1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Laurent Gbagbo ataka silaha ziwekwe chini haraka

30 Machi 2011

Vikosi tiifu kwa rais wa Côte d'Ivoire anaetambuliwa kimataifa ,Alassane Ouattara vinasonga mbele na kuutia kishindo utawala wa Laurent Gbagbo.

Laurent GbagboPicha: picture alliance / dpa

"Tunatoa mwito silaha ziwekwe chini haraka na kuanza mazungumzo ya amani yatakayosimamiwa na muakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika" amesema hayo msemaji wa  serikali ya Laurent Gbagbo,Ahua Don Mello aliyezungumzia juu ya mwaliko walipokea kutoka Umoja wa Afrika kuhudhuria mazungumzo ya amani April nne ijayo mjini Addis Ababa."Hatukujibu bado lakini hakuna sababu ya kukataa kuzungumza."Ameongeza kusema Ahua Don Mello.

Lakini hata kabla ya kambi ya Gbagbo kutoa mwito uhasama ukome,Alassane Ouattara na wafuasi wake walisema katika taarifa yao tunanukuu:Njia zote za amani za kumtanabahisha Laurent Gbagbo akiri kwamba ameshindwa hazijasaidia kitu."Mwisho wa kunukuu.

Hii ni mara ya kwanza kwa kambi ya Ouattara kutanguliza mbele ufumbuzi wa kijeshi ili kumaliza mgogoro uliosababishwa na uchaguzi wa rais na kugharimu maisha ya watu wasiopungua 460 pamoja na kutishia kuitumbukiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchi hiyo inayosafirisha kwa wingi kabisa cacao ulimwenguni.

Rais anaetambuliwa kimataifa OuattaraPicha: AP

Kwa mujibu wa balozi wa Côte d'Ivoire nchini Ufaransa,Ally Coulibaly,vikosi vya Alassane Ouattara vinadhibiti  robo tatu ya ardhi ya nchi hiyo.

Mapigano yaliyoanza jumatatu yamepelekewa kutekwa miji kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na Bondoukou,upande wa mashariki,Abengourou,kusini mashariki,Daloa,upande wa kati- magharibi na Douekoue katika njia panda inayoelekea katika bandari muhimu  ya San Padro.

Katika wakati ambapo karibu watu milioni moja wametawanyika nchini humo,laki moja na 12 elfu wamekimbilia Liberia,Umoja wa mataifa unajiandaa kukabiliana na wimbi la wakimbizi wa Côte d'Ivoire nchini Ghana.

Mjini Abidjan hali inatisha.Mapigano yameripotiwa umbali wa kilomita 40 toka mji mkuu huo wa kiuchumi wa Côte d'Ivoire.

Rais Obama wa MarekaniPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama  amesema katika mahojiano pamoja na kituo cha televisheni cha NBC Laurent Gbagbo anawatumia "wahuni" ili kuendelea kung'ang'ania madaraka.

Navyo vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa nchini Côte d'Ivoire, vimewalaumu wanajeshi tiifu kwa Gbagbo kwa kuwafyetulia risasi raia wasiokua na hatia katika mtaa wa Williamsville na kuwauwa watu dazeni moja."

Msemaji wa serikali ya Gbagbo amekanusha ripoti hiyo na kusema imepotoshwa na vikosi vya Umoja wa mataifa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,Reuters

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW