Lafontaine arejea Saarland
25 Januari 2010Mrengo wa shoto-Die Linke- watumbukia katika bahari ya mizozo na nani asamehe kurejea kazini baada ya mtoto kuzaliwa, mama au baba? Masuala hayo ndiyo yaliyohanikiza magazetini hii leo.
Tuanze basi na uamuzi wa Oscar Lafontaine wa kutopigania tena wadhifa wa mwenyekiti mwenza wa chama cha mrengo wa shoto, Die Linke. Gazeti la "Schwäbische Zeitung" linaandika:
Chama cha Die Linke katika eneo la Mashariki hakijataharuki na uamuzi wa Oscar Lafontaine wa kung'atuka madarakani. Kwa sababu wataendelea vile vile kama walivyokuwa kabla ya muungano kati ya PDS na WASG; chama chenye kiu ya madaraka na kinachovutiwa kushiriki serikalini. Kiunzi cha asili mia tano hawakiogopi huko. Kinyume na katika eneo la magharibi, ambapo linazuka suala la mustakbal wa mrengo wa shoto, Die Linke. Wafuasi wa chama hicho, mchanganyiko wa wakuu wa mrengo wa shoto wa zamani na wanasocial Democratic waliovunjika moyo,wamejijenga upande wa upinzani. Mfalme wa Saar, Oscar Lafontaine, anawashawishi waendelee kubisha. Hivi sasa anajitenga. Kilichosalia ni kundi la wasiokua na mipango- kama baadhi ya wafuasi wa chama hicho wanavyojiita.Uamuzi wa Lafontaine ni kama nukhsi kwa chama cha Die Linke kuelekea uchaguzi wa mwezi May ujao katika jimbo la North Rhine Westphalia. Chama hicho kinaweza kuondoka patupu na kwa namna hiyo kuzidisha mwanya kati ya mashariki na magharibi.
Gazeti la "Der neue Tag linahisi kujiuzulu Lafontaine ni faida kwa Chama cha SPD. Gazeti linaendelea kuandika:
Oscar Lafontaine, anaeangaliwa kama kitambulisho cha Magharibi, amekitumbukiza chama chake Die Linke katika bahari ya mtafaruku. Na pengine hata chama cha SPD. Kinyang'anyiro cha kuania kura za wafuasi wa Lafontaine kinaashiria kuleta natija. Wana SPD wanaolalama,wameshaanza kujipa matumaini.
Gazeti la Badische Zeitung linatathmini yaliyosemwa na mwenyekiti wa chama cha Social Democratic, Sigmar Gabriel, na kuandika:
Hata neno moja linaweza kutafsirika kwa namna nyingi.Pale mwenyekiti wa chama cha SPD alipojibu "la" alipoulizwa kama chama chake kitabadilika,,jibu hilo ni la kisiasa na mara nyingi linamaanisha kinyume chake.Gabriel hataki tuu kuungama.Bila ya shaka Lafontaine alikua kizingiti kikubwa cha kujongeleana SPD na mrengo wa shoto Die Linke.Chama cha SPD kinaweza kwa hivyo kutafakari na kuangalia kama kinaweza kurejea katika enzi zake za zamani kilipokua chama cha umma bila ya kwamba chama cha mrengo wa shoto kigeuke kitisho kwake.
Mada yetu ya pili inahusu ulezi wa watoto.Gazeti la Bild-Zeitung la mjini Berlin linaandika:
Vyama ndugu vya CDU/CSU vimeshaielewa hali ya mambo na vinajiambatanisha na wakati. Kama mwaka mmoja uliopita, makatibu wakuu wa CSU na CDU,DOBRINDT na POFALLA walikubaliana pawepo muda wa miezi minne ambapo baba watawashughulikia watoto na kupokea sehemu ya malipo kwa wazee, jambo ambalo linamrahisishia mtu kufanya kazi kwa muda na wakati huo huo kulipwa mara dufu na serikali. Kristina Köhler,waziri mpya na kijana anaeshughulikia masuala ya familia, anafuata mpango ulioahidiwa wakati wa uchaguzi. Hajabadilisha kitu. Hata hivyo, familia zinafurahia na wakati huo huo sera za familia zinapendwa na wapiga kura, kwa hivyo zinaendelea pia kuwapatia umaarufu wahafidhina.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Inlanadspresse)
Imepiitiwa na:Othman Miraji