1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon: Hezbollah, waandamanaji dhidi ya serikali wapambana

Daniel Gakuba
25 Novemba 2019

Yametokea makabiliano kati ya waandamanaji wanaoipinga serikali ya Lebanon, na wafuasi wa makundi mawili ya wanamgambo wa Kishia katikati mwa mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Polisi imeingilia kati kwa mabomu ya machozi.

Libanon l Anti-Regierungsproteste in Beirut
Picha: Reuters/A. M. Casares

Vyombo vya habari nchini Lebanon vimeripoti kuwa wafuasi wa makundi hayo ya Kishia, Hezbollah na Vuguvugu la Amal, wamewashambulia wandamanaji waliokuwa wameweka vizuizi katika barabara kuu ya mjini Beirut.

Kituo cha habari cha Annahar kimesema kuwa wafuasi wa Hezbollah wamewasili wakitumia bodaboda, wakiwa wamejihami kwa marungu na nondo, wakiimba kaulimbiu za kundi lao. Waandamanaji walijibu kuwa walikuwa wakitaka amani.

Kwa muda wa masaa kadhaa, watu wa pande hizo pinzani walirushiana mawe, kabla ya jeshi ya jeshi na kikosi cha polisi cha kupambana na ghasia kuingilia kwa kufyatua mabomu ya kutoa machozi, na kufanikiwa kuyatenganisha makundi hayo.

Uharibifu mkubwa mitaani

Watumiaji wa mitandao wa kijamii wameweka picha za magari yaliyoharibiwa, na mahema ya waandamanaji yaliyosambaratishwa. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba, wafuasi wa Hezbollah na vuguvugu la Amal pia walishambulia na kuvunja mahema yaliyokuwa yamewekwa na waandamanaji dhidi ya serikali. Makundi hayo, Hezbollah na Amal, yalikuwa sehemu ya serikali iliyoongozwa na waziri mkuu aliyejiuzulu, Saad al-Hariri.

Saad al-Hariri, waziri mkuu aliyejiuzulu kutokana shinikizo la maandamanoPicha: picture-alliance/dpa

Ghasia za leo ni miongoni mwa mbaya zaidi zilizojitokeza tangu kuanza kwa maandamano ya umma tarehe 17 Oktoba, yaliyoitishwa kwa lengo la kupinga ubadhirifu uliokithiri, na tabaka la wanasiasa ambalo walilishutumu kutumia vibaya madaraka kwa zaidi ya miongo mitatu.

Washiriki katika maandamano ya upinzani ambayo hayana kiongozi, walisema maandamano ya leo yaliazimia kuwawekea shinikizo wanasiasa hao, ili waharakishe kupata suluhu katika mkwamo wa kuunda serikali.

Nasrallah asema maandamano yameingiliwa

Kiongozi wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran Hassan Nasrallah amesema maandamano hayo ya umma hivi sasa yanatumia na mataifa ya nje. Amewataka waandamanaji kuweka vuzuizi barabarani, akiwaonya kuwa wanaweza kuitumbukiza Lebanon katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wafuasi wa Hezbollah wamekuwa wakivunja mahema yaliyowekwa na waandamanaji mjini BeirutPicha: picture-alliance/dpa/AP/B. Hussein

Maandamano hayo yameshinikiza kujiuzulu kwa waziri mkuu Saad al-Hariri Oktoba 19, lakini wanasiasa wa Lebanon wameshindwa kukubaliana juu ya serikali mpya, wakati nchi hiyo ikipitia kipindi kigumu kiuchumi na kifedha.

Vuguvugu hili la maandamano ya nchi nzima lilianzishwa na hasira iliyofuatia hatua ya serikali ya kuanzisha kodi mpya, ikiwemo ile juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii kama Whatsapp, na sera ya kubana matimizi iliyopunguza matumizi katika sekta ya umma na malipo ya pensheni, katika juhudi za kurekebisha hali ya uchumi inayozidi kudorora.

ape,dpae

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW