1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Laschet asema muungano wa CDU/CSU wahitaji kujifufua upya

27 Septemba 2021

Mgombea ukansela wa Ujerumani kupitia chama cha kihafidhina cha CDU Armin Laschet, amesema chama hicho kinahitaji kujitathmini na kujifufua upya baada ya kusajili matokeo mabaya zaidi tangu Vita Vikuu vya Pili.

Nach der Bundestagswahl I Armin Laschet I CDU
Picha: Ina Fassbender/AFP

Laschet pia amekiri kubeba dhamana kufuatia matokeo hayo mabovu yaliyosababisha chama chake kushindwa na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto- SPD. 

Katika hotuba yake Jumatatu, Armin Laschet amesema muungano wa CDU/CSU hauwezi kuridhishwa kamwe na matokeo ya uchaguzi wa Jumapili na kuongeza kwamba ipo haja kwa muungano huo kujifufua upya katika kila nyanja.

Hata hivyo, Laschet amesema yuko tayari kuongoza serikali ya mseto akishikilia kwamba hakuna chama chochote kikiwemo SPD ambacho kimepata ushindi wa wazi kuongoza, kutokana na matokeo ya uchaguzi uliofanywa jana Jumapili.

Kulingana na Laschet, yeyote yule atakayeweza kuunganisha vyama pinzani anaweza kuwa kansela.

Kansela anayeondoka Angela Merkel (kushoto) akiwa na mgombea ukansela wa CDU/CSu Armin Laschet.Picha: Martin Meissner/AP/picture alliance

Vyama Ujerumani kuanza mazungumzo kuunda serikali ya mseto

"Yeyote asijifanye kana kwamba wao pekee ndio wanaweza kuunda serikali. Ndiyo sababu mazungumzo na washirika wengine ni muhimu kwa sasa," amesema Laschet.

Laschet amesisitiza kwamba CDU Kiko tayari kwa mazungumzo na chama cha Kijani na kile kinachowapendelea wafanyabiashara FDP kwa uwezekano wa kushirikiana ili kuunda serikali ya mseto.

Alipoulizwa ikiwa atafutilia mbali ushirikiano mpya na SPD, badala yake washirikiane na vyama vidogo, alisema kama wanademokrasia hawafutilii mbali chochote, ila mazungumzo kuhusu ushirikiano na SPD hayafanyiki kwa sasa.

Uhariri: Wajerumani wachagua mabadiliko

Wahafidhina walipata matokeo mabaya katika historia ya chama hicho ya asilimia 24.1, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kupata chini ya asilimia 30. Wakashindwa na SPD waliopata asilimia 25.7.

Laschet ameahidi mageuzi kabambe kwenye chama mnamo wakati mdau muhimu katika chama hicho kansela Angela Merkel ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 16 kama kansela akijiandaa kuondoka.

Kwa upande wa SPD kiongozi wa chama hicho ambaye pia ni mgombea ukansela Olaf Scholz ameelezea imani yake kwamba ataweza kuunda serikali mpya ya mseto akishirikisha vyama viwili vidogo.

Wapiga kura wa Berlin waunga mkono kutaifisha nyumba zinazomilikiwa na makampuni makubwa

Scholz amedai kwamba raia wamejieleza bayana kwa kuimarisha vyama vya Kijani, FDP na SDP na kwamba muungano wa CDU/CSU unapaswa kuelekea upande wa upinzani.

amesema anataka mazungumzo kati ya chama chake na vyama vya kijani na FDP ya kuunda serikali kuanza na kuendelea kwa utulivu.

Wagombea wa siasa pamoja na wachambuzi wamesema mazungumzo hayo huenda yakachukua wiki au hata miezi kadhaa.

Mgombea ukansela kupitia chama cha SPD Olaf Scholz.Picha: Lisa Leunter/AP Photo/picture alliance

Vyama vya Kijani na FDP vimetajwa kuwa na karata muhimu kubaini nani ataunda serikali. Hata hivyo suala ambalo litahitaji kupigwa msasa ni tofauti za ajenda zao kisiasa.

FDP kinataka kizungumze kwanza na watetezi wa mazingira kwa lengo la kuafikiana baina yao kabla ya kushiriki mazungumzo mapana na chama kingine cha tatu kuhusu uundaji serikali.

Kiongozi wa FDP Christian Lindner amesema hayo Jumatatu alipozungumza na waandishi wa habari mjini Berlin.

Chama cha Kijani kinachotetea mazingira kilipata asilimia kubwa kuliko uchaguzi uliopita.Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Tofauti kubwa za kisera ni kati ya chama cha FDP na cha Kijani. Aidha FDP na Kijani ndivyo vyama vinavyopinga hali ilivyo kwa sasa katika serikali ya muungano inayoshirikisha CDU/CSU na vilevile SPD.

Katika taifa ambalo limekuwa tulivu kwa miaka 16 Merkel akiwa usukani, wachambuzi wanasema mvutano wa kisiasa unaweza kutishia kuiweka Ujerumani katika darubini ya ulimwengu kwa muda.

(DPAE, AFPE, RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW