Kyagulanyi na Besigye kuungana na vyama vingine vitatu
2 Agosti 2022Hatua hii ya vyama vitano vya upinzani kusaini mkataba wa kimkakati inachukuliwa wiki moja baada ya Rais Museveni kusaini mwingine na rais wa chama cha DP, Norbert Mao na kumteua kwa wadhifa wa waziri. Haijafahamika kama huo ndiyo umewatia hima wanasiasa wa upinzani kuamua kushirikiana ili wasije wakaonekana na wafuasi wao kuelekea mkondo aliochukua Norbert Mao.
Hatua ya viongozi wa upinzani nchini Uganda kusaini mkataba wa ushirikiano imepokelewa kwa maoni mseto.
Watu mbalimbali wamelezea kushangazwa na hatua za ghafla za viongozi hao wawili kuamua kushirikiana ili hali msimu wa uchaguzi uko mbali. Aidha wana mtazamo kuwa ndiyo njia ya pekee kuwafanya wabaki kuwajibika kwa wafuasi wao na kudhihirisha kuwa upinzani ungali una nguvu na ushawishi licha ya wimbi jipya la chama tawala cha NRM kuwashawishi wajiunge kwa kutoa ahadi na zawadi za nyadhifa kwa wale wanaokubali.
Kulingana na mkataba huo wa ushirikiano, vyama hivyo vitaungana katika chaguzi ndogo ndogo zitakazofanyika ili kuwa na mgombea mmoja wa upinzani. Kwa sasa chama cha DP ambacho rais wake Norbert Mao amejiunga na serikali kama waziri wa masuala ya sheria na masuala ya kikatiba kinakabiliwa na tishio la mpasuko.