1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon baada ya uchaguzi wa bunge

Miraji Othman8 Juni 2009

Mtihani mgumu kwa Lebanon baada ya uchaguzi

Saad al-Hariri, kiongozi wa kundi lililoshinda katika uchaguzi wa bunge la LebanonPicha: AP

Hizo ni sauti za wapiga kura wa Lebanon, mmoja akisema amepiga kura kwa ajili ya Lebanon, na mwengine akisema amepiga kura kutaka mabadiliko.


Jee uchaguzi huo wa bunge mwishoni mwa wiki iliopita ulikuwa uteuzi baina ya Vita na Amani, kama vile alivosema mwanasisa mmoja wa huko Libanon? Au jee uchaguzi huo ulikuwa zaidi kuhusu mgawo wa madaraka katika siku za mbele kwenye bunge la Beirut na ushindi wa kundi lolote ni wenye umuhimu wa alama tu ya kisiasa? Katika uchaguzi huo wa nchi hiyo ya Kiarabu, ambayo pia ina umuhimu mkubwa katika mchakato mzima wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati, kundi la vyama vya kisiasa vinavoungwa mkono na nchi za Magharibi, kwa mshangao, lilikishinda Chama cha Hizbullah na washirika wao. Hata hivyo, walioshinda sasa wanakabiliana na kazi kubwa ya kulibakisha taifa hilo likiwa limeungana...


Muungano wa vyama vinavoipinga Syria, ukiongozwa na Saad al-Hariri, mtoto wa kiume wa waziri mkuu wa zamani aliyeuliwa, Rafiq al-Hariri, ulijipatia viti 71 dhidi ya viti 57 vilivokwenda kwa Chama cha Hizbullah na washirika wake wa kutokea madhehebu ya Shia na pia ya Kikristo. Baada ya kujulikana ushindi huo, Saada al-Hariri alisema hiyo ilikuwa ni siku kubwa kwa Lebanon...

"Nawapongeza wote ambao leo wamepiga kura. Hakuna mshindi na aliyeshindwa katika uchaguzi huu. Ilioshinda pekee ni demokrasia na mshindi mkubwa kabisa ni Lebanon."

Aliyasema hayo huku fataki na fashifashi zikizagaa katika anga ya mji mkuu wa Beirut, hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa..

Lakini wachunguzi wa siasa wanajiuliza kama makundi yanayopingana ndani ya Muungano ulioshinda yataweza kuunda serekali ya Umoja na kuhakikisha kwamba Lebanon haiingii katika duru nyingine ya michafuko ya kisiasa na uhasama wa kimadhehebu ya dini.

Kabla ya uchaguzi huu, wachunguzi walikisia kwamba pande zote mbili zilzoshindana zilikuwa na uzito wa kisaiasa karibu sawa. Upande mmoja kulikuweko Muungano wenye muelekeo wa nchi za Magharibi, ukiongozwa na vyama vya kisiasa vilivo na wafuasi wengi wa madehehbu ya Sunni, chini ya uongozi wa waziri mkuu, Fuad Siniora, na Saad al-Hariri. Katika upande mwengine, kulikuwemo Chama cha Hizbullah, kinachosaidiwa na Syria na Iran, kikiwa na ushirikiano na chama cha mwanasiasa wa Kikristo, Michel Aoun, jenerali wa zamani aliyewahi kuwa adui mkubwa wa Syria. Yeye alirejea Libanon baada ya kuweko uhamishoni kwa miaka 15.

MLibanon , kwa jina la Ahmed, alisema hivi:

" Hisia za watu ni kwamba lazima tuende tukapige kura kutokana na matatizo yaliotokea mnamo miaka minne iliopita. Nchi imegawika, nusu moja inataka kuwa na maisha ya heshima, kukiweko nafasi za mutakbali na daima kuweko nafasi za kazi. Upande mwengine unajaribu kuifungamanisha nchi yetu na Iran pamoja na Syria, na, kwa mujibu wa maoni yangu, ni kwamba zaidi ya nusu ya Wa-Libanon wanalikataa jambo hili."

Watetezi 587 walipigania viti 128 vya bunge, na viti hivyo viligawanywa baina ya mkundi 16 ya kidini, Wasunni, Washia, Wa-Druz pamoja na madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Huo ni mfumo uliowekwa kwa miongo ya miaka nchini humo. Ikumbukwe kwamba hata nyadhifa za juu huko Libanon hugawiwa kwa misingi ya madhehebu ya dini. Rais anakuwa ni Mkristo wa madhehebu ya Maronite, waziri mkuu ni wa madhehebu ya Kiislamu ya Sunni, na spika wa bunge kutoka madehebu ya Kiislamu ya Shia. Mara hii wasiwasi ulikuweko juu ya matokeo ya ushindani baina ya kundi linalotawala la waziri mkuu Fuad Siniora na lile linaloongozwa na Chama cha Hizbullah, kwa vile Jeneral Michel Aoun na chama chake cha Kikristo alikiunga mkono Chama cha Hizbullah cha Sheikh Hassan Nasrallah.

Wa-Libanon milioni 3.2 walikuwa na haki ya kupiga kura, japokuwa waliokwenda kutumbukiza kura zao kwenye masanduku walifikia tu asilimia 54 ya hao. Hata hivyo, hiyo ni idadi kubwa kabisa angalau tangu kumalizika vita vya kienyeji vya nchi hiyo baina ya mwaka 1975 hadi 1991. Wa-Libanon wengi wanaishi nchi za ngambo, kwa hivyo wale waliotaka kupiga kura iliwabidi wasafiri na kurejea nyumbani ili kuitimiliza haki hiyo. Wachunguzi 200 wa kimataifa waliuangalia uchaguzi namna ulivoendeshwa, na wote yaonesha wameridhika na hali ilivokuwa. Licha ya hayo, wanajeshi na polisi 50,000 waliwekwa katika maeneo tete ya nchi, lakini hamna visa vikubwa vya uvunjaji wa sheria vilivoripotiwa, baada ya viongozi wa kisiasa kutoa miito watu wawe watulivu.

Kwa hakika kwa muda mrefu sasa kumekuweko mawaziri wa Chama cha Hizbullah ndani ya serekali ya Lebanon, jambo ambalo halijazifurahisha sana serekali za Marekani na pia Israel. Ilivokuwa sasa kambi inayopendela nchi za Magharibi imeshinda, kuna wasiwasi kwamba kunaweza kukatokea michafuko kama ile ya mwaka jana. Wakati huo walikufa watu mia moja katika mapigano baina ya makundi ya watu wenye silaha kutoka madhehebu ya Sunni na Shia

Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, akiongoza kikundi cha waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi huo, alikuwa na haya ya kusema:

"Waangalizi wa kimataifa wanazitarajia na kuzitaka pande zote kutambua matukeo ya uchaguzi. Tunataraji pia Marekani, Iran, Saudi Arabia na nchi nyingine zitayakubali matukeo."

Lakini magazeti ya Syria yalilalamika kwamba kulikuweko ununuzi wa kura na udanganyifu katika uchaguzi huo wa bunge la Lebanon. Gazeti la al-Watan linalojitegemea liliandika kwamba huo ulikuwa uchaguzi muhimu wa kisiasa katika historia ya Lebanon, na fedha zilizopakwa rangi ya kisiasa zilikuwa na kauli ya mwisho.

Lakini, licha ya kukubali kushindwa, chama cha Hizbullah kinachoungwa mkono na Iran na Syria, na ambacho kimeorodheshwa na Marekani kuwa ni jumuiya ya kigaidi, kinabaki bado kuwa ni nguvu imara ya kisiasa katika Lebanon na kina jeshi kubwa la wanamgambo. Huenda kushindwa kwake kunatokana na hofu ya wapiga kura kura kwamba chama hicho kingeweza kuitangaza Lebanon kuwa dola ya kiislamu, kuifanya izitegemee zaidi Iran na Syria, na kutengwa kimataifa. Nchi za Magharibi zisingestahamilia kuendelea kuisaidia, kifedha, na kwa misaada ya vifaa vya kijeshi Lebanon pindi ushirika wa Hizbullah, unaoongozwa na Hassan Nasrallah, ungeshinda. Pia Saudi Arabia na nchi nyingine tajiri za Ghuba huenda zingejizuwia kuisaidia Lebanon inayoongozwa na Hizbullah.

Mshabiki mmoja wa Hizbullah akiwa anaelekea kupiga kura, alisema:

" Serekali ya taifa ya Hizbullah inafuata njia inayotakiwa na Wa-Lebanon, sio njia inayotakiwa na nchi za kigeni, Wa-Israeli, Wamarekani au nchi za Magharibi."

Lakini Hizbullah imeshatoa onyo wazi kwamba haitakubali ikiwa serekali mpya itajaribu kukinyanganya silaha zake, kikisema silaha hizo ni muhimu katika kupambana na Israel, na jambo hilo si la majadiliano. Washirika wakubwa wa Kikristo wa Chama cha Hizbullah, vuguvugu la wazalendo walio huru la Michel Aoun, wamekiri kushindwa, na wamekula kiapo kwamba watashirikiana na washindi wa uchaguzi katika kuunda serekali.

Inangonjewa serekali mpya iundwe, na hapo itajulikana mitihani gani serekali hiyo itakabiliana nayo.

Bila ya shaka matokeo haya ya uchaguzi yanafuatiliwa kwa hamu na nchi zilizo jirani na Libanon na jamii ya kimataifa, ikijulikana kwamba nchi hiyo ilipitia miaka ya vita vya kienyeji na mizozo mibaya ya kisiasa. Nayo Israel, ambayo ilipigana vita vikali na wapiganaji wa chini kwa chini wa Chama cha Hizbullah, imesema serekali mpya ya huko Beirut lazima izuwie mashambulio yanayofanyiwa Israel kutokea ardhi ya Lebanon. Kama hilo litawezekana, tusubiri na tuone.


Mwandishi:Othman Miraji

Mhariri:Thelma Mwadzaya