1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lawama za Trump dhidi ya Ujerumani Magazetini

Oumilkheir Hamidou
31 Mei 2017

Lawama za rais mpya wa Marekani Donald Trump dhidi ya Ujerumani, msimamo wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kuelekea mazungumzo ya Brexit na nyuso mpya katika uongozi wa chama cha Social Democrat, magazetini

G7-Gipfel - Trump und Merkel
Picha: Reuters/T. Gentile

Tunaanza na kishindo kilichosababishwa na lawama zinazotolewa na rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya sera za kibiashara za Ujerumani. Gazeti la "Die Welt linahisi kama wamarekani wanapendelea zaidi kununua magari ya Ujerumani sababu kuu ni kwamba magari hayo ni bora zaidi". Gazeti linaendelea kuandika: "Hakuna anaeubisha ule usemi "America First"yaani Marekani kwanza. Kila nchi inaweza kusema hivyo hivyo. Lakini pale rais wa Marekani anapokasirika eti magari mengi ya Ujerumani yanaingia Marekani kuliko yale ya Marekani yanayoingia Ujerumani, hapo hasira zake haziwezi kueleweka. Mahitaji ya magari yaliyotengenezwa Ujerumani au "Made in Germany" nchini Marekani chanzo chake ni kimoja tu: Magari ya Ujerumani ni bora zaidi kuliko ya Marekani. Mnamo miongo kadhaa iliyopita viwanda vya Marekani vilifungwa na shughuli za kutengeneza magari kuhamishiwa nchin za nje. Tatizo sio magari mengi ya Ujerumani yanayonunuliwa Marekani, bali magari machache ya Marekani yanayoweza kupata wanunuzi nchini Ujerumani. Bora tuwasaidie wamarekani, kwa kununua magari ya chapa za Chrysler, Ford na General Motors. Si mabaya hivyo na kwa namna hiyo tutachangia kuimarisha urafiki kati ya Ujerumani na Marekani."

Theresa May aahidi kisichotekelezeka

Kampeni za uchaguzi wa bunge zimepamba moto nchini Uingereza. Kitovu cha kampeni ni uamuzi wa waingereza kujitoa katika Umoja wa ulaya. Misimamo inatofautiana kati ya vyama vya kisiasa kuhusu suala hilo. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linachambua msimamo wa waziri mkuu Theresa May kuhusu Brexit. "Ni Mbinu tu za waziri mkuu Theresa May anaesema eti angependelea zaidi kutolipa chochote na kwamba mazungumzo ya kujitoa katika Umoja wa ulaya yasingelazimika kuitishwa. Anajua fika lakini anapendelea kuuficha ukweli wiki moja kabla ya uchaguzi.  Utaratibu wa kujitoa katika Umoja wa ulaya bila ya mwongozo ungekuwa na madhara makubwa kwa nchi hiyo. Baadhi ya waingereza wanaoishi katika nchi za Umoja wa ulaya wanabidi warejee nyumbani. Makampuni ya kiuchumi ya Uingereza yatawapoteza washirika wao wakubwa. Na kutokana na ushuru bidhaa za Uingereza zitakazoingizwa sehemu ya bara ya Ulaya hazitonunulika."

SPD wafanya mageuzi baada ya Erwin  Sellering kujiuzulu kwa sababu za afya

Mada yetu ya mwisho inahusiana na tangaza la kujiuzulu waziri mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern Erwin Sellering kutokana na maradhi na jinsi uamuzi huo ulivyobadilisha sura ya  mambo katika uongozi wa chama cha Social Democrat-SPD. Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linaandika: "Kwamba tangazo kama hilo la kuhuzunisha linafuatiwa siku hiyo hiyo na mkakati wa kubadilisha nafasi za uongozi, hilo halikumstahiki hata kidogo Erwin Sellering. Hata hivyo ni ukweli kwamba tangazo la kujiuzulu waziri mkuu huyo ambae ni kipenzi cha umma katika mwambao wa eneo la Ostsee limezusha kishindo.Kwa kuzingatia uchaguzi mkuu unaokuja, uamuzi wa kufanya mabadiliko katika uongozi hautasaidia pakubwa. Kuteuliwa Hubertus Heil kuwa katibu mkuu hilo sio suala muhimu: Muhimu zaidi ni SPD wanajiandaa vipi kuwahamasisha wafuasi wake kuweza kumtoa madarakani Angela Merkel?"

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW