Lakhdar Brahimi atangaza kujiuzulu
14 Mei 2014Kwa muda mrefu Bwana Brahimi alikuwa analitafakari wazo la kujiuzulu.Na sasa mjumbe huyo aliekuwa anasuluhisha katika mgogoro wa Syria kwa niaba ya Umoja wa Matifa na jumuiya ya nchi za kiarabu hatimye ameuchukua uamuzi huo.
Brahimi amesema ni jambo la kusitikisha kwamba anaondoka akiiacha Syria katika hali mbaya.Lakini amesema anao uhakika kwamba mgogoro wa nchi hiyo utakwishwa.Lakini amewataka wenye wajibu na ushawishi juu ya Syria waiiulize ni mpaka wafe watu wangapi zaidi, na ni kiasi gani cha madhara kitokee kabla ya Syria iwe tena Syria "tuliyoijua"
"Syria tuliyoienzi"
Bwana Brahimi amesema Syria mpya itakuwa tofauti na Syria ya siku za nyuma lakini itakuwa Syria "tuliyoienzi na iliyotuvutia."
Brahimi hakuwa na njia nyingi.Hayo ameyasema mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati Anthony Cordesman kutoka kituo cha Washington cha masuala ya usalama na mitaala ya kimataifa.
Hata hivyo Brahimi ametoa mchango katika kuyapunguza makali ya maafa kwa raia wa Syria.Lakini hakufanikiwa kusonga mbele katika juhudi za usuluhishi.Lengo lilikuwa mbali kwake kulifikia. Bwana Brahimi ni mjumbe wa pili wa ngazi za juu kushindwa kuleta suluhisho la mgogoro wa Syria.
Alizianza harakati za kusuluhisha baada ya mjumbe wa hapo awali,aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kujiuzulu mnamo mwezi wa Septemba mwaka wa 2012.Yeye pia alivunjika moyo na kujizulu.
Matumaini yazama zaidi
Hata hivyo katika juhudi zake Lakhdar Brahimi alifanikiwa kuwaleta pamoja kwa ajili ya mazungumzo ,mjini Geneva ,wawakilishi wa serikali ya Syria na wa upinzaniLakini tokea Rais Bashar al-Assad atangaze mwezi wa Aprili ,juu ya kufanyika uchaguzi tarehe tatu ya mwezi ujao, utakaokuwa na maana ya kuuimarisha utawala wake, matumaini ya kufikia suluhisho yamezidi kuzama.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ameyapokea kwa masikitiko makubwa maombi ya Bwana Brahimi ya kujiuzulu. Katibu Mkuu Ban amemsifu bwana Brahimi kuwa ni mmoja wa wanadiplomasia mahiri duniani. Katibu mkuu huyo amesema kushindwa kwa Bwana Brahimi kulifikia lengo lake, licha ya tajiriba zake za hali ya juu ni maafa kwa watu wa Syria. Katibu Mkuu Ban amekiri kwamba kushindwa kwa bwana Brahimi ni kushindwa kwa wote.
Atakaefuatia atapaswa kuwa na subira kubwa
Yeyote atakaemfuatia Brahimi atahitaji kuwa na jambo moja awali ya yote- subira kubwa .
Waziri wa mambo ya nje wa Tunisia Kamel Morjane ametajwa kuwa miongoni mwa watu wanaoweza kuichukua nafasi ya Brahimi Mtaalamu kutoka chuo cha Washington cha masuala ya usalama na mitaala ya kimataifa Cordesman amesema yeyote atakaemfuatia Brahimi hatahitaji kuwa mtu mwenye hadhi ya kimataifa kama wajumbe waliotangulia, bali atahitajika awe na uwezo wa kuonyesha imani ,atatakiwa awe mwadilifu na mtu asiegemea upande wowote.
Mwandishi: Musscat,Sabine
Tafsiri:Mtullya Abdu.
Mhariri:Iddi Ssessanga