mwisho unakubali na unaonekana kutoa picha ya wazi.

Na nafikiri kuwa zilikuwa hatua kama hizo ambazo hatimaye ziliweza kutoa mwanga wa alipo Bin Laden. Sasa fikiria kuwa wakati watu katika utawala nchini Marekani wanasema hawana uhakika wa 100% kuwa alikuwa pale, walikuwa na kiwango kikubwa cha imani kwa msingi wa taarifa za ushahidi wa kimazingira, japokuwa hawakuwa na uthibitisho kamili kuwa alikuwapo mahali hapo. Kwa hivyo, naweza kuhisi tu binafsi na kusema walikuwa na uhakika wa 75% ama 80% kuwa alikuwapo mahali hapo. Lakini hawakuwa na uhakika wa moja kwa moja.

Deutsche Welle: Wakati ulipokuwa unashughulika na mtu kama Bin Laden, ukijaribu kumtafuta na kusoma na kujifunza tabia zake na kila kitu alichokuwa anachofanya ama kusema, uliweza kuwa na uhusiano wa aina fulani na mtu huyu kwa njia fulani. Vipi unaweza kueleza vipi uhusiano binafsi uliokuwa nao na mtu kama Bin Laden?

McLaughlin:

Hakukuwa na mengi kwangu binafsi, kwa sababu naweza kufikiria mengi juu ya watu ambao walikuwa naweza kusema wafanya tathmini wa mstari wa mbele ambao walikuwa wanafanyia kazi hilo. Nilikuwa nafanya kazi katika kiwango cha juu sana. Nilikuwa dhamana kuhusu dunia nzima, Mashariki ya Kati, Asia, Afrika na Amerika ya Kusini. Ugaidi ulikuwa katika ngazi ya juu sana, katika orodha yangu binafsi ya malengo.

Lakini iwapo ninaweza kutabiri juu ya wale ambao walikuwa moja kwa moja wanafanya kazi katika suala hili kila siku, ninaweza kusema kwamba mtu hajengi mapenzi, bali uhusiano wa karibu sana. Lengo la uhusiano huo ni kukusanya taarifa nyingi ambazo unahisi kama unamjua mtu huyo na unakosa vitu vichache vya mwisho kuweza kumfahamu na kuingia ndani ya akili yake kumuelewa aliko na anachofanya. Naweza kukuambia kuwa kwa watu wanaofanya kazi kuhusu suala kama hili, inakubalika kabisa na ni haki yao kuwa na ukaribu sana na mtu wanayemtafuta.

Mtazamo katika CIA baada ya mashambulizi ya Septemba 11, unaweza kujumuishwa katika maeneo mawili: hasira na uvumilivu. Hasira kwa kuwa tumeshindwa kujua lengo halisi la mpango wa al-Qaida. Kwa sababu hatukujua kuwa walikuwa wanapanga mashambulizi wakati huo wa majira ya joto. Tulikuwa na taarifa nyingi za kijasusi zinazoonyesha kuwa tulitarajia mashambulizi, lakini hatukufahamu yangelifanyika wapi.

Kwa hiyo, sehemu ya jinsi tulivyolichukulia ilikuwa ghadhabu, na sehemu nyingine uvumilivu. Ni uvumilivu wa kutotaka tena kutokea kwa tukio kama hilo na kuharibu kundi hili ambalo limesababisha hali hii. Watu ambao walifanyia kazi hilo wameweza kuhamasika kutokana na lengo na kazi yenyewe.

Mwandishi: Michael Knigge/ZPR

Tafsiri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW