1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Lavrov: Magharibi na Ukraine zataka kuiangamiza Urusi

27 Desemba 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameishutumu Ukraine na washirika wake wa Jumuiya ya kujihami ya NATO kutaka kuidhoofisha nchi yake katika uwanja wa mapambano ili kuiangamiza.

Minister Sergey Lavrov trifft  Esteban Lazo Hernandez
Picha: Russian Foreign Ministry Press Service/AP/picture alliance

Sergei Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Urusi amesema matendo ya nchi za Magharibi pamoja na kumdhibiti rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, vyote vinathibitisha hali ya mzozo wa Ukraine ulimwenguni.

Ameliambia shirika la habari la Urusi Tass kwamba si siri kwa yeyote yule kwamba lengo la kimkakati la Marekani na washirika wake katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO ni kuishinda Urusi katika uwanja wa mapambano kama njia ya kuidhoofisha au kuiharibu Urusi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, alianzisha uvamizi nchini Ukraine mnamo Februari 24 akiutaja kuwa operesheni maalum ya kuutokomeza 'Unazi' mamboleo na matendo ya kijeshi ya Ukraine aliyosema yalikuwa kitisho kwa Urusi.

Ukraine yatuma tena ndege zisizo rubani ndani ya Urusi

Kwa upande mwingine, Ukraine na washirika wake wa Magharibi wanasema uvamizi wa Urusi ulikuwa tu unyakuzi wa ardhi kwa njia ya ubeberu.

Lavrov alikariri kuwa Urusi na Marekani haziwezi kuendeleza uhusiano wa kawaida, huku akiulaumu utawala wa rais wa Marekani Joe Biden kwa kupanga mkakati wa kuishinda Urusi kama lengo lake maalum.

Aliongeza kuwa makabiliano ya Marekani dhidi ya Urusi yanaendelea kutanuka na kuwa mabaya.

Biden aapa kuimarisha msaada kwa Ukraine

Zelensky: Hali mashariki mwa Donbas ni ngumu na ya kusikitisha

Afisa wa kupambana na moto akijaribu kuzima moto kwenye jengo baada ya shambulizi la angani la Urusi katika mji wa Kherson.Picha: Dimitar Dilkoff/AFP

Miongoni mwa kauli za Lavrov zilizochapishwa na TASS, aliipa Ukraine masharti ya kutimiza mapendekezo ya Urusi ili kusuluhisha mzozo wao la sivyo jeshi la Urusi ndilo litaamua suala hilo.

Huku uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ukiendelea, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema hali katika eneo la mashariki mwa jimbo la Donbas ni ngumu na ya kusikitisha.

Alisema pia kuwa uhaba wa nishati umeendelea kuwaacha takriban watu milioni tisa taabani.

"Kwanza, eneo la mbele la makabiliano. Bakhmut, Kreminna na maeneo mengine ya Donbas, kwa sasa yanahitaji nguvu kamili. Hali huko ni ngumu na ya kuhuzunisha. Wanyakuzi wanatumia rasilmali zao zote ili wapate angalau mafanikio," amesema Zelensky kwenye hotuba yake ya kila siku kwa Waukraine siku ya Jumatatu.

Ukraine yataka mkutano wa kilele wa "amani"

Dmytro Kuleba, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine.Picha: Efrem Lukatsky/AP/dpa/picture alliance

Katika tukio tofauti, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba serikali yake inataka mkutano wa kilele wa 'amani' miezi miwili ijayo, katika Umoja wa Mataifa, na katibu mkuu wa umoja huo Antonio Guterres ndiye awe mpatanishi.

Umoja wa Mataifa tayari umetoa jibu lakini kwa njia ya tahadhari. Msemaji mshirika wa umoja huo Florencia Soto Nino-Martinez, amesema "Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewahi kusema mara kadhaa kwamba anaweza kuwa mpatanishi ikiwa tu kila upande utamtaka awe mpatanishi.

Putin asema yuko tayari kwa majadiliano kuhusu Ukraine

Kuleba aliongeza kuwa ni sharti Urusi iwajibishwe kwa uhalifu wa kivita kabla ya mazungumzo yoyote kati yao.

Vita hivyo vikiendelea, mnamo Jumatatu, Urusi ilisema ilizuia shambulizi jipya la Ukraine lililolenga kambi ya kijeshi ya kimkakati ya Urusi iliyoko umbali wa mia kadhaa kutoka mpaka kati yake na Ukraine.

Urusi ilisema iliangusha ndege isiyokuwa na rubani iliyokuwa ikitumiwa kufanya shambulizi hilo.

Siku hiyo hiyo, shirika la ndani la usalama nchini Urusi lilisema liliwaua "wahujumu" wanne wa Ukraine, waliodaiwa kujaribu kuingia Urusi kupitia mpaka huo.

Bajeti ya kijeshi ya Ujerumani yapindukia dola bilioni 8.9

Ujerumani imeipa Ukraine mfumo wa ulinzi aina ya IRIS-T, ikiwa ni miongoni tu mwa zana nyingine imekuwa ikiipa Ukraine.Picha: Diehl Defence/abaca/picture alliance

Vita nchini Ukraine vimeathiri ulimwengu kwa njia mbalimbali. Nchini Ujerumani, serikali imeidhinisha usafirishaji wa silaha zenye thamani ya dola bilioni 8.9 mwaka huu. Hiyo ikiwa bajeti ya juu kwa mara ya pili mwaka huu.

Zaidi ya robo ya silaha hizo na vifaa vingine vya kijeshi vilipelekewa Ukraine kati ya Januari 1, hadi Disemba 22, katika juhudi za kukabili uvamizi wa Urusi.

Data hiyo imetolewa na wizara ya Uchumi kufuatia ombi la mbunge Sevim Dagdelen wa chama cha Linke. Shirika la habari la Dpa limepata nakala ya data hiyo.

vyama vya mseto vinavyotawala Ujerumani viliahidi kupunguza matumizi ya kijeshi vilipochukua uongizi mwaka 2021. Lakini vita vya Ukraine vilibadili hali.

Kwa ulinganisho na miaka 16 ambayo Angela Merkel aliiongoza Ujerumani kama kansela, matumizi ya kijeshi zaidi ya kikomo cha bilioni 6, yalishuhudiwa mara tano pekee.

Vyanzo: (RTRE, APE, AFPE, DPAE)