Lance Amstrong aungama ametumia madawa
18 Januari 2013Bingwa huyo wa zamani wa mashindabo ya kimataifa ya mbio za baiskeli - "Tour de France" ameungama alianza kutumia madawa ya kuimarisha misuli kuanzia katikati ya miaka ya 90 hadi mwaka 2005. Katika mahojiano hayo ya televisheni yaliyotangazwa alfajiri ya leo, Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 41 hakuonyesha dalili zozote za huzuni au fadhaa seuze kuomba radhi kwa hadaa alizofanya.
Alipoulizwa na Oprah Winfrey kama amewahi kutumia madawa marufuku kuzidisha nafasi yako ya ushindi? Lance Amstrong alijibu, "Ndio." Alipoulizwa kama inawezekana kushinda Tour de France bila ya kutumia madawa ya kuimarisha misuli Lance Amstrong alisema" Kwa maoni yake, haamini."
Lance Amstrong ajibebesha dhamana ya yote
Lance Amstrong amesifu timu yake akisema ni ya wajuzi. Amekwepa kusema lakini jinsi timu hiyo inavyoendesha shughuli zake, akiyaacha masuala kadhaa yaliyozushwa na shirika la Marekani la kupambana na matumizi ya madawa ya kuimarisha misuli - USADA bila ya majibu. "Sitaki kumtuhumu yeyote, makosa ni yangu" amesema.
Shirika hilo la USADA limempokonya Lance Amstrong mataji yake yote tangu Oktoba mwaka 2012. Mwenyekiti wa shirika la USADA, Travis Tygart, amesema Amstrong amefanya la maana kukiri kwamba "ushindi wake ulijengeka kwa misingi ya madawa ya kuimarisha misuli na hadaa. "Tygart anapanga kumhoji mwenyewe Lance Amtsrong kuhusuiana na kashfa hiyo. Akishirikiana na shirika hilo, anaweza Amstrong kupunguziwa makali ya marufuku aliyowekewa ya kutoshiriki milele katika mashindano ya kimataifa ya mbio za baiskeli.
Mwenyekiti wa shirikisho la kimataifa la mbio za baiskeli -UCI, Pat McQuaid, amesema kukiri Amstrong kwamba ametumia madawa ya kuimarisha misuli "ni hatua moja muhimu kuelekea njia ndefu ya kuondowa madhara aliyoyasababisha katika mashindano ya mbio za baiskeli ulimwenguni.
Sehemu ya pili ya mahojiano ya Lance Amstrong pamoja na mtangazaji mashuhuri wa televisheni nchin Marekani, Oprah Winfrey, itatangazwa leo usiku.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo