1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Las Vegas: Trump akwepa suala la umilikaji holela wa silaha

Daniel Gakuba
3 Oktoba 2017

Rais Donald Trump wa Marekani amelaani mashambulizi ya bunduki yaliyouwa watu  59 na kujeruhi wengine zaidi ya 500, lakini amejizuia kusema chochote kuhusu umilikaji holela wa silaha, wala sababu ya mashambulizi hayo.

Donald und Melania Trump Schweigeminute Las Vegas Opfer
Rais Donald Trump na mkewe Melania wakiwakumbuka wahanga wa Las VegasPicha: Reuters/K.Lamarque

Akilihutubia taifa baada ya mauaji hayo jioni ya jana kwa saa ya Marekani, Rais Donald Trump alitoa pole kwa familia zilizoathiriwa na mauaji hayo, na kuhimiza mshikamano wa kitaifa. Aliagiza bendera zote zipeperushwe nusu mlingoti hadi machweo ya Ijumaa, na pia ameahidi kuuzuru mji wa Las Vegas kesho Jumatano. Baadaye, aliwaongoza wafanyakazi wa Ikulu ya White House katika dakika nzima ya kusalia kimya kuwakumbuka wahanga. Lakini, Trump, hakusema chochote kuhusu umilikaji holela wa silaha za moto nchini Marekani. Alisema mauaji hayo ni ubaya wa hali ya juu.

''Ndugu zangu wamarekani, leo tunaungana katika huzuni, na mshituko, na machungu. Usiku wa jana, mtu mwenye bunduki alifyatua risasi katika kundi la wapenzi wa muziki mjini Las Vegas, akaua kikatili watu zaidi ya 50 na kujeruhi mamia wengine. Ulikuwa ubaya mtupu''. Amesema Trump.

Mauaji ya bunduki kitu cha kawaida Marekani

Visa vya mashambulizi ya bunduki vimekuwa vikitokea mara kwa mara MarekaniPicha: Getty Images/D.Becker

Hotuba kama hizi za kuomboleza wahanga wa mauaji ya halaiki yaliyofanywa na mtu mwenye bunduki, zimekuwa kitu cha kawaida kwa marais wa Marekani mnamo miaka ya hivi karibuni. Mwaka 2012 Rais Barack Obama alidodosha chozi baada ya mauaji katika shule ya msingi ya Sandy Hook ambamo watoto 20 wa miaka kati ya sita na saba waliuawa. Kabla yake, Rais George W Bush alijaribu kulifariji taifa baada ya mauaji mengine kama hayo katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Virginia.

Umoja aliouzungumzia Trump baada ya msiba kama huu haukudhihirika katika kauli zilizotolewa na wanasiasa. Hilary Clinton ambaye alishindwa na Donald Trump katika uchaguzi wa Novemba iliyopita, alilikosoa shirika la wamiliki wa bunduki, NRA ambalo kwa kushirikiana na waundaji wa silaha humwaga mamilioni ya dola kulishawishi bunge kuweka sheria zinazorahisisha mauzo ya bunduki, na vizibo vya kuzuia milio ya bunduki kusikika.

''Kuomboleza hakutoshi, tunapaswa kuweka chini tofauti zetu, na kupambana na NRA, na kuhakikisha janga kama hili halitokei tena'', amesema Bi Clinton.

Mtangulizi wa Trump, Barack Obama, ametaka mkwamo kuhusu suala la umiliki holela wa silaha umalizike na bunge kutimiza wajibu wake.

''Sio wakati wa kuzungumza siasa''

Msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Huckabee Sanders, akijibu miito ya wanaokoa ukimya kuhusu umilikaji holela wa bunduki, amesema huu siyo wakati wa kufanya siasa, hiyo ikiwa mbinu inayotumiwa mara nyingi na wale wanaopigia debe uhuru wa kununua silaha, kuzima hasira za umma. NRA iliifadhili kampeni ya Donald Trump kwa dola milioni 30, kwa mujibu wa kituo cha Uwajibikaji katika siasa.

Katika chumba cha hotel cha mtu aliyefanya mashambulizi hayo Stephen Paddock, polisi walikuta bunduki 16, zikiwemo za kivita, na katika msako nyumbani kwake, zilipatikana bunduki nyingine 18. Watu wapatao 33,000 hupoteza maisha kila mwaka nchini Marekani, kutokana na ghasia za Bunduki.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri:Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW