Laporta arejea kuiongoza Barcelona
8 Machi 2021Laporta mwenye umri wa miaka 58, mara ya mwisho alikuwa rais wa Barca kati ya 2003 na 2010, ambapo alisimamia kuteuliwa kwenye mafanikio kwa Pep Guardiola kama kocha na timu ya kihistoria iliyobeba mataji matatu katika msimu wa 2008/2009. Laporta amelipa kipau mbele suala la Messi "Leo anaipenda Barca, na kutufanya tujihisi kuwa familia kubwa. mchezaji bora duniani anaipenda Barca na hilo ni muhimu. Tuna matumaini hilo litasaidia maamuzi tutakayoyachukua baadaye na kumhimiza kuendelea kuichezea Barca kitu ambacho sote tunakitaka."
Kwa jumla, klabu hiyo ilishinda mataji manne ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa wakati wa uongozi wa Laporta wa miaka saba. Amewapiku wapinzani wake Victor Font na Toni Freixa.
Rais wa mwisho Josep Maria Bartomeu alilazimika kujiuzulu Oktoba baada ya wanachama wa klabu kupiga kura ya kutokuwa na Imani naye.
Na wakati Barca ilipata uongozi mpya, ndani ya uwanja mambo yanaonekana kutulia. Hii ni baada ya Atletico Madrid kwa mara nyingine tena kujikwaa katika nafasi yake ya kujiimarisha kileleni mwa ligi kwa kutoka sare ya 1 – 1 na watani wao wa mjini Real Madrid. Sare hiyo imezirejesha mbioni Barcelona na Real. Kocha wa Atleti Diego Simeone ameridhika na pointi hiyo "Katika msimu mgumu, ambao kila mtu alidhani tutashinda ubingwa na pengo la pointi 20 au 15, sijui walichodhani watu, lakini tunacheza dhidi ya timu ngumu kama Real Madrid, Barcelona na Sevilla ambao wana msimu mzuri sana. Ni wazi njia ya kuelekea mwisho wa msimu itakuwa ngumu kwa kila mmoja. tunataka kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita na tupo njiani."
Atletico sasa wanaongoza ligi na pointi 59, pointi tatu mbele ya Barcelona na 56 ambao ilipata ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Osasuna na Real Madrid ni wa tatu na 54. Atleti hata hivyo wana faida ya mechi moja mkononi.
AP, AFP, DPA, Reuters